1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yashinda Eurovision 2010 mjini Oslo

Oumilkher Hamidou31 Mei 2010

Msichana wa miaka 19 wa Ujerumani,Lena aibuka na ushindi wa mashindano ya nyimbo barani Ulaya kwa nyimbo yake aliyoipa jina "Satellite" na kuirejesha Ujerumani kileleni,miaka 28 baada ya "Ein bisschen Frieden"

https://p.dw.com/p/Ndcj
Lena baada ya kutangazwa mshindi wa Eurovision 2010 mjini OsloPicha: EBU

Mashindano ya waimbaji nyota barani Ulaya,"Eurovision" yamemalizika kwa ushindi wa msichana wa miaka 19 wa kutoka Ujerumani na nyimbo yake aliyoiita Satellite.Lena ni wa pili kushinda mashindano hayo tangu yalipoanzishwa miaka 55 iliyopita.Kabla ya hapo alikua Nicole aliyeibuka na ushindi wa mashindano hayo mnamo mwaka 1982.

Ujerumani nzima ilishangiria, msichana mdogo wa miaka 19,Lena Meyer-Landrut alipojipatia ushindi wa mashindano ya nyimbo barani Ulaya-Eurovision jumamosi usiku mjini Oslo.Kwa mujibu wa gazeti la Die Welt toleo la leo,rais wa shirikisho Horst Köhler na mkewe walikua pia miongoni mwa waliopendezewa sana na bashasha za msichana huyo mdogo.Kansela Angela Merkel pia amempongeza Lena na kumtaja kuwa "kitambulisho cha Ujerumani changa."

Jana mchana Lena alirejea nyumbani mjini Hannover akipokelewa kama mwimbaji nyota baada ya ushindi wa Grand Prix mjini Oslo.Maelfu ya mashabiki walimashangiria katika uwanja wa ndege.

Lena aliduwaa na hakuwa na la kusema isipokuwa kuwaomba mashabiki wake wakimbie mvua na warejee nyumbani.

"Nyie,hamuoni mvuwa,rejeeni nyumbani,ahsanteni"

Lena Meyer-Landrut amejikingia jumla ya pointi 246 akimpita kwa zaidi ya pointi 70 muimbaji wa kutoka Uturuki aliyekamata nafasi ya pili.

Lena amejipatia pointi 12 mara tisaa-idadi kubwa kabisa ya pointi muimbaji anazoweza kujipatia katika mashindano hayo ya nyimbo barani ulaya.Nchi tano tuu kati ya 39 zilizokua na haki ya kupiga kura ndizo zilizomtoa patupu msichana huyo.Haiba yake pengine ndio iliyowavutia zaidi wapiga kura.

Puzzle-Bild Deutschland Ankunft von Lena Dossierbild 1
Mashabiki zaidi ya elfu nne wamekusanyika mbele ya ofisi ya mewa wa jiji la Hannover kumshangiria Lena Meyer-LandrutPicha: picture alliance/dpa

Hii ni mara ya pili kwa Ujerumani kuibuka na ushindi wa mashindano haya makubwa ya nyimbo barani Ulaya-Eurovisioni,tangu yalipoanzishwa miaka 55 iliyopita.Mara ya kwanza ilikua mwaka 1982 pale Nicole alipoimba "Ein bisschen Frieden"

Tangu wakati huo ilikua nadra kuwaona waimbaji wa Ujerumani wakikamata nafasi za mbele-mara tatu walifika hadi ya kuburura mkia.Enzi hizo zimekwisha anasema Stefan Raab aliyemgundua na kumwandaa Lena hadi kufikia ushindi.

Ujerumani ndio itakayoandaa mashindano ya Eurovision mwakani.

Mwandishi:Langer,Marko(DW Deutsch),Hamidou,Oummilkheir

Mpitiaji:Mohammed Abdul-Rahman