1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yatafuta wafanyakazi

16 Agosti 2012

Katika wiki za hivi karibuni, maelfu ya vijana wanaanza mafunzo ya kitaalamu kwa fani zao, mfumo ambao ulianzishwa zamani sana, lakini hadi sasa madarasa ya kutolea mafunzo hayo yanaonekana yakiwa matupu.

https://p.dw.com/p/15qmr
Kiwanda cha magari cha Opel, Bochum, Ujerumani.
Kiwanda cha magari cha Opel, Bochum, Ujerumani.Picha: Reuters

Nchini Ujerumani, soko la mafunzo ni jambo jema, anaamini Markus Kiss, mtaalamu wa Elimu katika Taasisi ya Biashara ya Viwanda na Biashara.

Hadi mwishoni mwa mwezi uliopita, tayari mikataba 250,000 ilishasainiwa katika sekta ya viwanda na biashara, likiwa ongezeko la mara mbili ikilinganishwa na wakati kama huo mwaka jana. Lakini bado kuna nafasi zilizoko wazi.

“Kwenye baraza la biashara pekee kuna nafasi 12,000 za kazi kwa wanafunzi, zinazopaswa kujazwa. Na wigo wa kazi hizo ni mpaka, kutoka zile za taaluma ya migahawa na hoteli hadi mameneja viwandani au wataalamu wa teknolojia ya habari.” Anasema Kiss

Katika jumla ya nafasi za kazi 480,500 zilizotangazwa na Shirika la Ajira la Ujerumani tangu mwezi Oktoba 2011, ni chini ya nafasi 144,000 zilizojazwa hadi kufikia mwezi uliopita wa Julai. Wakati huo huo, kuna waombaji 142,000 ambao “bado hawajashughulikiwa.”

Kati ya nafasi hizo kwa mujibu wa wakala wa ajira, waombaji wengi waliomba nafasi za ualimu. Nafasi nyingi zilizo wazi ziko kwenye sekta za hoteli na upishi zikingoja wataalamu wa kuzijaza.

Vijana wa Kijerumani wanachagua kazi

Kitisho kwa Ujerumani, kwa hivyo, si kukosekana kwa nafasi za ajira, "bali ni vijana wa Kijerumani kuchagua ajira hizo," anasema Otto Kentzler, Rais wa Shirika la Ajira la Ujerumani.

Watu wasio na ajira wakisuburi nje ya ofisi inayotoa huduma kwa watu hao, März, Ujerumani.
Watu wasio na ajira wakisuburi nje ya ofisi inayotoa huduma kwa watu hao, März, Ujerumani.Picha: AP

“Bahati mbaya vijana hawa wamejikita kwenye maeneo fulani tu mahsusi, kama vile ufundi wa magari na utengenezaji wa nywele, hawana hamu sana na sekta ya chakula. Ingawa kwenye vyuo vya mafunzo ya ajira kuna mambo mengi sana ya kuchagua. Kazi za kujifunza si mambo ya fesheni na urembo tu, bali pia ufundi wa umeme, mabomba ya maji na mashine za joto." Anafafanua Kentzler.

Suala jengine lililojitokeza kwenye soko la mafunzo ya kazi sasa ni mabadiliko ya aina ya vijana wanaoomba mafunzo. Kwa mujibu wa Shirika la Ajira la Ujerumani, tangu mwaka 2007, asilimia 50 ya walioomba kuchukua mafunzo hayo walikuwa vijana kutoka Ujerumani Mashariki, lakini sasa wameshuka kwa zaidi ya asilimia 30. Na sasa wengi walioomba nafasi kwenye vyuo vya mafunzo wanakwenda vyuo vikuu. Matokeo yake ni kuwa nafasi nyingi zaidi za mafunzo zimeendelea kubakia bila kujazwa.

Sekta ya ujenzi ya Ujerumani inajikuta katika kitisho cha upungufu wa vijana na wataalamu kwa kiasi kikubwa maana wengi wa waombaji wa nafasi hizo ni wale waliokimbia skuli. Katika mwaka 2011 moja kati ya kampuni tatu kubwa za ujenzi ilishindwa kuwachukua waombaji wengi kwa sababu nafasi za mafunzo zilijaa sana.

Ukosefu wa Kijerumani na Hisabati

b Kilichokuwa hakijabadilika kwa miaka ya hivi karibuni, hata hivyo, ni malalamiko ya kampuni nyingi kwamba waombaji wa nafasi za mafunzo ya kazi hawana ujuzi mzuri wa lugha ya Kijerumani na hisabati.

Wakala wa Ajira Ujerumani.
Wakala wa Ajira Ujerumani.Picha: AP

“Tumeziuliza kampuni na zinasema kwamba robo tatu ya wale wanaoomba hawana uwelewa wa kutosha wa lugha ya Kijerumani na hisabati, lakini zaidi ni ukosefu wa stadi za kijamii za waombaji hao ndilo tatizo kubwa zaidi.” Anasema Markus Kiss.

Kiwango cha juu cha ukosefu wa ajira kusini mwa Ulaya kiliwafanya vijana wengi kukimbia Ujerumani kutafuta kazi. Hivi sasa kuna vyuo vya mafunzo nchini Hispania, kwa mfano, kwa ajili ya makampuni ya Kijerumani, ambako miongoni mwa masomo yanayosomeshwa ni kozi maalum ya Kijerumani.

Hadi sasa Ujerumani inaweza kuitwa "salama" katika soko la ajira la Umoja wa Ulaya, ambapo kwa mujibu wa Idara ya Takwimu ya Umoja huo, Eurosat, hadi mwezi Juni ni vijana 350,000 tu ndio waliokuwa hawakuajiriwa, ikiwa sawa na asilimia 7.9, wakati katika mataifa kama Ugiriki na Hispania, vijana wasio na ajira ni zaidi ya asilimia 50.

Mwandishi: Monika Lohmüller/Mohammed Khelef/DW
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman