1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yapata kiti Baraza la Usalama.

Sekione Kitojo13 Oktoba 2010

Yasema itatoa mchango wake kama inavyotakikana

https://p.dw.com/p/PdEZ
Waziri wa mambo ya nchi za nje Guido Westerwelle kwenye Umoja wa mataifa.Picha: picture alliance/dpa

Baada ya Kampeni kali, Ujerumani ilifanikiwa kupata kiti cha miaka miwili, japo si cha kudumu kwenye Baraza la  Usalama la Umoja wa Mataifa. Ujerumani ilikuwa inashindana na Ureno na Canada kujaza viti viwili vinavyotengewa mataifa ya Magharibi katika Baraza hilo lenye ushawishi mkubwa- na ikafanikiwa kupata kura 128 kutoka kwa wanachama 192 wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa. Na saa kadhaa baada ya ushindi wake huo, Ujerumani kupitia waziri wake wa mambo ya nje Guido Westerwelle ikasema itapigania kupatikana mageuzi katika Baraza hilo la Usalama.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani ambaye alifanya kazi kubwa mjini New York kutafuta uungwaji mkono ili  Ujerumani ipate nafasi ya kuhudumu katika baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa- alikuwa ni mwenye furaha akiwaambia waandishi wa habari kwamba ushindi wa Ujerumani, ni jukumu kubwa na ni ishara kuwa Jumuiya ya kimataifa ilikuwa na imani na nchi hiyo.

Westerwelle pia aliongeza kwamba wakati umewadia kuanzisha majadiliano ya kuufanyia mageuzi Umoja wa Mataifa ili uwe chombo kinachowanufaisha watu wote.

Alisema Ujerumani itatoa mchango wake katika Baraza hilo la Usalama na hasa katika masuala kama ya amani, usalama, maendeleo, mabadiliko ya hali ya hewa pamoja na kuhakikisha mataifa yanaachana na silaha za nuklia.

Kwa upande wake Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alisema ni heshima kubwa kwa Ujerumani kupewa nafasi ya kuhudumu katika baraza la usalama la Umoja huo na kwamba watahakikisha Ujerumani inatoa mchango kama inavyotakikana.

Angela Merkel in Rumänien
Kansela Angela Merkel .Picha: picture-alliance/dpa

Mbali na Ujerumani India, Afrika Kusini na Ureno ndio mataifa mengine yalifanikiwa pia kupata nafasi katika baraza hilo na watahudumu kwa miaka miwili. Canada ambayo ilikuwa inamenyana na Ujerumani na Ureno kujaza nafasi mbili zinazotengewa mataifa ya Magharibi ilipata pigo ilipolazimika kujiondoa kutoka katika kinyanganyiro hicho iliposhindwa na kupata uungwaji mkono- na nafasi hiyo ikachukuliwa na Ureno.

Kuna wanachama watano wa kudumu wa baraza la usalama la umoja wa mataifa ambao wana kura ya turufu- na wanachama hawa ni Marekani, Uingereza, Ufaransa, Urusi na China. Kisha kuna wanachama wengine kumi ambao sio wa kudumu na hawana kura ya turufu. Mataifa matano katika baraza hilo la usalama lenye wanachama 15, huchaguliwa kila mwaka, kuhudumu kwa kipindi cha miaka miwili.

Wanachama hao wapya waliochaguliwa jana, watachukua nafasi ya mataifa ya Japan, Austria, Uturuki, Mexico na Uganda.  Kwa upande wao, Afrika Kusini kupitia Waziri wake wa mambo ya nje Maite Nkoana Mashabane alisema Afrika Kusini itayapa kipau mbele masuala yanayolenga Afrika na itashirikiana na Umoja wa Afrika kupaaza sauti yao katika baraza hilo la usalama. Alisema pia Afrika Kusini itaunga mkono suala la kuondolewa kwa mashtaka ya mauji ya halaiki dhidi ya Rais wa Sudan Omar El Bashir.

Uingereza kupitia balozi wake katika umoja wa Mataifa, ilisema baraza la usalama la umoja wa mataifa limepata uso mpya, kupitia wanachama wapya waliochaguliwa jana.

Mwandishi: Munira Muhammmad/ AFPE

Mhariri: Sekione Kitojo.