1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yailaza Bafana Bafana 2:0

7 Septemba 2009

Kinyanganyiro cha tiketi za Kombe lijalo la dunia la FIFA.

https://p.dw.com/p/JU2V
Brazil yaikomea Argentina 3:1Picha: AP

-Ujerumani yaikomea Afrika kusini,wenyeji wa kombe lijalo la dunia mabao 2:0 mjini Leverkusen-

-Katika kanda ya Amerika Kusini,Brazil ni timu ya kwanza kukata tiketi yake ya Kombe lijalo la dunia baada ya kuikomea Argentina mabao 3-1.

-Kanda ya Afrika Ghana ni timu ya kwanza kutoroka na tiketi yake ya Kombe lijalo la dunia

-Kanda ya Ulaya ilikua Holland.

-Wanariadha wa Kenya watamba katika mashindano ya riadha ya Grand Prix huko Rieti,Itali.

Afrika Kusini, wenyeji wa Kombe lijalo la dunia, waliondoka na mabao 2:0 kikapuni kurudi Johannesberg Jumamosi katika mpambano wao wa kupimana nguvu na Ujerumani .

Mabao 2 -moja kutoka kwa mshambulizi mpya wa Ujerumani Mario Gomez na jengine kwa stadi mpya anaetazamiwa kujaza pengo la nahodha Michael Ballack baadae- Mesut Oezil yalitosha kuwapa Bafana bafana darasa la dimba.

Gomez alilifumania lango la Bafana Bafana tayari mnamo dakika chache kabla kipindi cha mapumziko.Ilikua dakika ya 37 ya mchezo. Kipa wa Afrika kusini Fernandez ,anaeichezea klabu ya daraja ya pili ya Bundesliga-Arminia BIelefeld, hakuweza kuzuwia bao hilo lisiingie.Afrika kusini ilijibisha haraka na laiti si kipa wa Ujerumani Rene Adler,basi timu hizo 2 zingeondoka uwanjani kwa mapumziko zikiwa bado suluhu bao 1:1.Katika dakika ya 77 ya mchezo Oezil,mjerumani wa asili ya kituruki alipokea pasi maridadi kutoka kwa mshambulizi wa Taifa Miroslav klose na kutia bao la pili na la ushindi.

Nahodha Michael Ballack alitoka nje ya uwanja dakika 10 zikisalia ili kujipumzisha kwa changamoto halisi ya kuania tiketi ya kombe la dunia keshokutwa jumatano pale Ujerumani itakapocheza na Azerbaijan.

Wakati mpambano kati ya Ujerumani na afrika kusini ulikuwa wa kujiandaa tu kwa changamoto za kombe la dunia, mapambano mengine yalikuwa ya kufa-kupona:

Katika kanda ya Ulaya, Holland ilikua timu ya kwanza kunyakua tiketi yake ya Afrika kusini.Holland inaongoza kundi la 9 ikifuatwa nafasi ya pili na Scotland,Norway.Mazedonia na Iceland.

Ama kanda ya Amerika Kusini ilizusha msisimko mwengine pale wabrazil walipowachezesha watoto wa Diego Maradona samba nyumbani mwao.Kwa mabao 3:1,Brazil imekuwa timu ya kwanza kanda ya Amerika kusini kukata tiketi yake ya Kombe lijalo la dunia nchini Afrika kusini.

Mahasimu wao Argentina wakiongozwa na kocha Maradona, waliduwaa nyumbani.Sasa hatima ya Maradona itaamuliwa ikiwa Argentina iliopo nafasi ya 4 itateleza na kuachwa nyuma na Brazil.

Ama katika kanda ya Afrika,mchezaji wa kiungo wa chelsea Michael Essien alipiga hodi na kuitikiwa katika lango la Sudan na kuifanya Ghana kuwa timu ya kwanza barani Afrika kujiunga na wenyeji Bafana Bafana katika kombe lijalo la dunia. Ilikuwa lakini mchezaji wa kiungo wa Inter milan Sulley Muntari alielifumania kwanza lango la Sudan kabla Essien kuupiga msumari wa pili mlangoni mwao.Kwahivyo, Ghana imejiunga na orodha ya timu kama Brazil,Holland,Japan,Korea ya Kaskazini,Korea ya Kusini zinazojulikana tayari zimekata tiketi zao kwa Kombe la dunia 2010.

Mpambano mwengine wa kukata na shoka Kanda ya Afrika, ni ule uliomalizika sare 2:2 kati ya Nigeria na Tunisia mjini Abuja.Baada ya Super Eagles-Nigeria kuongoza kwa mabao 2:1, bao la Oussama Darragi katika dakika ya mwisho ya 90 liliitilia Nigeria tena kitumbua chake mchanga. Tunisia inaongoza kwa pointi 2 mbele ya Nigeria huku duru 2 tu zikisalia.Mpambano 1 utakua mwezi ujao wa Oktoba na mwengine Nov.

Msumbiji iliwapiku Harambee Stars mjini Maputo, kwa kuwachapa bao 1:0 kati-kati ya kipindi cha pili.Morocco iliondoka sare nyumbani mwa Togo. Simba wa nyika Kamerun, wamepania mara hii kunguruma katika pori la Afrika kusini mwakani.Kwani, mbele ya rais wao mpya wa kutatanisha, Ali Ben Bongo, Kamerun iliichapa Gabon mabao 2:0.

Washindi wa makundi 5 ya kanda ya Afrika wanafuzu kucheza Kombe la dunia litakaloanza juni 11 mwakani hadi Julai 11.Timu 3 za usoni kutoka kila kundi zinafuzu kwa Kombe la Afrika la Mataifa nchini Angola.

Grand Prix huko Rieti,Itali:

Wakati katika mbio za masafa mafupi, majogoo wa Jamaica akina Asafa Powell na Nesta Carter waliwika,mbio za masafa ya kati na marefu , zilitawaliwa na wanariadha wa Afrika na hasa Kenya:

David Lekuta Rudisha alirudisha muda wa dakika 1:42.01ili kunyakua ushindi wa mbio za mita 800.Mwenzake Alfred Kirwa Yego-makamo-bingwa wa dunia mjini Berlin mwezi uliopita, alitokea wapili na bingwa wa dunia wa Berlin, muafrika kusini Mbulaeni Mulaudzi,alibidi i kuridhika na nafasi ya 3 nyuma ya wakenya hao wawili.MBIO ZA MITA 1.500 wanaume pia zilileta ushindi wa wakenya: William Biwott Tanui alimpiku muamerika Leonel Manzano ili kushinda mbio hizo kwa muda wa dakika 3:33.00

Mwenzake Geoffrey Rono alitokea watatu.

MITA 3000 pia ushindi ulikwenda Kenya.Joseph Kitur Kiplimo aliwaongoza wakenya wengine 2 akina Sammy Mutahi na Edwin Cheruiyot Soi kushinda mbio hizo kwa muda wa dakika 7:31.20.

Ushindi pia uliletwa huko Rieti,Itali na wanariadha wakike wa Kenya:

Katika mbio za mita 3000 ,Sylvia Kibet, alitamba kwa kuchukua nafasi ya kwanza kwa muda wake wa dakika 8:43.93.Mwenzake Mercy Cherono ,alitupwa nafasi ya 3 na msichana wa Ethiopia, Kalkidan Gezahgne, aliedhibiti nafasi ya pili.

Wasichana wa Kenya walikamilisha ushindi wao katika mbio za mita 3000 kuruka viunzi pale Ruth Bisibori Nyangau aliponyakua ushindi akifuatwa kama kawaida ya wakenya na wenzake 2 Milcah Cheywa na Gladys Kipkemboi.

Muandishi: Ramadhan Ali/AFPE

Mhariri: M.Abdul-Rahman