1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaikandamiza San Marino 8-0

Sekione Kitojo
12 Novemba 2016

Serge Gnabry aliifungia Ujerumani mabao matatu jana Ijumaa (11.11.2016) katika ushindi wa mabao 8-0 dhidi ya San Marino katika mchezo wa kufuzu kucheza katika fainali za kombe la dunia mwaka 2018 nchini Urusi.

https://p.dw.com/p/2Samt
Fussball WM Qualifikation: San Marino - Deutschland Serge Gnabry
Mchezaji chipukizi wa Ujerumani Serge Gnabry aliyefunga mabao 3.Picha: picture alliance/GES/M. I. Güngör

Serge Gnabry alipachika  mabao  matatu katika  mchezo wake  wa kwanza  na  timu  ya  taifa  ya  Ujerumani, Die Mannschaft, wakati mabingwa  hao  wa  kombe  la  dunia  wakiisambaratisha  San Marino kwa  mabao 8 bila  majibu jana Ijumaa (11.11.2016) katika mchezo  wa  kufuzu kucheza  katika  fainali  za  kombe  la  dunia mwaka  2018  nchini  Urusi.

Mlinzi wa  kushoto Jonas Hektor aliongeza mabao  mawili wakati kocha  Joachim Loew alitimiza  ushindi  wa  michezo 95  kama kocha  wa  timu  ya  taifa  ya  Ujerumani , Die Mannschaft. Ushindi wa  nne  wa  Ujerumani, ikifunga  mabao 16 bila  ya  kufungwa  bao, umeimarisha  uongozi  wake  katika  kundi C.

San Marino , taifa  dogo  sana  linalozungukwa  na   Italia , haikufanikiwa  kupiga mpira  hata  mara  moja  langoni  mwa Ujerumani  na  inaendelea  kubaki  bila  ushindi  katika  michezo 126.

Fußball | WM-Qualifikation | San Marino vs Deutschland
Wachezaji wa Ujerumani Sami Khedira(kushoto) Ilkay Gundogan(kulia) wakishangiria bao la Serge GnabryPicha: picture-alliance/GES/M. Ibo Güngör

Pamoja  na  hayo , San Marino imefanya  vizuri  kuliko  miaka  10 iliyopita , wakati  ilipokandikwa  mabao 13-0  na  Ujerumani  katika mchezo  wa  kufuzu  kucheza  katika  fainali  za  kombe  la  mataifa ya  Ulaya.

Ikicheza  bila  ya  wachezaji  wake kadhaa  wa  timu  ya  kwanza katika  uwanja  ambapo  mvua  kubwa  ilikuwa  inanyesha  , Loew aliteua  wachezaji  wawili  wapya  kwa  ajili  ya  kuanza  mchezo  wa jana  katika  uwanja wa  San Marino mjini Serravalle, na  mmojawao alikuwa  mlinzi Benjamin Henrichs, ambaye  ndie  alianza kuvurumusha  mkwaju  wa  kwanza  golini  mwa  San Marino, na kukosa  kwa  sentimita  chache. Bao  la  kwanza  lilifungwa  na  Sami Khedira , Gnabry  akapachika mabao  mengine  mawili. Gnabry alifunga  bao  la  nne  muda  mfupi  baada  ya  kipindi  cha  pili, baada  ya  Hector  kufunga  bao  la  tatu.

Mabao  mengine  yalifungwa  na Mattia Stefanelli  alijifunga mwenyewe  na  kisha  Kevin Volland  alikamilisha  karamu  ya mabao  kwa  Ujerumani  kwa  kufunga  bao  la  nane. Serge Gnabry , ambaye  hivi  sasa  anachezea  Werder  Bremen  anakuwa mchezaji  wa  pili  kufunga  mabao  matatu  katika  siku  ya  kwanza kuchezea  timu  ya  taifa  tangu alipofanya  hivyo  Dieter Mueller zaidi  ya  miaka  40  iliyopita.

Fußball | WM-Qualifikation | San Marino vs Deutschland
Benjamin Henrichs(kushoto) akipambana na mchezaji wa San Marino Marco BerardiPicha: picture-alliance/GES/M. Ibo Güngör

Katika  mchezo  mwingine mjini  Prague , Michael Krmencik alifunga bao  katika  mchezo  wake  wa  kwanza  na  Jamhuri  ya  Cheki  na Jaromir Zmrhal  aliongeza  bao  la  pili  kwenye  timu  wenyeji, kabla ya  Norway  kupata  bao  la  kufutia  machozi  la  dakika  za  mwisho lililofungwa  na  Joshua King. Ulikuwa  ushindi  wa  kwanza  katika kundi  C kwa  Jamhuri  ya  Cheki ,  ambayo  hivi  sasa  ina  pointi tano   na   katika  nafasi  ya  tano  katika kundi  hilo.

Ireland  ya  kaskazini  ilipata  ushindi  mnono  wa  mabao 4-0  dhidi ya  Azerbaijan, na  timu  hiyo  imesogea  hadi  nafasi  ya  tatu katika  kundi  C.

 

Mwandishi:  Sekione  Kitojo / afpe / rtre

Mhariri: Sylvia  Mwehozi