1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani na Israel zimetia saini ushirikiano wa kijeshi.

Scholastica Mazula17 Machi 2008

Serikali za Israel na Ujerumani zimekubaliana kuongeza nguvu za ushirikiano wa kijeshi na zaidi katika uwekezaji wa miradi ya teknolojia kulingana na matakwa ya pande zote mbili.

https://p.dw.com/p/DQEA
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel akiwa na Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert nchini Israel.Picha: AP

Makubaliano hayo yanafuatia ziara ya siku tatu ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel nchini Israel.

Mmoja wa wajumbe kutoka Ujerumani aliyeongozana na Kansela Merkel, ameyafafanua makubaliano hayo kuwa ni pamoja na kuboresha ulinzi wa kijeshi kwa pande zote mbili za Ujerumani na Israel dhidi ya mashambulizi ya makombora.

Nchi hizo mbili pia zitakuwa zikibadilishana wanajeshi na kupanua mpango wa mabadilisho ulioanzishwa mwaka 1998 ambao unawajumuisha maafisa na wanajeshi kutoka majeshi yao ya majini na angani.

Makubaliano haya yametiwa saini na baina ya Waziri wa ulinzi wa Israel Ehed Barak na mwenzake wa Ujerumani, Franz Josef Jung, na kuuelezea ushirikiano huo kuwa ni sehemu ya makubaliano makubwa ya pande hizo mbili.

Makubaliano hayo ambayo yamekuja kufuatia ziara ya siku tatu ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel yanajumuisha pia ushirikiano katika masuala ya ulinzi wa mazingira, utafiti wa kisayansi na mabadilishano katika masuala ya Utamaduni.

Ziara ya merkel imekuja wakati Israel ikiadhimisha miaka 60 tangu kuanzishwa kwaTaif hilo na pia kukiwa na historia ya Ujerumani kuhusika katika mauaji ya wayahudi wakati wa vita Vikuu vya pili ya dunia.

Kansela Angela Merkel ambaye aliwasili jana nchini Israel, Leo ametembelea kituo cha kumbukumbu ya mauaji ya halaiki ya wayahudi cha Yad Vashem.

Bi Merkel, akiandamana na waziri mkuu wa Israel, Ehud Olmert, na mawaziri wengine wengi wa Israel walipangiwa kuhudhuria ibada ya kuwakumbuka wayahudi millioni sita waliouawa katika vita vikuu vya pili vya dunia.

Kansela ya Ujerumani Angela Merkel,alipowasili mjini Tel Aviv na aligusia yaliyopita na kusema Ujerumani ina wajibu maalum kwa kuwepo kwa Israel.

Kwa upande wake Waziri mkuu Olmert, ameielezea Ujeruamni,miaka 63 baada ya mauaji ya halaiki,kuwa ni mshirika mkubwa wa Israel.

Baadae kansela Angela Merkel na waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert walifunguwa mkutano wa kwanza wa pamoja kati ya Israel na mawaziri saba wa Ujerumani wanaofuatana na kansela Merkel.

Mawaziri kadhaa wa Israel, wakiwemo Waziri wa mambo ya kigeni, waziri wa ulinzi, waziri wa sheria na waziri wa fedha nao pia watafanya mazungumzo tofauti na wenzao wa Ujerumani yote hayo ikiwa ni kuongeza nguvu ya ushirikiano wa pande hizo mbili.

Kesho Kansela Merkel anatarajiwa kulihutubia Bunge la nchi hiyo, ikiwa ni kwa mara ya kwanza kwa Kansela wa Ujerumani kufanya hivyo.

Ni zaidi ya miaka sitini sasa imepita tangu kufanyike kwa mauaji ya halaiki ya wayahudi yaliyofanywa na utawala wa Nazi na kusababisha mauaji ya wayahudi milioni sita.