1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yajiandaa kukwaruzana na Argentina

11 Julai 2014

Ujerumani inajiandaa kushuka dimbani katika fainali ya Kombe la Dunia katika uwanja wa Maracana Brazil, dhidi ya Argentina huku ikipigiwa upatu kumzidi nguvu mpinzani wake huyo wa Amerika ya Kusini.

https://p.dw.com/p/1CbSA
FIFA WM 2014 Training Löw Schweinsteiger Müller
Picha: picture-alliance/dpa

Katika mechi tatu za mwisho ambazo timu hizo zimekutana, Wajerumani ndio walioibuka washindi. Ujerumani ilishinda katika fainali ya 1990 mjini Rome goli moja kwa sifuri, ikawabwaga Argentina katika robo fainali za Kombe la Dunia 2006 kupitia penalty mjini Berlin, na tena ikawachabanga magoli manne kwa sifuri katika robo fainali miaka minne iliyopita mjini Cape Town, Afrika Kusini. Kabla ya hapo hata hivyo, Argentina iliipiku iliyokuwa Ujerumani ya Magharibi magoli matatu kwa mawili katika fainali ya 1986 mjini Mexico City.

Kocha msaidizi wa Ujerumani Hansi Flick anawaonya mashabiki dhidi ya kuwa na matarajio makubwa. "Bila shaka, wengi wanasema Ujerumani ina uwezo wa kushinda fainali hii, lakini fainali kila mara huwa na sheria zake na mazingira na naamini timu iko imara kabisa na haifikirii kuhusu jukumu hilo. Kama nilivyosema awali, hatuzingatii chohcote ila mchezo huu pekee na sote tunajua, tukikumbuka tulivyocheza dhidi ya Brazil, mengi yanawezekana. Huu ndio mfumo wetu katika mechi hii. Hata hivyo amesema kuwa waanmfahamu vyema mpinzani wao na wamejiandaa vilivyo kwa kivumbi. "Argentina ni timu yenye ulinzi mklai, ambayo inalikinga lango lao vyema na bila shaka Messi ana uwezo mkubwa wa kushambulia. Tunamfahamu mpinzani wetu kwa sababu tumewahi kukutana mara kadhaa katika miaka ya karibuni. Tena, ni fainali, kwa mara ya tatu sasa nadhani ni Ujerumani dhidi ya Argentina".

Porträt - Thomas Müller
Thomas Müller wa Ujerumani analenga kunyakua tuzo ya mfungaji bora wa dimba la Kombe la Dunia 2014Picha: Getty Images

Namna ya kumzuia Messi

Kambi ya Ujerumani uliuangalia kwa makini mchuano wa nusu fainali kati ya Uholanzi na Argentina na hasa namna ambavyo Waholanzi walivyomkaba na kumnyamazisha Lionel Messi kwa kipindi kirefu cha mchezo. Na beki wa Ujerumani Benedikt Howedes analo jibu la Messi. "lazima tumkabe kwa pamoja na wala siyo kwa mapambano ya mchezaji kwa mchezaji. Kama tutacheza vyema dhidi ya Messi, basi hata mchezaji mwenye uwezo wake, hatapata nafasi nyingi. Hilo ndio lengo letu na nitajaribu kutoa mchango wangu".

Fußball WM 2014 Halbfinale Niederlande Argentinien
Mabeki wa Ujerumani wana jukumu la kumnyamazisha mshambuliaji wa Argentina Lionel MessiPicha: Reuters

Mshambuliaji wa Ujerumani Miroslav Klose, aliyeweka rekodi ya kuwa mfungaji wa magoli mengi katika Kombe la Dunia, alipofunga lake la 16 katika mchuano wa nusu fainali dhidi ya Brazil, amesema sasa ameangazia tu fainali ya kesho. "hii itakuwa mechi mpya na tunapaswa kujizatiti tena. Ni fainai, bila shaka na najua namna inavyokera kushindwa katika fainali. Nina matumaini makubwa kuwa mara hii kwa kweli ni wakati wetu na kwamba tunaweza kushinda mechi hii."

Mshambuliaji wa Argentina Sergio Aguero anasema wataucheza mchezo wao kwa sababu shinikizo liko kwa Ujerumani. Kiungo Maxi Rodriguez anasema mechi hiyo ya kesho ni kama ndoto iliyotimia kwa kikosi kizima.

Brazil kupambana na Uholanzi

Brazil inachuana na Uholanzi katika mpambano ambao kila timu haingetaka kushiriki, baada ya kuondolewa katika nusu fainali. Na hata Loius Van Gaal, kocha wa Uholanzi anasema mchuano huu huwa hauna maana na haufai kabisa. Mechi ya kumtafuta mshindi wa tatu kwa kawaida huwa siyo maarufu, na kivumbi cha leo mjini Brasilia kitakuwa tu cha kuwaliwaza wenyeji Brazil ambao bado wana maruweruwe ya kichapo walichopewa na Ujerumani.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA/AFP
Mhariri: Yusuf Saumu