1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yakabiliwa na umasikini wa chakula

Lilian Mtono25 Februari 2016

Kuna idadi isiyo ndogo ya watu ambao wanashindwa kula vizuri kwa sababu ya umasikini wao, wakiwemo wastaafu, wazee, wakimbizi, wasiokuwa na ajira za kudumu na wasio na kazi kwa muda mrefu.

https://p.dw.com/p/1I1Ww
Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) linasema kuna ongezeko la umasikini miongoni mwa watoto kwa asilimia 2.7 nchini Ujerumani.
Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) linasema kuna ongezeko la umasikini miongoni mwa watoto kwa asilimia 2.7 nchini Ujerumani.Picha: Getty Images

Kanisa Katoliki la Mtaa wa Holweide mjini Bonn ni miongoni mwa vituo vingi vinavyotoa msaada wa chakula, matunda na hata nguo kwa wenye mahitaji. Kituo hicho hukusanya mabaki ya vyakula kutoka kwenye maduka ya vyakula na masoko ya bidhaa nyingine za jumla na rejareja.

Mchungaji Michael Mombartz anasema hali ya umasikini imekuwa ikiongezeka katika miaka ya hivi karibuni, jambo linalopunguza kasi ya ugawaji wa chakula.

"Katika kipindi cha miezi 18 iliyopita, watu hawa wenye uhitaji walipata chakula kila Jumatatu ya kila wiki, lakini kutokana na ongezeko la idadi yao, hivi sasa hupata mara moja kila baada ya siku kumi," anasema Mchungaji Mombartz, ambaye amekuwa akisimamia ugawaji wa chakula kwa muda wa miaka 20 sasa.

Watu wengi wanashindwa kupata mlo kamili kwa siku kutokana na kutokuwa na ajira za kudumu na wengine wakiwa hawana ajira kwa muda mrefu. Kituo hicho huandaa pia mikutano kwa watu wasiokuwa na makaazi maalumu na kuwagawia mavazi pamoja na vyakula.

Kituo cha Holweide hutumia kiwango cha pato la mtu mwenye uhitaji ili kufanya mgao huo kuwa sawa. Kulingana na maelezo yake, kulikuwa na ongezeko kubwa la wahitaji mwaka 2014, na tangu wakati huo hali haijabadilika - aidha imeendelea kubaki palepale au kukua zaidi.

Kituo hicho kilianza kugawa misaada ya chakula mwaka 2014 kikiwa na watu 10 tu, lakini sasa kina kiasi ya watu wapatao 120, wengi wa walioandikishwa ni kina mama wanaoishi peke yao, wastaafu na wale wasiokuwa na ajira kwa muda mrefu.

Wakimbizi wakiwania kuingia nchini Croatia katika safari yao ya kuelekea Ujerumani.
Wakimbizi wakiwania kuingia nchini Croatia katika safari yao ya kuelekea Ujerumani.Picha: Getty Images/AFP/E. Barukcic

Ongezeko la wakimbizi na umasikini wa chakula

"Lakini sasa kuna wakimbizi wanaoishi kwenye vyumba vya kupangisha hapa, ambao nao huchukua chakula na kwenda kupika kwenye makazi yao", anasema Mchungaji Mombartz.

Hata hivyo, kuongezeka kwa wakimbizi hao hakujaleta shida yoyote ya msaada, anasema Vesna Tomic, anayesaidia shughuli ya ugawaji chakula kituoni hapo. "Wote wanaelewa kwamba sasa na hawa wapo. Sote tunajua kwamba hawaji hapa kujifurahisha, bali wanakuja kwa sababu wanahitaji msaada."

Mchungaji Mombartz anaona kwamba hali ni tofauti kidogo kwa sasa. Awali watu waliona aibu kufika kituoni hapo, kitu kilichomtia uchungu mwingi, hasa akiwaona wazee waliofanya kazi kwa muda mrefu na sasa wanahitaji msaada lakini wanaogopa kwenda kuomba msaada. "Kwenye nchi kama Ujerumani, hali inahitaji kubadilika", anaongeza.

Hata kwa vijana na watu wenye uwezo wa kufanya kazi, bado hali ngumu huwaandama kwa muda refu. "Kwa bahati nzuri, wakati mwingine watu hupata ajira na kututaarifu, lakini ni wachache sana ambao huweza kupata ajira, nadhani ni kati ya asilimia 5 na 10 tu hufanikiwa kupata ajira za kudumu, hivyo wengi wao hurejea hapa baada ya miezi miwili ama mitatu", anasema Mchungaji Mombartz.

Mwandishi: Nicolas Martin/DW English
Tafsiri: Lilian Mtono
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman