1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yakaza sheria za COVID-19 kwenye mabaa na migahawa

John Juma
8 Januari 2022

Wateja kwenye mabaa na migahawa kote nchini Ujerumani watalazimika kuthibitisha kuwa wamepata dozi ya tatu ya chanjo au waonyeshe cheti cha vipimo kuthibitisha kuwa hawajaambukizwa ndipo waruhusiwe ndani kuhudumiwa.

https://p.dw.com/p/45HYz
Berlin Impfung in der Sage Beach Bar und Restaurant
Picha: Markus Schreiber/AP/picture alliance

Masharti hayo mapya yamejiri baada ya mkutano wa Ijumaa, kati ya kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na wakuu wa majimbo yote 16.

Akiyatetea masharti hayo, Scholz alisema anafahamu ni magumu lakini yanahitajika ili kusaidia kuzuia au kudhibiti maambukizi hata katika siku za baadaye kuliko jinsi hali ilivyo kwa sasa.

Scholz alisisitiza umuhimu wa kupata dozi ya tatu ya chanjo ambayo ni nyongeza, akisema ndiyo kinga bora zaidi dhidi ya aina ya kirusi cha Omicron.

Serikali mablimbali duniani zawahimiza raia wake kupata chanzo ya ziada

Scholz pia alifupisha muda ambao watu watahitajika kukaa karantini kutoka siku 14 hadi siku 10. Muda huo huweza kufupishwa hata zaidi ikiwa mtu haonyeshi dalili ya kuambukizwa na vipimo pia vithibitishe kuwa hajaambukizwa.

Wafanyakazi katika sekta muhimu zaidi mathalan wahudumu wa afya, maafisa wa polisi na watoao huduma za dharura wataruhusiwa kukaa karantini hata siku chache zaidi.

Kansela wa Ujerumani (kushoto) akikutana na wakuu wa majimbo 16 ya Ujerumani mjini Berlin kuhusu sheria mpya za kudhibiti maambukizi ya COVID-19 Ijumaa 7, 2022.
Kansela wa Ujerumani (kushoto) akikutana na wakuu wa majimbo 16 ya Ujerumani mjini Berlin kuhusu sheria mpya za kudhibiti maambukizi ya COVID-19 Ijumaa 7, 2022.Picha: John MacDougall/AP/picture alliance

Wale ambao hawajachanjwa kuendelea kukabiliwa na vikwazo

Kulingana na masharti hayo mapya, watu ambao wameshapata dozi ya tatu ya chanjo hawatahitajika kukaa karantini hata wakijumuika na mtu yeyote aliyeambukizwa COVID-19.

Sheria inayosisitiza kuwa watu 10 pekee ndio wanaruhusiwa kujumuika pamoja ikiwa wamechanjwa au wamepona COVID-19, itaendelea kutekelezwa. Wale ambao hawajachanjwa wataendelea kukabiliwa na vikwazo vikali zaidi.

Soma: Wasiochanjwa Ujerumani kuzuiwa baadhi ya huduma muhimu

Mkutano huo wa kwanza wa Olaf na wakuu wa majimbo katika mwaka 2022, ulijiri mnamo wakati serikali ya Ujerumani ikiimarisha kampeni ya chanjo ili kukabili ongezeko la maambukizi kutokana na kirusi cha Omicron.

Kwa sasa kampeni ya upokeaji chanjo nchini Ujerumani inazidi kushika kasi baada ya sikukuu za Krismasi na mwaka mpya. Hadi sasa asilimia 71 ya watu Ujerumani wameshapokea dozi mbili za chanjo.

Je hali ya COVID ikoje Ujerumani?

Serikali ya Ujerumani inadhamiria kuwachanja watu milioni 30 ifikapo mwisho wa Januari ili kufikisha jumla ya asilimia 80 ya watu waliopokea chanjo dhidi ya COVID-19.
Serikali ya Ujerumani inadhamiria kuwachanja watu milioni 30 ifikapo mwisho wa Januari ili kufikisha jumla ya asilimia 80 ya watu waliopokea chanjo dhidi ya COVID-19.Picha: Markus Schreiber/AP/picture alliance

Idadi ya watu waliochanjwa dhidi ya COVID nchini Ujerumani ni asilimia 71.5. Aidha asilimia 40.9 tayari wamepokea dozi ya tatu ya chanjo.

Hata hivyo idadi hiyo ni chini ikilinganishwa na hali ilivyo katika mataifa mengine ya Ulaya.

Serikali ya Scholz imejiwekea lengo la kuwachanja watu milioni 30 ili kuhakikisha asilimia 80 ya idadi jumla ya watu wamepokea chanjo ifikapo mwisho wa Januari.

Mnamo Alhamisi, Ujerumani ilirekodi maambukizi mapya 64,340 ya virusi vya corona. Hayo ni kulingana na taasisi ya Ujerumani inayopambana na maradhi ya kuambukiza Robert Koch.

Idadi ya vifo pia iliongezeka kwa watu 443 hivyo kusababisha idadi jumla ya watu waliokufa Ujerumani kutokana na janga la COVID-19 kufikia 113, 368.

(DW, AP, DP, RTR)