1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kurejesha turathi za Benin

19 Desemba 2022

Waziri wa Mambo ya kigeni wa Ujerumani Annalena Baerbock yuko nchini Nigeria kwa ziara inayojumuisha kurejesha sehemu ya kazi za sanaa zilizoporwa enzi ya utawala wa kikoloni na kutathmani hali ya usalama

https://p.dw.com/p/4LBdx
Nigeria Annalena Baerbock
Picha: Muhammad Al Amin/DW

Bibi Baerbock ambaye aliwasili mjini Abuja siku ya Jumapili, alianza rasmi ziara yake nchni Nigeria jana Jumatatu kwa kulitembelea eneo lenye mzozo wa uasi wa itikadi kali huko kaskazini mwa Nigeria. Ziara yake kwenye kanda hiyo ya kaskazini mashariki mwa taifa hilo ililenga kupata picha ya hali ya usalama.

Mwanasiasa huyo alikwenda hadi Maiduguri, mji mkuu wa jimbo la Borno lililo umbali wa kiasi kilometa 800 kutoka mji wa Abuja.

Eneo hilo ndiyo kitovu cha hujuma za kundi la itikadi kali la Boko Haram. Kundi hilo likisababisha madhila makubwa kwa watu, ikiwemo kufanya mauaji, kuteka nyara raia , kuchoma moto vijiji na kuwalazimisha mamia kwa maelfu ya watu kuyakimbia maakazi yao.

Soma zaidi:Ujerumani yatambua kufanya mauaji ya kimbari Namibia wakati wa ukoloni

Baerbock aliitembelea kambi ambako wapiganaji wa zamani wa Boko Haram na wafuasi wao wanapatiwa mafunzo na msaada mwingine kuwasaidia kurejea tena kwenye maisha ya uraiani baada ya kutoka msituni.

Mradi huo unaofadhiliwa na serikali ya Ujerumani unalenga kubadili maisha yao ya uhalifu, kuwawezesha kiuchumi na kujenga taasisi imara za ulinzi na jamii kama vituo vya polisi, shule na hospitali.

Yote hayo yanatarajiwa kuwazuia watu kuvutiwa na kujiunga na makundi ya itikadi kali.Wapiganaji wa zamani wanapewa mafunzo ya ujuzi na stadi nyingine za maisha mfano wa fani ya useremala, fundi mchundo na mafundi bomba.

Dhima ya ziara ya Baerbock Afrika

Baada ya ziara hiyo huko Maiduguri Baerbock alitarajiwa kurejea mjini Abuja kwa moja ya shughuli muhimu inayobeba dhima ya safari yake barani Afrika.

Großbritannien | British Museum in London
Watu wakitazama kazi za sanaa kwenye jumba la makumbushoPicha: David Cliff/NurPhoto/picture alliance

Mwanadiploamasia huyo atakabidhi kazi 20 za sanaa zilizoporwa enzi ya utawala wa kikoloni. Kazi hizo zinazofahamika na wengi kama "vinyago vya shaba vya Benin" zitakabidhiwa kwa viongozi wa serikali ya Nigeria.

Kurejeshwa kwa vinyago hivyo ni sehemu ya makubaliano yaliyofikiwa mapema mwaka huu baina ya nchi hizo mbili, ambayo yatashuhudia Ujerumani ikiikabidhi Nigeria kazi za kale za sanaa 514.

Soma zaidi:Bunge la Namibia kujadili makubaliano ya fidia ya Ujerumani

Vinyago hivyo ni miongoni mwa turathi chungunzima zilizoibwa mwaka 1897 na kundi la wapelelezi wa ukoloni wa Uingereza kutoka kwenye kasri la ufalme wa Benin, eneo ambalo sasa ni kusini magharibi mwa Nigeria.

Bibi Baerbock anayefuatana na waziri wa utamaduni Claudia Roth na wakuu kadhaa wa majumba ya makumbusho nchini Ujerumani anatumai hatua hiyo itatanua ushirikiano zaidi na Nigeria.

Bearbock:Tunataka kuimarisha ushirikiano

Kabla ya kuondoka mjini Berlin siku ya Jumapili mwanasiasa huyo wa chama cha kijani alisema uamuzi wa kubeba vinyago vya Benin ni sehemu ya kuonesha kwamba Ujerumani inajali na kujutia historia mbaya ya ukoloni barani Afrika.

Frankreich, Paris |  Ukraine Konferenz
Waziri wa mambo ya kigeni Ujerumani Annalena BaerbockPicha: Xander Heinl/photothek/picture alliance

Zaidi ya kazi sanaa 1,100 za iliyokuwa Falme ya Benin zipo kwenye makumbusho karibu 20 kote Ujerumani. Mbali ya madini ya shaba, nyingi ya turathi hizo zilitengenezwa kwa kutumia pembe za ndovu na vipusa.

Soma zaidi:Kwa kiwango gani Ujerumani inautambua uovu wa ukoloni wake?

Kazi zinazorudishwa leo zilikuwa kwenye makumbusho ya miji ya Dresden, Hamburg, Cologne na Stuttgart.

Miongoni mwa kazi zitakazokabidhiwa, ni kiti cha enzi kilichotumika na mtawala wa milki ya Benin Oba Eresoyen mnamo karne ya 18.

Kiti hicho chenye uzito wa kilo 90 kilikuwa kwenye jumba la makumbusho mjini Berlin hadi mwishoni mwa wiki iliyopita.