1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gabriel warnt vor Völkermord an Jesiden

Admin.WagnerD14 Agosti 2014

Naibu Kansela wa Ujerumani Sigmar Gabriel amekutana leo mjini Berlin na wawakilishi wa jamii ya Yazidi waishio nchini Ujerumani, kuzungumzia kitisho cha kuangamizwa ambacho kinawakabili wenzao waishio nchini Irak

https://p.dw.com/p/1Ct9V
Sigmar Gabriel akiupokea ujumbe wa wayazidi mjini Berlin
Sigmar Gabriel akiupokea ujumbe wa wayazidi mjini BerlinPicha: picture-alliance/dpa

Mazungumzo hayo yalionekana kuzigusa hisia za Sigmar Gabriel ambaye akizungumza na waandishi wa habari amesema Jamii ya Yazidi nchini Irak inakabiliwa na kitisho kikubwa cha kuangamizwa kabisa. Wawakilishi wa jamii hiyo wamesema maafa yanayowakabili wenzao nchini Irak hayaelezeki kwa maneno.

Tangu kuibuka kwa kundi la wasuni wenye itikadi kali linalojiita taifa la kiislamu au IS, mamia ya maelfu ya raia katika kanda hiyo wamekuwa wakikimbia, hususan wale ambao sio wa madhehebu ya Suni, wakiwemo wakristo.

Shida isioelezeka

Kiongozi wa ujumbe wa wa-yazidi mjini Berlin Irfin Ortac amesema ni vigumu kwa wakati huu kuelezea kwa uhakika masaibu yaliowafika wenzao nchini Irak, kama vile idadi ya waliouawa au kujeruhiwa. Amesema kwamba kundi la IS huyavamia makundi ya wachache bila huruma yoyote, akiongeza kuwa kwa sasa takribani watu 200,000 wameachwa bila huduma ya maji wa umeme.

Sigmar Gabriel ambaye vile vile ni waziri wa uchumi amesema Ujerumani itatoa msaada wa kibinadamu nchini Irak ikishirikiana na nchi nyingine katika jumuiya ya kimataifa, na itaangalia uwezekano wa kuongeza idadi ya wakimbizi kutoka kaskazini mwa Irak na katika nchi jirani, ambao wanakaribishwa nchini Ujerumani.

Naibu Kansela wa Ujerumani, Sigmar Gabriel
Naibu Kansela wa Ujerumani, Sigmar GabrielPicha: picture-alliance/dpa

Kwa upande wao, wawakilishi wa Yazidi wamesema wangependa wenzao huko Irak wawekewe eneo lenye ulinzi karibu na mji wa Sinjar, badala ya kusaidiwa kulihama eneo lao kwa idadi kubwa. Sigmar Gabriel amesema kuunda eneo kama hilo kimsingi ni jukumu la jeshi la Irak.

Hakuna mpango wa kupeleka vikosi

Amesema kwa sasa suala la kupeleka vikosi vya Ujerumani nchini Irak halifikiriwi, lakini akaunga mkono hatua ya Marekani kuanzisha operesheni za kijeshi dhidi ya wanamgambo wa IS. Sigmar Gabriel amesema kuwa hawezi kusema kwa uhakika kuwa Ujerumani haitaiuzia silaha Irak, akisisitiza kuwa mambo yote lazima yafikiriwe kwanza kwa makini.

Amesema, ''Mnamo siku zilizopita nimesikia mjadala kuhusu kupeleka silaha nchini Irak. Inabidi tuwe makini katika mjadala huo, kwa sababa kwa kawaida baada ya mgogoro silaha hizo hubakia katika nchi zilizopelekwa, na uzoefu wa jumuiya ya kimataifa siku za nyuma, sio mzuri.''

Raia wakikimbia uovu wa wanamgambo wa IS nchini Irak
Raia wakikimbia uovu wa wanamgambo wa IS nchini IrakPicha: Reuters

Nchini Irak kwenyewe, mgogoro wa kisiasa umeendelea kuhusu wadhifa wa waziri mkuu, ambapo Nouri al-Maliki aliyekuwa akiushikilia amegoma kumpisha Haider al-Abadi aliyeteuliwa na rais Fouad Massoum kuwa waziri mkuu mpya. Al-Maliki amevitolea wito vikosi vya usalama vya nchi hiyo kujizuia kuingilia katika mzozo huo.

Huku hayo yakiarifiwa, maelefu ya wakristu wa Irak wameendelea kuikimbia nchi hiyo, wakiepuka uovu wanaotendewa na wanamgambo wa IS. Makao makuu ya kanisa katoliki ulimwenguni, Vatican, yamewatolea wito viongozi wa kiislamu duniani kuulaani uovu huo.

Mwandishi: Sven Pöhle/Gakuba Daniel/RTRE

Mhariri:Yusuf Saumu