1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Ujumbe wa AU Somalia waanza kuwaondoa wanajeshi wake

1 Julai 2023

Jeshi la Umoja wa Afrika katika nchi iliyoharibiwa kwa vita Somalia limesema limekamilisha awamu ya kwanza ya kuwapunguza askari wake, kwa lengo la hatimaye kuuweka usalama wa nchi mikononi mwa jeshi la kitaifa na polisi

https://p.dw.com/p/4TIxT
Uganda Kampala | Meeting zu Somalia
Picha: Ministry foreign affairs Uganda

Ujumbe wa Mpito wa Afrika nchini Somalia - ATMIS umesema katika taarifa kuwa jumla ya vituo saba vimekabidhiwa kwa vikosi vya usalama vya Somalia, na kuwezesha kupunguzwa wanajeshi 2,000 kufikia muda wa mwisho wa Juni 30.

Soma pia: Uganda yathibitisha kuuawa wanajeshi wake 54 wa jeshi la kulinda Amani la Umoja wa Afrika nchini Somalia.

Mkuu wa operesheni za ATMIS Bosco Sibondavyi ameelezea hatua hiyo kuwa muhimu katika utekelezaji wa Mpango wa Mpito wa Somalia na maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu kuhamishwa kwa jukumu la usalama.

Baraza la Usalama mapema wiki hii liliongeza kwa miezi sita idhini yake kwa jeshi la Umoja wa Afrika, ambalo lina hadi mwisho wa Septemba kuwaondoa wanajeshi wengine 3,000.

Ujumbe wa ATMIS ulijumuisha zaidi ya askari 19,000 na maafisa wa polisi kutoka matafifa kadhaa yakiwemo Burundi, Ethiopia, Kenya na Uganda na wote wanapaswa kuondoka nchini humo ifikapo mwisho wa 2024.