1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yakubali kulegeza sheria za uraia kwa wahamiaji

Bruce Amani
23 Agosti 2023

Baraza la mawaziri la Ujerumani limeidhinisha leo mipango ya kufupisha utaratibu wa uraia kwa wahamiaji na kuwaruhusu watu zaidi kupata uraia pacha.

https://p.dw.com/p/4VVT4
Pasipoti
Hati ya kusafiria ya Ujerumani(Pasipoti)Picha: Inga Kjer/photothek/imago Images

Baraza la mawaziri la Ujerumani limeidhinisha leo mipango ya kufupisha utaratibu wa uraia kwa wahamiaji na kuwaruhusu watu zaidi kupata uraia pacha.

Chini ya kanuni mpya zinazopendekezwa, ambazo lazima ziidhinishwe na bunge, kupewa uraia nchini Ujerumani kutawezekana baada ya miaka mitano badala ya miaka nane kama ilivyo kwa sasa.

Wale ambao hasa wamejumuishwa vyema katika jamii na wanazungumza Kijerumani kizuri kabisa wataweza kupata uraia baada ya miaka mitatu tu. Raia wapya wanaotarajiwa watahitajika kuonyesha kuwa hawategemei msaada wa serikali, ijapokuwa sharti hilo litategemea na mhusika.Sherehe za kukabidhiwa wageni uraia wa Ujerumani

Rasimu ya sheria hiyo pia itafungua mlango kwa watu zaidi kuwa na uraia pacha, ikiwemo wale kutoka jamii kubwa ya Kituruki nchini Ujerumani. Taifa hilo kubwa kiuchumi barani Ulaya pia linajaribu kuwavutia wafanyakazi wa kigeni ili kuziba uhaba mkubwa wa wafanyakazi, na inadhamiria kujiweka kuwa kivutio kikubwa.