1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yapata kiti kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

13 Oktoba 2010

Baada ya kampeini kubwa, Ujerumani yapata kiti katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kwa miaka miwili.

https://p.dw.com/p/Pd1F
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, mjini New York.Picha: cc-by-sa-Patrick Gruban

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle amesema wakati umewadia kulifanyia mageuzi Baraza la Usalama la umoja wa Mataifa. Westerwelle alisema hayo saa kadhaa tu baada ya Ujerumani kufanikiwa kupata kiti, ingawa sio cha kudumu kwenye Baraza hilo la Usalama la Umoja wa Mataifa.  Wanachama wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa walipiga kura na kuipa Ujerumani nafasi katika baraza hilo la usalama kwa muda wa miaka miwili kuanzia mwaka ujao wa 2011 hadi 2012.  India, Afrika Kusini, Colombia na Ureno pia zilichaguliwa kama wanachama wasiodumu wa baraza hilo la usalama. Mbali na wanachama watano wa kudumu wa baraza hilo la usalama, nyadhifa zingine kumi katika baraza hilo lenye ushawishi mkubwa hupewa mataifa yanayowakilisha kanda kadhaa, huku wanachama wa tano wakichaguliwa kila mwaka. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alisema ilikuwa heshima kuu kwa Ujerumani kupewa kiti katika baraza hilo la usalama. Wakati huo huo, wanasiasa wengine wa Ujerumani akiwemo, Waziri wa zamani wa mambo ya nje Klaus Kinkel wamesema Ujerumani inafaa kupewa kiti cha kudumu katika baraza la usalama kama ishara ya umuhimu wa nchi hii katika jukwaa la kimataifa.