1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaisaidia Syria

Josephat Charo29 Agosti 2007

Ujerumani imetoa euro milioni 34 kwa Syria kupitia waziri wake maendeleo, Hedermarie Wieczorek-Zeul, ambaye anafanya ziara rasmi ya siku tatu nchini Syria.

https://p.dw.com/p/CHjW
Heidermarie Wieczoreck-Zeul
Heidermarie Wieczoreck-ZeulPicha: AP

Waziri wa misaada ya maendeleo wa Ujerumani, Heidermarie Wieczoreck-Zeul, akiwa katika ziara rasmi ya siku tatu nchini Syria, amesema Ujerumani imetoa euro milioni 34 kuwasaidia wakimbizi wa Irak walio nchini humo. Kila siku Syria huchukua wakimbizi 2,000 kutoka Irak.

Bi Heidermarie Wieczoreck-Zeul amesema mjini Damascus kwamba idadi hiyo ni changamoto kubwa kwa Syria katika maswala ya kiuchumi na kijamii. Kiongozi ameisifu Syria kwa ukakamavu wake katika kukabiliana na wimbi kubwa la wakimbizi.

´Na jambo moja la mwisho ambalo ningependa kulisema: Tumeona kwa heshima kubwa jinsi nchi yenu inavyojaribu kukabiliana na hali ngumu ya idadi kubwa ya wakimbizi, vipi hali hii livyo ngumu kwa nchi yenu na pia kwa nchi nyengine ambazo zimekabiliwa na wimbi kubwa la wakimbizi.´

Waziri Heidermarie Wieczoreck-Zeul amesema kati ya euro milioni 34 zitakazotolewa na Ujerumani, euro milioni nne zitatengwa kwa ujenzi wa shule ambako watoto wa Irak na Syria watasoma pamoja.

´Na leo tumeamua kwamba hata sisi tunataka kuonyesha ishara ya kusaidia katika ujenzi wa shule kwa kutoa euro milioni nne, ili kusaidia sehemu ya mzigo. Lakini huo pia ni mwito kwa jumuiya ya kimataifa isaidie.´

Wakati wa ziara yake nchini Syria waziri Heidermarie Wieczoreck- Zeul amesema mbali na Ujerumani kuipa Syria euro milioni 34, itashirikiana nayo katika maswala ya maji na kusaidia kilimo cha nchi hiyo kwa kutoa mikopo midogo midogo. Jana kiongozi huyo alizitembelea ofisi za ushirikiano wa kiuchumi na Ujerumani mjini Damascus.

Msaada wa fedha kwa Syria unaboresha uhusiano kati ya Ujerumani na Syria ambao kwa kipindi cha miaka miwili umekuwa ukilegalega. Msaada wa euro milioni 34, umegawanywa katika sehemu ya mkopo mdogo na misaada ya fedha itakayolenga kugharamia miundombinu na miradi ya maendeleo. Msaada huo ni wa kwanza kuwahi kutolewa na Ujerumani kwa Syria tangu mwaka wa 2005 wakati waziri mkuu wa zamani wa Lebanon Rafik Hariri alipouwawa mjini Beirut.

Waziri wa misaada ya maendeleo wa Ujerumani, Heidermarie Wieczoreck-Zeul, na kiongozi wa kitengo cha uratibu nchini Syria, Rayseer al Radawi, walisaini makubaliano juu ya kanuni za msaada huo mjini Damascus. Wakati wa mkutano na waandishi wa habari mjini Damascus, Bi Heidermarie Wieczoreck-Zoel alisema Syria inahitaji kuendelea katika nyanja za kisiasa, kijamii, sheria na utengamano, lakini kazi imekita katika misingi ya ushirikiano na wala sio malumbano.

Mauaji ya Rafik Hariri yaliharibu uhusiano baina ya nchi za magharibi na Syria. Umoja wa Ulaya ulisitisha mazungumzo na Syria kuhusu mkataba wa kiuchumi baada ya mauaji hayo. Uchunguzi wa Umoja wa Mataifa umewashutumu maafisa wa usalama wa Lebanon na Syria kuhusiana na mauaji hayo, lakini Syria inapinga madai hayo.