1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yakataa kuwa msuluhishi Syria

9 Oktoba 2013

Rais Bashar al Assad wa Syria ameitaka Ujerumani kusuluhisha mzozo wa Syria lakini serikali ya Ujerumani moja kwa moja imelikataa wazo hilo ambapo baadhi ya wataalamu wa sera wanaamini kuwa ni uamuzi sahihi.

https://p.dw.com/p/19wbB
Rais Bashar al-Assad wa Syria.
Rais Bashar al-Assad wa Syria.Picha: Reuters

Katika mahojiano marefu na toleo la hivi karibuni kabisa la jarida mashuhuri la Ujerumani la "Der Spiegel" Assad amekataa kuwajibishwa na matukio yoyote ya umwagaji damu unaotokea nchini Syria na kudokeza kwamba atakuwa tayari Ujerumani iwe msuluhishi katika mzozo unaondelea nchini mwake.

Amekaririwa akisema bila ya shaka angependelea kuona wajumbe kutoka Ujerumani wanakwenda Syria kuangalia na kujadili hali halisi ya mambo na kwamba kwenda nchini Syria hakumaanishi kwamba wanaiunga mkono serikali ya nchi hiyo bali kwenda kwao huko wataweza kufanya kitu,kuzungumza,kujadili na kushawishi. Ameongeza kusema kwamba iwapo watu wanafikiria kuitenga nchi hiyo,wataishia kwa kujitenga wenyewe na huo ndio ukweli wa mambo.

Suluhisho kupitia Umoja Mataifa

Lakini waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle amelikataa pendekezo hilo.Amesema mwenye jukumu hilo ni Lakhdar Brahimi akiwa kama mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa na wanaunga mkono kikamlifu juhudi zake kutafuta suluhisho la kisiasa nchini humo. Akizungumza wakati akiwa katika ziara ya Afghanistan hapo Jumatatu waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani pia amemshutumu Assad kwa kukanusha kufanya mashambulizi ya gesi za sumu kwenye kiunga cha Damascus hapo mwezi wa Augusti. Amesema kwa hakika suala la kukanusha na kubishana ni mambo yasiofaa katika kutafuta suluhisho la amani nchini Syria.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle.
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle.Picha: picture-alliance/dpa

Kwa mujibu wa mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati Guido Steinberg wa Taasisi ya Masuala ya Kimataifa na Masuala ya Usalama uamuzi wa Ujerumani kukataa dhima ya kuwa msuluhishi katika mzozo huo wa Syria ni uamuzi sahihi.Mtaalamu huyo amesema wale wote wanaotafuta suluhisho la kisiasa nchini Syria wanapaswa kumuunga mkono Lakhdar Brahimi na amesisitiza kwamba mataifa binafsi hayapaswi kujichukulia hatua za upande mmoja za kutimiza dhima ya usuluhishi.Isitoshe amesema Ujerumani yenyewe hivi sasa kisiasa iko katika njia panda kwani Kansela Angela Merkel bado yuko katika mchakato wa kuunda serikali ya mseto baada ya kushinda katika uchaguzi mkuu. Amesema kwa hivi sasa hakuna anayejua nani atakuwa waziri mpya wa mambo ya nje.

Kuepuka kiburi cha kisiasa

Hata Profesa Thomas Jäger wa Masuala ya Kimataifa na Sera za Umma katika Chuo Kikuu cha Cologne nchini Ujerumani anaunga mkono uamuzi huo wa serikali ya Ujerumani.Ameiambia DW kwamba hususan kwa vile Urusi na Marekani zinatafautiana katika suala la mzozo wa Syria kwa hiyo iwapo Ujerumani itaingilia kati kuwa msuluhishi kati ya Marekani na Urusi jambo hilo litaonekana kuwa ni kiburi cha kisiasa. Kwa mujibu wa Jäger kuchukuwa dhima ya msluhishi pia kutatowa ishara ya balaa kwa washirika wa Ujerumani.Jäger anaamini kwamba sio tu Ujerumani bali Ulaya kwa jumla inapaswa kujizuwiya kuchukuwa hatua ya aina hiyo.Ameongeza kusema nchi za Ulaya zimejituma mno kupindukia uwezo wake katika kujaribu kutafuta suluhisho la mzozo huo au hata kutowa mchango wa maana katika kutafuta ufumbuzi.Amesema huu sio mzozo wa sera ya kigeni ambao wanaweza kuushughulikia.

Sera ya wakimbizi ni mwelekeo sahihi

Hata hivyo Steinberg amesisitiza kuwa Ujerumani inaweza na inapaswa kujishughulisha katika suala la mzozo huo wa Syria.Amesema"Nafikiri Wajerumani wanapaswa kuchukuwa hatua kwa njia fulani kuwaonyesha Wasyria kwamba sio kweli kama vile mara nyengine inavyoonekana kwamba mzozo huo sio jambo muhimu kwa Wajerumani.Ni vizuri kuchukuwa hatua kwa kuanzia katika fani ya sera ya wakimbizi." Kama hatua ya kwanza anapendekeza Uturuki inabidi ifunguwe mipaka na kukubali kupokea wakimbizi zaidi na hapo Ujerumani inaweza kutowa msaada wa vifaa na wa fedha wakati huo huo ikizingatiwa kwamba Lebanon na Jordan pia zinahitaji msaada.

Wakimbizi wa Syria wakiwasili katika mpaka wa Uturuki.
Wakimbizi wa Syria wakiwasili katika mpaka wa Uturuki.Picha: Bulent Kilic/AFP/Getty Images

Steinberg anasema nchi hizo zinakabiliwa na tishio la kupoteza utulivu wa kisiasa kutokana na kutowa hifadhi kwa idadi kubwa ya wakimbizi wa Syria.Na kwa hatua ya pili Umoja ya Ulaya inabidi nao ukubali kupokea wakimbizi zaidi ambapo hapo tena Wajerumani wanaweza kutafuta njia nyengine ya kutowa mchango. Jäger anaamini utowaji wa msaada wa kibinadaamu ni njia sahihi ya kufuatwa na Ujerumani ambapo serikali inaweza kusaidia kupunguza taathira za vita vya wenyewe kwa wenyewe katika kanda hiyo.Pia inaweza kusaidia kusukuma mbele mazungumzo kufikia aina fulani ya suluhisho.Anasema kujenga mawazo ya kufanikisha hilo kutategemea hatua zitakazoweza kuchukuliwa na serikali.

Mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati Guido Steinberg.
Mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati Guido Steinberg.Picha: DW

Mwandishi:Günther Birkenstock/Mohamed Dahman

Mhariri: Yusuf Saumu