1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaitunisia misuli Ugiriki

Admin.WagnerD11 Mei 2012

Ujerumani imeionya Ugiriki kuwa isitarajie fedha nyingine za msaada hadi pale itakapofanya mageuzi, kama ilivyokubaliana na washirika wa kimataifa.

https://p.dw.com/p/14tls
Waziri wa mambo ya Nje wa Ujerumani Guido Westerwelle.
Waziri wa mambo ya Nje wa Ujerumani Guido Westerwelle.Picha: dapd

Ujerumani imesema pia kuwa kanda ya sarafu ya Euro itaweza kuhimili endapo Ugiriki itaamua kujitoa kwa ghafla kutoka uanachama wa kanda hiyo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, amesema pamoja na kwamba washirika wa Ugiriki wanataka kuisaidia nchi hiyo kutoka katika mkwamo, Ugiriki nayo inapaswa kuonyesha kuwa inataka kusaidiwa.

Westerwelle amesema Ujerumani inapenda kuona nchi za kanda ya sarafu ya Euro zinaendeleza umoja wao, lakini akaongeza kuwa mustakabali wa Ugiriki ndani ya Umoja huo uko mikononi mwa Wagiriki wenyenwe.

Evangelos Venizelos (kushoto) katika mazungumzo na kiongozi wa chama cha Dimar Fortis Kouvelis.
Evangelos Venizelos (kushoto) katika mazungumzo na kiongozi wa chama cha Dimar Fortis Kouvelis.Picha: picture-alliance/dpa

Kanda yajiandaa kwa kujitoa kwa Ugiriki
Naye Waziri wa Fedha wa Ujerumani, Wolfganga Shäuble, amanukuliwa na gazeti la Rheinische Post leo akisema kuwa Ugiriki lazima itimize wajibu wake wa kifedha ili iendelee kuwemo ndani ya kanda hii inayotumía sarafu ya Euro yenye jumla ya wanachama 17.

Schäuble amesema Kanda ya sarafu ya Euro imejifunza mengi ndani ya miaka miwili iliyopita na wamejenga mifumo imara ya kuzuia mtikisiko endapo Ugiriki itaamua kujitoa kutoka kanda hiyo.

Amesema hatari ya kujitoa ugiriki kwa wanachama wengine imepunguzwa kwa kiasi kikubwa na kwamba kanda ya Euro kwa ujumla imejizatiti kukabiliana na mtikisiko.

Jitihada za kuunda serikali bado zaendelea Ugiriki
Wanasiasa nchini Ugiriki bado wanaendelea na jitihada za kuunda Serikali ya Umoja wa kitaifa  baada ya uchaguzi wa wabunge siku ya Jumapili iliyopita kuvipa ushindi vyama vinavyopinga masharti ya kubana matumizi ya Umoja wa Ulaya kwa Ugiriki ili iokolewe kutokana na mgogoro wa madeni uliyokuwa unatishia uhai wake.

Kulikuwepo na dalili ndogo za mafanikio siku ya Alhamis baada ya kiongozi wa chama cha kisoshalsti, Evangelos Venizelos, kufanikiwa kukishawishi chama kidogo cha Dimar kukubali kuunda serikali.

Kiongozi wa chama cha kihafidhina cha New Democracy Antonis Samaras.
Kiongozi wa chama cha kihafidhina cha New Democracy Antonis SamarasPicha: Reuters

Evangelos pia alikutana na kiongozi wa chama cha New Democracy Antonis Samaras katika jitihada za mwisho kuhakikisha wanaunda serikali. Viongozi wote hawa wanafahamu kuwa kushindwa kufukia muafaka kutailaazimu Ugiriki kufanya uchaguzi mpya, jambo ambalo litahatarisha nafasi ya Ugiriki ndani ya Umoja wa nchi zinazotumia sarafu ya euro.

Hofu ya jitihada zake kutumbukia nyongo
Ujerumani imekuwa mstari wa mbele kuishinikiza Ugiriki itekeleze masharti ya kubana matumizi au ikumbane na athari za ukaidi wake.  Schäuble alisema siyo kwamba Ujerumani inaitishia Ugiriki, lakini alisisitiza kuwa laazima wawe wazi kwa taifa hilo na washirika wengine kwamba hakuna njia nyingine isipokuwa ile waliokubaliana wote.

Waziri wa Fedha wa Ujerumani Wolfgang Schäuble.
Waziri wa Fedha wa Ujerumani Wolfgang Schäuble.Picha: dapd

Ujerumani, taifa lenye uchumi mkubwa zaidi barani Ulaya ndiyo mdhamini mkuu wa ugiriki na imetumia fedha nyingi kuhakikisha Kanda inayotumia sarafu ya euro haitumbukii katika mgogoro wa madeni uliyozikumba nchi kadhaa hadi sasa.

Mwanzoni mwa wiki hii, kanda ya  sarafu ya Euro ilitangaza kuzuia Euro bilioni moja kati ya 5.2 kwa Ugiriki hadi Jumatatu, kutokana na wasiwasi juu ya mustakabali wa siasa za nchi hiyo.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\AFPE\APE
Mhariri: Othman Miraji