1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yagundua akaunti bandia za Wachina

Mohammed Khelef
11 Desemba 2017

Shirika la Ujasusi la Ujerumani (BfV) limechapisha taarifa za watumiaji wa mitandao ya kijamii linaosema ni majina feki yanayotumiwa na majasusi wa Kichina kukusanya taarifa kuhusu maafisa na wanasiasa wa Ujerumani.

https://p.dw.com/p/2p7sp
Symbolbild Social Media & Geld
Picha: picture-alliance/dpa/F. Gabbert

Shirika hilo la ujasusi wa ndani lilichukuwa hatua hiyo isiyo ya kawaida kwa kuwataja majina watumiaji wa mitandao ya kijamii na taasisi bandia ili kuwaonya maafisa wa serikali juu ya kitisho cha kupenyeza taarifa muhimu kupitia mitandao hiyo.

"Majasusi wa Kichina wako kwenye mitandao kama vile Linkedln na wamekuwa wakijaribu kwa kitambo kirefu sasa kukusanya taarifa na kupata vyanzo vya kijasusi kwa njia hii," ikiwemo kusaka taarifa za tabia za watumiaji, mambo wanayopendelea na muamko wao kisiasa, linasema shirika hilo.

Miezi tisa ya utafiti wa shirika hilo umegundua kwamba zaidi ya raia 10,000 wa Kijerumani wamewahi kutafutwa kupitia mtandao wa wasomi wa Linkedln na akaunti bandia ambazo zinajitambulisha kama washauri, wataalamu, wabunifu ama wasomi, lilisema shirika la BfV.

"Inawezekana kuna idadi kubwa zaidi ya watu waliolengwa na akaunti bandia ambazo bado hazijatambuliwa," kwa mujibu wa maafisa wa BfV.

China yakanusha

Akizungumza mjini Beijing leo Jumatatu (11 Disemba), msemaji wa wizara ya nje ya China, Lu Kang, alisema shutuma hizo hazina msingi wowote.

Shirika la Ujasusi wa Ndani la Ujerumani (BfV) linasema zaidi ya Wajerumani 10,000 wameshawasiliana na akaunti bandia za Kichina.
Shirika la Ujasusi wa Ndani la Ujerumani (BfV) linasema zaidi ya Wajerumani 10,000 wameshawasiliana na akaunti bandia za Kichina.Picha: picture-alliance/dpa/O. Berg

"Tunatarajia taasisi sahihi za Kijerumani, hasa idara za serikali, zinaweza kusema na kutenda mambo kwa utaratibu na sio kufanya vitu ambavyo havina faida kwa maendeleo ya mahusiano kati ya pande hivi mbili," alisema Lu.

Miongoni mwa akaunti bandia ambazo taarifa zake zilichapishwa na BfV, ni ya "Rachel Li" anayejitambulisha kama kiongozi wa taasisi ya RiseHR na "Alex Li" anayejitambulisha kama "Meneja Miradi kwenye Kituo cha Utafiti kati ya Ulaya na China." 

Nyingi kati ya akaunti hizo zina picha za vijana warembo wa kike na wa kiume. Picha ya "Laeticia Chen", meneja kwenye "Kituo cha Siasa za Kimataifa na Uchumi" ilitolewa kutoka mtandao wa warembo, anasema afisa wa BfV.

Utafiti wa shirika la habari la Reuters kwa taarifa hiyo umegunduwa kuwa baadhi ya akauti hizo zimeunganishwa na wanadiplomasia wa ngazi za juu na wanasiasa kutoka mataifa kadhaa ya Ulaya. Hata hivyo, haikufahamika mara moja ikiwa pamewahi kufanyika mawasiliano baina yao.

Onyo hili la shirika la ujasusi la Ujerumani linaakisi wasiwasi unaoongezeka barani Ulaya na miongoni mwa mashirika ya kijasusi ya Magharibi juu ya harakati za chini kwa chini za China na pia linafuatia onyo kutoka Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) juu ya uwepo wa jitihada za kuwapa mafunzo raia wa Kimarekani kuyafanyia ujasusi mashirika ya Kichina.

BfV imewaalika watumiaji wa mitandao ya kijamii wenye wasiwasi kuwasiliana na shirika hilo endapo wameona akaunti zinazotiliwa mashaka.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman