1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kuwajibika zaidi kimataifa

3 Februari 2014

Marekani na washirika wa Ujerumani wa Ulaya katika Mkutano wa Usalama wa Munich uliomalizika Jumapili(02.02.2014)wameikaribisha ahadi ya serikali ya Ujerumani ya kuwa na sera ya kigeni na usalama imara zaidi.

https://p.dw.com/p/1B1q9
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier katika Mkutano wa Usalama wa Munich wa 2014.
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier katika Mkutano wa Usalama wa Munich wa 2014.Picha: picture alliance/abaca

Katika mkutano wa usalama wa mwaka huu mjini Munich ambapo miaka 11 iliopita waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani aliegeuka kuwa mpinga vita Joschka Fischer alimwambia waziri wa ulinzi wa Marekani Donald Rumfsfeld na hapa nanukuu "samahani sijasidiki juu ya kile kinachoelezwa kuhusu vita nchini Iraq", Ujerumani imeahidi kuwa haitotowa tena jibu la hapana kwa hatua itakazochukuwa katika harakati za kukabiliana na mizozo nchi za nje.

Katika ujumbe wa Rais Joachim Gauck wa Ujerumani katika mkutano huo ambao umeimarishwa na mawaziri wake wa mambo ya nje na ulinzi amesema kwa maoni yake ili kuwa mshirika mzuri Ujerumani inapaswa kujihusisha kwa haraka zaidi , kwa ukamilifu na kwa njia endelevu zaidi katika harakati hizo.

Miongo saba baada ya kushindwa kwa Manazi Ujerumani bado inajikuta ikitanzwa na historia na onyesho la uzalendo hadharani kama vile kupeperusha bendera wakati wa mechi za kandanda ni tukio lililojitokeza hivi karibuni tu.

Rais Joachim Gauck wa Ujerumani katika Mkutano wa Usalama wa Munich wa 2014.
Rais Joachim Gauck wa Ujerumani katika Mkutano wa Usalama wa Munich wa 2014.Picha: picture-alliance/dpa

Wamarekani na washirika majirani wa Ujerumani kwa muda mrefu wamekuwa wakiihimiza nchi hiyo kuchukuwa jukumu la uongozi imara zaidi kwa Ulaya mbali na kutowa maagizo ya kubana matumizi wakati mzozo wa madeni katika kanda inayotumia sarafu ya euro barani Ulaya na kutimiza dhima kubwa zaidi ya kisiasa kwa kutumia ushawishi wake katika uhusiano wa kibiashara.

Ujerumani na harakati za kidiplomasia

Mwishoni mwa juma waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry ameuambia Mkutano huo wa Usalama wa 50 wa Munich ambao ni wa kila mwaka kwamba kuongoza ambalo ni jambo la heshima hakumaanishi kukutana Munich kwa ajili ya majadiliano bali kunamaanisha kujitolea kutowa rasilmali.

Waziri wa mambo ya nje wa Poland Radoslaw Sikorski ambaye hapo mwaka 2011 alisema "Sihofii sana nguvu za Ujerumani kama ninavyohofia kutojihusisha kwa nchi hiyo kwenye harakati". Ameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters mjini Munich kwamba ana furaha kusema kuwa katika mzozo wa Ukraine , Ujerumani imekuwa ikitimiza dhima yake.

Akizungumzia mzozo huo wa Ukraine waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter Steimeir amesema "Hatimae tunatakiwa kuchukuwa hatua,hatutakiwi tu kutangaza kuwa tayari kufanya hivyo bali tunatakiwa kutuma ujumbe na kuchukuwa hatua halisi kumjulisha Rais kwamba kunahitajika kufanyika mabadiliko ya haraka katika hali ya kisiasa nchini Ukraine."

Kiongozi wa upinzani wa Ukraine Vitali Klitschko na waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier wakikutana kwa mazungumzo wakati wa Mkutano wa Usalama wa Munich.
Kiongozi wa upinzani wa Ukraine Vitali Klitschko na waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier wakikutana kwa mazungumzo wakati wa Mkutano wa Usalama wa Munich.Picha: picture-alliance/dpa

Hadi sasa Ujerumani imekuwa ikijishughulisha na mzozo wa Ukraine kwa Kansela Angela Merkel kulaani vikali ukandamizaji wa kutumia nguvu wa Rais Viktor Yanukovych dhidi ya waandamanaji wanaopinga serikali na kuzungumza kwa simu na Rais Vladimir Putin wa Urusi.

Hivi sasa Umoja wa Ulaya na Marekani umekuwa ukiandaa mpango wa msaada kwa Ukraine kwa lengo la kuisadia nchi hiyo katika awamu ya mpito.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/dpa

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman