Ukame, mafuriko, njaa: El Nino yaivamia Afrika
El Nino ina matokeo mabaya kwa Afrika: Huku mataifa mengine yakipambana na ukame mkali, mvua kubwa kabisa zinayagharikisha maeneo mengine ya bara hilo.
Njaa nchini Zimbabwe
Umoja wa Mataifa umeonya kuwa matokeo ya El Nino nchini Zimbabwe yatakuwa mabaya zaidi. Kati ya dola za Kimarekani milioni 360 zinazohitajika kukabiliana na njaa, ni milioni 70 tu zilizopatikana. Zimbabwe inataka msaada wa haraka, na bado uliofika ni mchache tu.
Msaada wa haraka wahitajika
Kutokana na ukame mkubwa, serikali ya Zimbabwe ilitangaza hali ya dharura mwezi Februari. Zaidi ya watu milioni nne wanahitaji msaada wa chakula, ambao ni sawa na asilimia 30 ya raia wote. Kwa ujumla, eneo la kusini mwa Afrika lina watu milioni 14 wanaohitaji msaada wa haraka wa chakula.
Ukame nchini Ethiopia
Hakuna nchi ambayo imekumbwa vibaya zaidi barani Afrika kuliko Ethiopia. Kwa mwaka mzima, hakukuwa na mvua kusini mwa nchi hiyo. Zaidi ya watu milioni 10 wanahitaji msaada wa chakula, zaidi ya milioni sita hawana fursa ya kupata maji wala matibabu. Kijembe kilioje ni kuwa kwenye maeneo mengine ya nchi hiyo, mvua kali imesababisha mafuriko yaliyouwa watu kadhaa.
Kila kitu kimepotea
Katika jimbo la Shinile, kusini mwa Ethiopia watu wanawaona wanyama wao wakifa mbele ya macho yao pasi msaada wowote. Zaidi ya wanyama 600,000 tayari wameshakufa. Majanga kwa wachungaji: bila ya mbuzi na kondoo wao, maisha yao wao pia yako hatarini.
Mvua ya mauti
Wakati Simbabwe na Ethiopia zikihitaji mvua ya haraka, mji mkuu wa Kenya, Nairobi, unaghariki kwa mafuriko. Baada ya mvua kubwa iliyonyesha kwa siku chache, jengo hili kwenye mtaa wa madongo-poromoka wa Huruma lilititia chini na watu 51 wakapoteza maisha, huku 19 wakiwa hawajuilikani walipo.
Mafuriko mabaya Kenya
Waokozi wanakuja kuwaokoa wahanga wa nyumba iliyoboka. Lakini wahanga wengi wa mafuriko wako peke yao. Wapweke kwenye mtaa wa mabanda wa Mukuru - ambao ndio mkubwa zaidi jijini Nairobi - ambako takribani nyumba 300 zimeharibiwa na maji baada ya kingo za mito kupasuka.