1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kujipima nguvu dhidi ya Ufaransa

Bruce Amani
13 Novemba 2017

Joachim Loew ana nafasi ya kuufunga mwaka huu akiwa na rekodi nzuri sana. Kutoipoteza mechi yoyote kwa mara ya kwanza tangu alipochukua majukumu ya kuwa kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani mwaka wa 2006.

https://p.dw.com/p/2nX60
Deutschland DFB-Training in Köln
Picha: picture-alliance/GES/L. Schulze

Lakini hilo halitamzuia kuendelea kukifanyia majaribio kikosi katika mchuano wa mwisho wa mwaka 2017 dhidi ya Ufaransa. Loew atakifanyia mabadiliko kadhaa kikosi hicho cha mabingwa wa dunia katika mchuano wa kesho mjini Cologne dhidi ya Ufaransa, baada ya kutoka sare tasa dhidi ya England uwanjani Wembley.

Na huku akisalia na mechi mbili pekee za kirafiki – dhidi ya Uhispania na Brazil – kabla ya kukichagua kikosi cha awali cha Kombe la Dunia, kufanya majaribio ya hapa na pale ni kitu muhimu kwake. Loew amethibitisha leo kuwa mlinda mlango Kevin Trapp atacheza leo pamoja na wachezaji wa kiungo Toni Kroos na Sami Khedira.

Paris Länderspiel Joachim Löw
Kocha Loew hajapoteza mechi yoyote kwa mwaka huuPicha: picture-alliance/Pressefoto Baumann/H. Britsch

Ujerumani hawajapoteza mchuano kati ya 20 walizocheza tangu walipochapwa 2-0 na Ufaransa katika nusu fainali ya Euro 2016. Wamefuzu kwa kushinda mechi zao zote 10 kati ya 10 katika dimba la Dunia nchini Urusi ambako Loew analenga kuhifadhi taji hilo. Sweden – makamu bingwa wa mwaka wa 1958 – wanalenga kurejea kwenye jukwaa la ulimwengu baada ya kukosa la mwaka wa 2010 na 2014.

Nao Misri ambao tayari wana tikiti ya Kombe la Dunia, walimaliza kampeni yao ya kufuzu kwa kutoka sare ya 1-1 ugenini dhidi ya Ghana hapo jana. Congo ilitoka sare ya 1-1 na Uganda.

Michuano ya kufuzu ya barani Afrika itakamilika leo ambapo senegal ambao tayari wanaelekea Urusi watawaalika Afrika Kusini na Burkina Faso watakutana na Cape Verde.

Morocco siku ya Jumamosi ilifuzu kwa mara ya tano baada ya kuilaza Cote d'Ivoire mabao mawili kwa bila. Ushindi huo ulisababisha vurugu mjini Brussels, baada ya mashabiki wa Morocco kupambana na polisi wakati wakisherehekea. Polisi 20 walijeruhiwa, maduka yakaporwa na magari kuchomwa moto. Tunisia na Nigeria ni mataifa mengine ya Afrika ambayo yatatamba Urusi mwaka ujao.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri:Moahammed Abdul-Rahman