1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani, Uingereza kukutana katika Champions League

25 Novemba 2014

Duru ya Champions League itakayoamua timu gani inachukua nafasi ya kwanza na ipi inachukua nafasi ya pili inaanza wakati timu tatu za Bundesliga zikiumana na tatu za Premier league ya Uingereza.

https://p.dw.com/p/1DsVT
UEFA Champions League Chelsea vs. Schalke 04
Picha: Reuters/Eddie Keogh

Manchester City iliyoko katika nafasi finyu ya kufuzu kuingia katika timu 16 bora za kinyang'anyiro hicho, iko nyumbani ikiisubiri Bayern Munich na Chelsea london inasafiri kuwatembelea Schalke 04 siku ya Jumanne, wakati Arsenal iko nyumbani ikiisubiri Borussia Dortmund siku ya Jumatano.

Kocha wa Schalke 04 Roberto Di Matteo anamatumaini ya kuendeleza rekodi ya nyumbani ya timu hiyo chini ya uongozi wake kuinyima klabu yake ya zamani Chelsea uongozi wa kundi hilo katika mchezo wao kesho Jumanne.

Wakati Borussia Dortmund ambayo inasuasua katika ligi ya nyumbani Bundesliga msimu huu inakabana koo na Arsenal ambayo nayo pia haijafanya vizuri msimu huu katika ligi na hata Champions League. Mchezo huo utakuwa muhimu kwa timu zote kurejesha imani kwa wachezaji na pia mashabiki wa timu hizo.

Wakati huo huo Lionel Messi atawania rekodi nyingine wakati Champions League ikirejea dimbani, baada ya kupumzika kwa wiki tatu.

Mshambuliaji huyo kutoka Argentina atachukua rekodi ya ufungaji mabao katika kinyang'anyiro hicho siku tatu tu baada ya kuweka rekodi ya ligi ya Uhispania La Liga.

Mabao mawili katika ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Ajax Amsterdam Novemba 5 yalimuweka Messi katika kiwango sawa na Raul Gonzalez cha mabao 71. Messi sasa anamatumaini ya kumuacha nyuma Raul wakati Barcelona itakapokuwa wageni wa APOEL nchini Cyprus katika mchezo wa kundi F kesho Jumanne.

Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / ape / rtre
Mhariri: Mohammed Khelef