1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya wasiokuwa na kazi imepungua Ujerumani

Othman, Miraji2 Julai 2008

Idadi ya watu wasiokuwa na kazi hapa Ujerumani imefikia kiwango cha chini kabisa kuwahi kuonekana tangu miaka 15 iliopita.

https://p.dw.com/p/EUwf
Bwana Frank-Jürgen Weise, mkuu wa Idara ya Kazi ya Ujerumani.Picha: AP

Kwa mara ya kwanza tangu Disemba mwaka 1992, idadi ya watu wasiokuwa na ajira mwezi wa Juni uliopita ilifikia chini ya milioni 3.2. Kwa hivyo, ni asilimia 7.5 ya Wajerumani wanaoweza kufanya kazi ambao sasa wanatafuta ajira. Na kwa mujibu wa Idara ya Kazi ya hapa Ujerumani, makisio ni kwamba idadi hiyo inaweza kwenda chini ya milioni tatu ifikapo msimu wa mapukutiko ya mwaka huu.

Mkuu wa Idara ya Kazi ya hapa Ujerumani, Frank-Jürgen Weise, amesema kwamba kupunguzwa michango ya wafanya kazi kwa ajili ya bima ya kutokuwa na kazi mnamo mwaka 2009 kunawezekana, yaani kihesabu. Pindi uchumi utaendelea kun'gara kama ilivyo sasa,

idara ya kazi hadi mwaka 2012 itakuwa na ziyada ya Euro bilioni kumi hadi kumi na moja kutokana na michango ya bima za waajiriwa. Kwa hivyo,alisema, itategemea wanasiasa waamuwe kama fedha hizo zitumiwe katika kupunguza michango ya kila mwezi ya bima za kutokuwa na kazi kwa waajiriwa, au zitumiwe katika kuchukuwa hatua ziyada za kuunda nafasi za kazi. Chama tawala cha CDU kinataka wafanya kazi wapunguziwe asilimia 0.3 katika michango ya bima wanayolipia.

"Inawezekana kupunguza hadi asilimia 0.3 ya michango ya bima. Mtu lazima atilie maanani kwamba pindi uchumi utazorota, mambo yatakuwa magumu zaidi, kwani watu laki moja wasiokuwa na kazi wanagharimu Euro bilioni 1.3."

Mwezi Juni, watu milioni 3.16 walisajiliwa kuwa hawana vibarua, tarakimu hiyo ni 123,000 chini ya ile ya mwezi wa Mei na pia 528,000 chini ya ile ya mwezi Juni mwaka jana.

Sababu ya hali hii nzuri ni kwamba uchumi umepanda vizuri mwanzoni mwa mwaka huu, na jambo hilo limesaidiwa na marekebisho katika masoko ya kazi. Pia nafasi mpya za kazi zimechomoza na kuengezeka, huku wafanya biashara wakitaka wafanya kazi zaidi. Idadi ya watu waliokuwa wanafanya kazi Ujerumani nzima katika mwezi wa Mei ilikuwa milioni 40,27; idadi hiyo ni 155,000 zaidi ya tarakimu ya mwezi April, na 618,000 zaidi, uklinganisha na mwaka jana wakati kama huu. Kwa mujibu wa Idara ya kazi ilio na makao yake makuu mjini Nürnberg ni kwamba idadi ya wafanya kazi wanaolazimika kuchangia katika bima za kijamii imeongezeka kwa watu 602,000 mnamo mwaka uliopita.

Katika eneo la Umoja wa Ulaya ambalo lina nchi wanachama 27, kiwango cha ukosefu wa kazi ni kidogo, ni kiasi ya asilimi 6.8 ya watu wanaoweza kufanya kazi. Mwezi April kilikuwa asilimia 6.7 na mwezi Mei mwaka jana kiwango kilikuwa asilimia 7.2.

Uzuri wa hali hii nzuri iliochomoza hapa Ujerumani ni kwamba hata wafanya kazi wazee wanahitajika, kinyume na hapo zamani. Watu wa umri mbali mbali wanafaidika na neema hii, japokuwa kuna ugumu kwa vijana sana kuambulia nafasi za kazi.