1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yawajibika katika Umoja wa mataifa

18 Septemba 2013

Mzozo wa Syria na werevu wa Urusi,miaka 40 tangu Ujerumani ilipojiunga na Umoja wa Mataifa na awamu ya mwisho ya kampeni za uchaguzi nchini Ujerumani ni miongoni mwa mada magazetini.

https://p.dw.com/p/19jz9
Mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry na Urusi Serguei Lawrow wakipeana mikono baada ya kuafikiana kuhusu SyriaPicha: Reuters

Mzozo wa Syria na werevu wa Urusi,miaka 40 tangu Ujerumani ilipojiunga na Umoja wa Mataifa na awamu ya mwisho ya kampeni za uchaguzi nchini Ujerumani ni miongoni mwa mada zilizotangulizwa mbele na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.

Tunaanzia na mzozo wa Syria unaoonyesha kuurejeshea misuli yake Urusi.Gazeti la Stuttgarter Nachrichten linaandika:"Kwa hila na werevu mkubwa kuwahi kushuhudiwa tangu mkataba wa Warsaw ulipovunjika,Putin amewabainishia watu wa magharibi mambo mawili.Kwanza ni kwamba vikosi vya nchi yake vimerejea tena kuwa na nguvu kupindukia kipeo anachokikusudia kiongozi wa nchi hiyo.Ni kishindo hicho kwa wadadisi waliokuwa wakidhania wanajeshi wa Urusi wangali wanadorora baada ya kuaibishwa walipoivamia Georgia mwaka 2008.Na pili Putin ameubainishia ulimwengu kwamba Urusi imezindukana baada ya kukaa kimya kwa zaidi ya miaka 20 na inatanda.

Vereinte Nationen Vollversammlung Deutschland
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Guido Westerwelle akipiga kura katika zoezi la kuwachagua wanachama watano ambao si wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa mataifaPicha: imago stock&people

Ujerumani yawajibika duniani

Ujerumani inaadhimisha miaka 40 tangu ilipojiunga na Umoja wa Mataifa.Majukumu ya Ujerumani yamekuwa yakiongezeka tangu wakati huo.Gazeti la Leipziger Volkszeitung linaandika:"Ujerumani ingawa imeungana upya na ni mwanachama anaetoa mchango mkubwa,hata hivyo jumuia hiyo ya kimataifa bado haina nguvu za kutosha katika maamuzi yake.Na hilo si ajabu katika taasisi hiyo yenye wanachama 193-tuchukue mfano wa mzozo wa Syria ambapo sio tu Umoja wa mataifa bali hata Umoja wa ulaya wenye wanachama kidogo zaidi,una shida ya kufuata msimamo wa pamoja.Zaidi ya hayo baraza la usalama linatoa sura ya mivutano iliyokuwepo baada ya vita vikuu vya pili vya dunia.Juhudi zote za mageuzi zimeshindwa hadi sasa kutokana na ushupavu na hasa wa mataifa matano makubwa yenye kura ya turufu.Mwenye kuukosoa Umoja wa mataifa kuwa ni "jukwaa la mabishano" hajakosoa.Lakini Umoja huo hauna mbadala.Jumuia ya kimataifa inaweza kuwa na nguvu tu ikiwa wanachama wake wataipatia nguvu."

Deutschland Bundestagswahl 2013 letzte Bundeskabinett Sitzung Rösler und Merkel
Waziri wa uchumi ambae ni mwenyekiti wa chama cha FDP Philipp Rösler na kansela Angela Merkel wakizungumza baada ya kikao cha mwisho cha baraza la mawaziri kabla ya uchaguzi mkuuPicha: picture-alliance/dpa

Homa ya uchaguzi yazidi kupanda

Na hatimae tunarejea hapa hapa Ujerumani ambako kampeni za uchaguzi zimeshika kasi zikiwa zimesalia siku tano tu kabla ya siku ya siku kuwadia.Utafiti wa maoni ya umma unaonyesha kuyamwagia mchanga matumaini ya baadhi ya viongozi.Katika wakati ambapo kansela Angela Merkel angependelea kuendeleza muungano pamoja na waliberali,FDP lakini watapa tapa.Gazeti la Volksstimme linaandika:"Kwa muda mrefu kampeni za mwaka huu za uchaguzi humu nchini zilikuwa zikiangaliwa kuwa chapwa.Hivi sasa lakini mambo yamebadilika.Utafiti wa hivi karibuni wa maoni unaashiria wezani sawa kati ya serikali na upande wa upinzani.Awamu ya mwisho inasisimua.FDP wanatapatapa,wamekata tamaa na kuomba wapatiwe kura ya pili kutoka kwa wafuasi wa vyama ndugu vya CDU/CSU.Walinzi wa mazingira wanazongwa na ya kale-mjadala kuhusu kunajisiwa watoto unamuathiri zaidi mgombeya wao mkuu Jürgen Trittin.Moyo unapiga kwa kishindo,wanasiasa wanajiuliza watafanya nini wale ambao hadi sasa hawajaamua?Na eti vyama vidogo vidogo:die Piraten na Chaguo mbadala AfD vitafanikiwa kiúkiuka kiunzi cha asili mia tano na kuwakilishwa bungeni?Au pengine SPD itapuuza ahadi na kuunda muungano pamoja na walinzi wa mazingira die Linke?Hakuna lolote la hakika kwa sasa.Kila kitu kinawezekana.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri:Yusuf Saumu