1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kupasha moto misuli na Australia

28 Machi 2011

Ujerumani kesho inapambana na Australia katika mechi ya kirafiki, baada ya Jumamosi kuichapa Kazakhstan mabao 4-0 kwenye mechi za kuwania kufuzu kwa fainali za Ulaya.

https://p.dw.com/p/10jBK
Kocha wa timu ya soka ya Ujerumani Joachim LoewPicha: dapd

Ujerumani katika mechi hiyo ya kesho itawakosa wachezaji wake muhimu akiwemo nahodha, Fhilip Lahm, viungo Sami Khedira na Mesut Ozil, kutokana na majukumu mazito waliyonayo kwenye vilabu vyao.

Kocha wa Ujerumani Joachim Löw alikubaliana na kocha wa Real Madrid Jose Mourinho, kuwaruhusu wachezaji hao viungo, mara baada ya mechi na Kazakhstan.

Ajax Amsterdam Mesut Özil
Mesut OzilPicha: picture-alliance/dpa

Ozil katika mechi hiyo ya Jumamosi alitengeneza magoli mawili, mechi ambayo Joachim Löw hata hivyo alisema ilikuwa si ya ushindani sana.

Ujerumani inaongoza katika kundi la A ikiwa na pointi 15 baada ya kushinda mechi zote tano.

Nao mabingwa watetezi Uhispania ambao pia ni mabingwa wa dunia, kesho wanapambana na Lithuania katika kuwania kufuzu kwa fainali hizo za Ulaya.

Uhispania ambayo inaogoza kundi lake la I Ijumaa iliyopita iliifunga Jamuhuri ya Czech mabao 2-1, na katika mechi hiyo Uhispania inahofu na dimba la uwanja wa Darius and Girenas huko Lithuania, dimba ambalo lina upara kutokana na baridi kali iliyoathiri nyasi zake.

Andreas Iniesta ambaye alifunga bao la ushindi lililoipatia ubingwa wa dunia Uhispania mwaka jana nchini Afrika Kusini, amesema kutokana na picha walizoziona dimba hilo ni kama yale ambayo walicheza walipokuwa watoto, na hilo linawapa shaka.Pia wana shaka na mbinu za wenyeji wao za kulinda zaidi lango lao, huku wakikaba sana.

Nchini Ufaransa, Frank Riberry na Patrice Evra kesho wanatarajiwa kupata mapokezi mabaya kutoka kwa washabiki pale watakaposhuka katika dimba la nyumbani kwa mara ya kwanza, tokea walipofungiwa kutokana na kuongoza mgomo kwenye fainali za dunia nchini Afrika Kusini.

Ufaransa kesho itapambana na Croatia katika pambano la kirafiki.Evra alifungiwa kuichezea timu hiyo mechi tano na Ribbery mechi tatu baada ya kupinga kitendo cha kutimuliwa kikosini kwa mchambuliaji Nicolas Anelka.

Ribbery alisema kuwa anategemea kutakuwa na filimbi nyingi kutoka kwa washabiki ambao wanakadiriwa watakuwa kiasi ya elfu 80.Naye Evra amesema anategemea kuzomewa lakini hicho hakimsumbui.

Mwandishi:Aboubakary Liongo

Mhariri:Othman Miraji