1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yachukua kiti cha muda katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa

4 Januari 2011

Katika kipindi hicho cha wadhifa wa muda, Ujerumani inapanga kupigania ufumbuzi wa kisiasa kwa mizozo ya kitaifa na kimataifa, ameahidi waziri wa mambo ya nchi za nje, Guido Westerwelle

https://p.dw.com/p/ztIF
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Guido WesterwellePicha: Marcin Antosiewicz

Tangu mapema mwaka huu wa 2011, Ujerumani inakalia kiti cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha miaka miwili. Ujerumani haitoweza kuleta miujiza katika Baraza la usalama. Mfumo wenyewe wa baraza hilo hautoi nafasi ya kufanya hivyo. Mataifa matano makuu yenye kura ya turufu, yaani Marekani, Urusi, China, Ufaransa na Uingereza ndio yenye usemi wa mwisho. Hata hivyo,waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani ana sababu ya kufurahia.

Kwa mara ya mwisho, Ujerumani ilipowakilishwa katika baraza hilo kama mwanachama wa muda, Marekani ilitaka vita vya Iraq vihalalishwe kimataifa. Lakini ilishindwa kwa sababu ya hofu na upinzani wa Ujerumani. Wanachama ambao si wa kudumu wana umuhimu wao, kwani maazimio yanaweza kupitishwa tu kwa wingi wa kura tisa katika baraza hilo lenye wanachama 15.

Mbali na hilo, Ujerumani ina uzito pia katika Baraza la Usalama kwani taifa hilo kubwa tayari lina miundombinu inayohitajiwa kwa jukumu kama hilo. Ukihesabiwa ule wakati ambapo DDR ilikuwemo katika baraza hilo la usalama, basi itakuwa mara ya sita kwa Ujerumani kukalia kiti katika baraza hilo.

Wanadiplomasia wa Ujerumani mjini New York, na hasa balozi Peter Wittig, hawaanzi leo kujifunza siasa zinaendeshwa vipi katika Umoja wa mataifa. Tangu zamani wamekuwa wakichangia kichini chini.

Kwa kuwa mwanachama wa Baraza la Usalama Ujerumani ina nafasi nzuri ya kushadidia, hasa katika suala la mabadiliko ya tabia nchi, mada mojawapo muhimu kabisa hasa kwa visiwa kadhaa. Ujerumani ilipigania nafasi hiyo kwa kutanguliza mbele suala hilo. Kwani katika barua iliyopelekwa mbele ya Umoja wa Mataifa, visiwa kadhaa vilitoa mwito hatua zichukuliwe kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi. Pakizuka kitisho cha mafuriko na ukame, na binadamu wanapolazimika kuyahama maskani yao, basi mabadiliko ya tabia nchi hugeuka kuwa suala la usalama wa kitaifa.

Katika mwaka 2012, Ujerumani itakuwa pia na fursa ya kuzipa msukumo mada nyengine zilizomkaa sana rohoni waziri wa mambo ya nchi za nje, Guido Westerwelle: kuzuia usambazaji wa silaha za nyuklia ulimwenguni na kumaliza mgogoro wa Mashariki ya Kati. Makubaliano ya kulitakasa eneo la Mashariki ya Kati na silaha za kinyuklia yanatazamiwa kufikiwa katika mkutano utakaoitishwa wakati huo.

Lakini hiyo ni mada tete, kwani ulimwengu mzima unaamini kuwa Israel inamiliki silaha za nyuklia, ingawa nchi hiyo haijakubali. Israel pia ni miongoni mwa mataifa matatu ambayo hayakutia saini mkataba wa kutosambaza silaha za nyuklia. Na katika mzozo wa mradi wa nyuklia wa Iran, Ujerumani tayari inajadiliana na mataifa matano yenye kura ya turufu, bila ya mafanikio. Hata hivyo, miaka miwili ijayo Ujerumani itaweza kupiga kura yake yenyewe katika maazimio yote.

Ujerumani itafanya vyema kushauriana na mataifa mengine ya Ulaya yanapohusika masuala yote muhimu. Kwa sababu, kwa kipindi cha karibuni hakuna uwezekano wa kupatikana kiti cha baraza la Usalama kwa ajili ya Umoja wa Ulaya, kama ilivyotajwa katika mkataba wa serikali ya muungano wa CDU/CSU na FDP. Na afadhali hivyo kwa sababu baraza la usalama linabidi kupitisha uamuzi wake haraka pindi mgogoro ukitokea. Umoja wa Ulaya bado haujafikia umbali huo.

Mwandishi:Bergmann,Christina/ZPR/Hamidou Oummilkheir

Mpitiaji: Miraji Othman