1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yashambulia uamuzi wa General Motors

Sekione Kitojo4 Novemba 2009

Serikali ya Ujerumani imeushambulia uamuzi wa kampuni ya kuunda magari ya General Motors kuing'ang'ania kampuni yake tanzu ya Opel, wakati wafanyakazi wanapanga kufanya mgomo.

https://p.dw.com/p/KOWO
Waziri wa uchumi wa Ujerumani kutoka chama cha FDP Rainer Bruederle.Picha: AP

Serikali ya Ujerumani imeshambulia leo Jumatano uamuzi wa kampuni ya kuunda magari ya General Motors kuing'ang'ania kampuni yake ya Opel wakati wafanyakazi waleeleza wasi wasi wao kuhusiana na uwezekano wa kufanyika mageuzi makubwa kwa kampuni hilo ambalo limeendelea kupata hasara.

Wafanyakazi pia wamepanga kufanya mgomo kupinga uamuzi huo wa GM wa kutotaka kuuza kampuni yake hiyo tanzu tawi la Ulaya.

Uamuzi wa General Motors haukubaliki kabisa, waziri wa uchumi wa Ujerumani Rainer Bruederle amewaambia waandishi habari siku moja baada ya kampuni hilo la kuunda magari la Marekani kufuta mpango wa kuiuza kampuni yake tanzu ya Opel kwa kampuni la Canada la kuunda vipuri Magna pamoja na washirika wao wa Urusi Sberbank.

General Motors ndio inawajibika binafsi na maendeleo yake, na Opel imo katika njia ya mpango wake wa mageuzi. Hatutaki kuiweka General Motors katika mbinyo.

Serikali ya Ujerumani imesema katika taarifa usiku wa jana kuwa inatarajia GM kurejesha kiasi cha Euro bilioni 1.5 kilichotolewa kama mkopo kwa kampuni hilo.

Serikali ya Ujerumani ilipigia debe kwa kiasi kikubwa kuuzwa kwa asilimia 55 ya hiza katika kampuni hilo la kuunda magari, ambalo kampuni ya Magna ilisema haitafikia katika kufunga viwanda vya Ujerumani licha ya kuwa maelfu kadha ya nafasi za kazi zitapotea.

Roland Koch, mkuu wa serikali ya jimbo la Hesse nchini Ujerumani , ambako Opel ina kiwanda chake kikuu , amesema kuwa ameshtushwa na wakati huo huo amekasirishwa kuwa juhudi zilizofanywa kwa muda wa mwezi mzima kutafuta suluhisho bora kwa ajili ya Opel zimeshindwa katika makao makuu ya GM. Mtaalamu wa masuala ya GM anayeandikia katika gazeti la Detroit Free Press Justin Hyde amesema kuwa Opel ni muhimu kwa GM.

Opel ni sehemu muhimu ya kibiashara sio tu kwa sababu ya mauzo, lakini pia kutokana na maendeleo, utafiti na teknolojia.

Ujerumani ambako Opel inawaajiri kiasi cha wafanyakazi 55,000 imetoa ahadi ya Euro bilioni 4.5 kutoka serikalini kwa kampuni ya Magna na Sberbank baada ya kufikiwa kwa makubaliano ya awali na GM mwezi Septemba.

Tangazo hilo la GM limekuwa pigo kubwa kwa kansela wa Ujerumani Angela Merkel wakati akiwa katika ziara nchini Marekani na kuyahutubia mabaraza mawili ya Congress.

Nchini Ujerumani viongozi wa vyama vya wafanyakazi wameingiwa na wasi wasi mkubwa kutokana na uamuzi huo. hatua ya pili itakuwa kwa General Motors kuzirubuni serikali za mataifa ya Ulaya pamoja na wafanyakazi kugharamia mpango ambao hauwezekani wa mageuzi katika kampuni hilo, mkuu wa kamati ya wafanyakazi wa Opel Klaus Franz amesema katika taarifa.

Wafanyakazi katika kampuni ya Opel wamepanga kutofanyakazi wakipinga uamuzi huo wa General Motors. Mkuu wa chama kikuu cha wafanyakazi wa viwanda vya vyuma IG Metal tawi la Frankfurt, Armin Schild amesema kuwa hatua hiyo ya wafanyakazi wa Ujerumani itazusha maandamano katika bara zima la Ulaya.

Nao wafanyakazi katika kiwanda cha Opel nchini Hispania wameeleza kushangazwa kwao kuhusiana na uamuzi huo wa General motors.

Lakini vyama vya wafanyakazi vya Uingereza vimeikaribisha hatua hiyo ya GM kutoiuza kampuni yake tanzu tawi la Ulaya, lakini serikali imesema inatafuta mazungumzo ya haraka na GM kuhusu hali ya baadaye ya kampuni yake ya Vauxhall.

Mwandishi Sekione Kitojo/DPAE/AFPE/APE

Mhariri : Mohammed Abdul Rahman