1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani na masuala ya rushwa

Claudia Hennen6 Juni 2012

Shirika lisilo la kiserikali linalofuatilia rushwa na ufisadi duniani, Transparency International limezichunguza nchi 25 za Ulaya na katika ripoti yake iliyochapishwa leo mjini Brussels, Ubelgiji.

https://p.dw.com/p/158h1
The new headquarters of the European Central Bank, center, rises in front of the skyline of Frankfurt, Germany, Thursday, April 26, 2012. The building is supposed to be finished in 2014. (AP Photo/Michael Probst)
Frankfurt Main SkylinePicha: dapd

Ujerumani inaonekana ikifanya vizuri kwenye ripoti hiyo, ingawa wataalamu wanasema bado kuna mengi yanayostahiki kufanywa na vyama vya siasa, wabunge na raia wa taifa hili kubwa kiuchumi barani Ulaya.

Kwa maana ya uhalifu, basi kansela wa zamani wa Ujerumani, Gerhard Schröder si fisadi. Kwa kila hali chama chake cha Social Democrat hakivunja sheria yoyote katika ule mradi wa bomba la gesi la "Mkondo wa Kaskazini", hadi kusababisha kushindwa uchaguzi wa bunge hapo mwaka 2005. Lakini bado ladha ya kushindwa huko imeendelea kusalia, anasema mkuu wa tawi la Transparency International hapa Ujerumani, Christian Humborg, katika mazungumzo yake na Deutsche Welle.

Kwa kukumbushia tu, mradi wa bomba la gesi kutoka Urusi kupitia Bahari ya Mashariki hadi Ujerumani ulikuwa na utata wa kisiasa, kiuchumi na kimazingira. Akiwa mkuu wa serikali, Schröder aliuunga mkono mradi huo. Mshirika wake kwa upande wa Urusi, alikuwa Rais Vladimir Putin, ambaye kwenye jicho la Schröder alikuwa "mwanademokrasia msafi". Schröder pia alionekana kujitolea moja kwa moja kwenye mradi huo ambao kampuni ya Kirusi ya Gazprom ingelikuwa na hisa za asilimia 51. Kampuni hii, kwa mujibu wa habari za uchunguzi, Jürgen Roth, ilikuwa na muundo na mafungamano na kundi la mafia.

Rais Vladmir Putin wa Urusi
Rais Vladmir Putin wa UrusiPicha: dapd

Lakini jambo hilo linamuhusishaje Schröder na Mradi wa Mkondo wa Kaskazini na ufisadi? Katika mtazamo finyu, linamuhusisha kidogo tu, katika mtazamo mpana linamuhusisha sana. Kwa sababu Transparency International inatafsiri ufisadi kama utumiaji wa nguvu mtu alizokabidhiwa kwa matumizi au manufaa binafsi. Kuutenganisha mpaka baina ya ufisadi wa wazi na ule wa mashaka ni kazi iliyopewa taasisi hii inayoendeshwa kwa fedha za michango tangu mwaka 1995. Kila mwaka Transparency International huchapisha kile kinachoitwa "faharasa ya ufahamu wa ufisadi", na mwaka huu kwa mara ya kwanza wametoa kile wanachokiita ripoti ya heshima kwa mataifa 25 ya Ulaya.

Miongoni mwa taasisi zilizochunguzwa ni pamoja na serikali, mabunge, mahakama na vyama vya siasa. Masuala makubwa yaliyokuwa yakizingatiwa ni hatua gani dhidi ya ufisadi zimechukuliwa, na pia kwa namna gani kuna uwazi na udhibiti kwenye taasisi hizo. Transparency International imeshindwa kuweka viwango vya pamoja vya mafanikio kwenye maeneo hayo kulingana na tafauti ya nchi na nchi na sekta na sekta, kwa mujibu wa Christian Humborg.

"Tulichokuwa hatukufanya ni kuweka orodha ya viwango. Bila ya shaka kuna tafauti. Ujerumani kwa mfano tumeitabiria kuwa na inafanya vyema au vizuri sana katika mfumo wake wa heshima. Ujerumani tayari ina utaraibu mzuri katika eneo hilo. Ila bado kuna nchi nyengine ambazo zinafanya vizuri zaidi kwenye maeneo mengine, kama vile Sweden na Denmark miongoni mwa mataifa ya Scandinavia."

Bado mapungufu yapo Ujerumani

Licha ya kufanya vyema, bado Transparency International inasema kuwa Ujerumani ina mapungufu makubwa katika maeneo mengine, hasa kwenye rushwa miongoni mwa wabunge. Ingawa katika sheria ya Ujerumani, kuna kifungu maalum namba 108e kinachozungumzia "ufisadi na rushwa kwa wabunge", ni makosa ya uuzaji na ununuaji kura tu ndiyo yanayoweza kuadhibiwa kisheria. Mwaka 2005, Umoja wa Mataifa ulipitisha Tamko Dhidi ya Ufisadi, ambalo sasa linatekelezwa kwenye mataifa 160 duniani. Lakini hadi sasa bado Ujerumani haijalitia matendoni tamko hilo, ambalo linataka adhabu kali zaidi.

Ili kulitekeleza Tamko hilo, bunge la Ujerumani lilipaswa kubadilisha sheria. Chama cha upinzani cha Social Democrat kilipeleka rasimu ya sheria hiyo, ambayo inataka wabunge waadhibiwe kwa kutoa kitu, ahadi au uthibitisho unaolingana na rushwa. Hata hivyo, vyama vinavyounda serikali, CDU/CSU na FDP vinapinga mswaada huo.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Reuters

"Tunafanya tuonekane kichekesho katika jukwaa la kimataifa. Kama tunataka kuziambia nchi nyengine la kufanya, lazima kwanza tuoneshe msimamo mkali dhidi ya rushwa. Lakini mabibi na mabwana huko bungeni hawako tayari kufanya mabadiliko ya sheria kukidhi matakwa ya tamko la Umoja wa Mataifa."

Udhaifu mwengine wa Ujerumani unaotajwa na Transparency International, ni utafutaji fedha wa wanasiasa na vyama vya siasa. Kwa mujibu wa sheria za sasa, wabunge wanalazimika kuweka wazi michango ya fedha wanazopokea, ikiwa tu imezidi euro 10,000. Wataalamu wanasema katika wakati kama huu ambapo kuna maelfu ya wapambe kwenye siasa, ni rahisi sana kutumbukiza rushwa na ufisadi kwenye sheria kama hii.

Mwandishi: Marcel Fürstenau (DW Berlin)

Tafsiri: Mohammed Khelef

Mhariri: Josephat Charo