1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kuitambua Sudan ya Kusini haraka

Abdu Said Mtullya16 Juni 2011

Ujerumani imesema itaitambua Sudan ya Kusini kama taifa huru, mara tu baada ya nchi hiyo iliyopiga kura ya maoni kuamua kujitenga na Kaskazini miezi michache iliyopita, kujitangazia uhuru wake hapo tarehe 9 Julai 2011.

https://p.dw.com/p/11b5Y
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido WesterwellePicha: dapd

Msemaji wa serikali ameeleza kuwa Ujerumani itaanzisha uhusiano wa kibalozi na nchi hiyo baada ya uhuru kutangazwa na itafungua ofisi ya ubalozi katika mji mkuu Juba.

Kwa kuitambua Sudan ya Kusini haraka,Ujerumani na nchi nyingine za Umoja wa Ulaya zinakusudia kutoa mchango katika kuleta utengemavu kwenye eneo lote linalopakana na Sudan. Hivi karibuni watu wa jimbo la Sudan ya Kusini walipiga kura ya maoni na kuamua kujitenga na Sudan ya Kaskazini.

Ujerumani imefahamisha juu ya hatua ya kuitambua Sudan ya Kusini muda mfupi tu baada ya kuzindua sera mpya juu ya Afrika inayoweka mkazo katika kukidhi maslahi ya Ujerumani, badala ya kutoa hisani ya msaada wa maendeleo kwa bara hilo. Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle aliitangaza sera hiyo kabla ya kuanza ziara nchini Sudan iliyoahirishwa baadae kutokana na mripuko wa jivu la moto nchini Eritrea .

Kwa mujibu wa sera hiyo mpya wafanya biashara wa Ujerumani watahimizwa kufikia mapatano yatakayojumuisha malengo ya kuweka vitega uchumi na kupatiwa haki za uziduaji wa madini.