1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yachekelea kulipa machungu ya kufungwa na Uingereza mwaka 1966

28 Juni 2010

Bao maridadi lililokataliwa la Frank Lampard,lazusha mjadala mpya juu ya kutumika kwa teknolojia mpya.

https://p.dw.com/p/O4yF
Baadhi ya magazeti nchini Uingereza yaanzisha mjadala kuhusu uwezo wa timu ya taifa baada ya kufungwa na Ujerumani mabao 4 - 1Picha: AP

Historia imejirudia,machungu ya miaka 44 waliyokuwa nayo Wajerumani baada ya Uingereza kufunga bao lenye utata na kuipa ubingwa wa dunia Uingereza mwaka 1966 katika uwanja wa Wembley,yamemalizwa nchini Afrika kusini,na kuzusha mjadala mpya juu ya kutumika kwa teknolojia mpya kwa waamuzi.

Bao ambalo lingekuwa la kusawazisha lililopachikwa wavuni na kiungo bora kwa sasa barani Ulaya, Frank Lampard, likionekana dhahiri kuwa limevuka mstari wa goli, lilikataliwa na mwamuzi kutoka Uruguay, na kuipa ari mpya Ujerumani iliyocharuka na kuivurumisha nje ya mashindano Uingereza.

Katika mechi hiyo iliyokuwa ya vuta n'kuvute hapo jana, Ujerumani imelipa kisasi cha miaka 44, lakini sasa imezua gumzo na shinikizo jipya kwa shirikisho la dimba ulimwenguni,FIFA, juu ya uwezekano wa kukubali kutumika kwa teknolojia mpya kwa ajili ya kuwasaidia waamuzi kutoa maamuzi ya haki.

Mchezaji wa zamani wa Uingereza, Allan Shearer, na kocha wa zamani wa Scotland, Craig Brown, wamelitaka shirikisho hilo kukubaliana na utashi wa wadau wa soka ambao wamekuwa wakionyesha kutoridhishwa kuboronga kwa waamuzi wa soka, kwa kukubali kutumika kwa teknolojia mpya.

Wakati gumzo la bao hilo lenye utata likiendelea, mchezaji aliyekuwa adui wa mashabiki wa soka hapa Ujerumani, mkongwe Miroslav Klose, amerejesha imani yake kwa mashabiki wa soka baada ya kutoa mchango mkubwa katika ushindi wa kihistoria wa mabao 4 - 1 dhidi ya Uingereza.

Klose, ambaye kuteuliwa kwake katika safu ya ushambuliaji hapa Ujerumani kulizua tafrani kubwa kutoka kwa wadau wa soka na hata baadhi ya makocha, ambao walikuwa wakimpigia chapuo mshambuliaji hatari wa Schalke, Kelvin Kuranyi, mpaka sasa Klose ameshapachika mabao 2.

Klose amekuwa hapati nafasi katika kikosi cha kwanza cha Bayern Munich,akiwa amepachika mabao 3 tu, lakini hapo jana nyota yake imezidi kung´ara kimataifa baada ya kufikisha mabao 12, na kufikia idadi ya mabao aliyofunga mfalme wa soka ulimwenguni, Pele wa Brazil, na pia kuikaribia rekodi ya Ronaldo De Lima wa Brazil mwenye mabao 15.

Katika mfululizo wa mechi za leo, Uholanzi itateremka dimbani kupambana na Slovakia, ambapo mashabiki wengi wa soka wameanza kutabiri mechi baina ya Brazil na Chile usiku huu kuwa huenda ikawakutanisha vijana hao wanaocheza soka la kuvutia kukumbana na Brazil katika hatua ya nusu fainali.

Uholanzi, ikiwa imeongezewa nguvu baada ya kurejea kikosini mshambuliaji mahiri wa Bayern Munich, Arjen Robben, wanatarajiwa kukumbana na ushindani mkali kutoka kwa Slovakia,ambayo iliushangaza ulimwengu kwa kuwavua ubingwa Itali katika hatua ya timu 16 bora.

Mwandishi; Ramadhan Tuwa/DPAE/RTRE

Mhariri:Miraji Othman