1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine wabadilishana wafungwa

22 Februari 2015

Jeshi la Ukraine na wawakilishi wa waasi wanaotaka kujitenga wamebadilishana wafungwa kadhaa gizani katika eneo la mapigano jana Jumamosi(21.02.2015) na kuanzisha mchakato wa kuleta amani mashariki mwa Ukraine.

https://p.dw.com/p/1EfdW
Ukraine und Separatisten starten Gefangenenaustausch
Mabadilishano ya wafungwa UkrainePicha: picture-alliance/dpa/AP Photo/Vadim Ghirda

Wanajeshi 139 na waasi 52 walibadilishwa, kwa mujibu wa afisa wa wanaotaka kujitenga ambaye ameshuhudia hatua hiyo ya mabadilishano ya wafungwa katika eneo ambalo halidhibitiwi na upande wowote karibu na kijiji cha Zholobok, kiasi ya kilometa 20 magharibi ya mji unaoshikiliwa na waasi wa Luhansk.

Ukraine und Separatisten starten Gefangenenaustausch
Baadhi ya wanajeshi wa serikali ya Ukraine walioachiliwa huruPicha: picture-alliance/dpa/AP Photo/Vadim Ghirda

Basi lililojaa wanajeshi wa Ukraine wakiwa katika sare za jeshi liliwasafirisha wanajeshi hao mapema siku hiyo kutoka jimbo ambalo ni ngome kuu ya waasi wa Donestk hadi katika eneo la vijijini kiasi ya kilometa 140 kaskazini mashariki , kabla ya kujiunga na makundi mengine ya wafungwa wenzao.

Ukraine und Separatisten starten Gefangenenaustausch
Wanajeshi wa jeshi la serikali ya Ukraine wakihutubiwa na wawakilishi wa waasiPicha: picture-alliance/dpa/AP Photo/Vadim Ghirda

Baada ya kuwasili katika eneo katika mji wa Zholobok , wanajeshi hao walipangwa katika mistari na kusikiliza hotuba iliyotolewa na wawakilishi wa waasi, ambao wamewaamuru watu hao kuondoka katika eneo hilo linalodaiwa na wapiganaji wanaotaka kujitenga katika majimbo ya Donetsk na Luhansk.

Wanajeshi, baadhi yao wakitembea kwa kutumia magongo, wakati mmoja akiwa amebebwa katika machela, walitembea kwa karibu kilometa tatu hadi katika eneo la makutano.

Ukraine Kiew Gefangenenaustausch 27.12.2014
Basi lililowachukua wanajeshi wa UkrainePicha: picture-alliance/ITAR-TASS/Mikhail Palinchak

Rais wa Ukraine Petro Poroshenko ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba amearifiwa kuwa mchakato mzima ulianzia katika idara ya usalama wa taifa.

Haifahamiki watu wangapi wanashikiliwa

Msemaji wake , Svyatoslav Tsegolko, baadaye amesema mwanajeshi mmoja zaidi wa Ukraine mfungwa ataachiwa huru katika siku zijazo.

Makubaliano ya amani yaliyotiwa saini wiki iliyopita mjini Minsk yameelekeza katika mabadilishano ya wafungwa wote katika mzozo huo. Haifahamiki ni watu wangapi wanashikiliwa kwa jumla katika pande zote , licha ya kwamba wapiganaji wanaotaka kujitenga katika mji wa Donetsk wamesema Ukraine inawashikilia kiasi ya waasi 580 kama wafungwa.

Ukraine Gefangenenaustausch zwischen Rebellen und Kiew 26.12.2014
Mabadilishano ya wafungwa UkrainePicha: AFP/Getty Images/V. Maximov

Waasi wamesema idadi kubwa ya wanajeshi wa Ukraine walioachiliwa siku ya Jumamosi wamekamatwa wakati wa mapigano ya hivi karibuni kwa ajili ya mji muhimu wa Debaltseve, ambao umekamatwa na wapiganaji wanaotaka kujitenga wiki iliyopita.

Jamhuri iliyojitangaza ya watu wa Donestk imeeleza katika taarifa kwamba wengi wa watu waliokabidhiwa kwa maafisa wa Ukraine walikuwa ni raia.

Lakini "wachache kiasi ya asilimia 50 ya wale waliohusika katika mabadilishano kutoka kwa jamhuri ya watu wa Donestk walikuwa wafungwa wanajeshi," taarifa hiyo imesema.

Taarifa ya waasi imedokeza kile ilichosema ni waangalizi katika mabadilishano hayo wakisema wengi wa wafungwa walioachiliwa huru na serikali ya Ukraine wana ishara za kutendewa vibaya.

"Baadhi ya wafungwa hawakuweza kutembea wenyewe.

Wakati huo huo , wafungwa wote wanajeshi waliokabidhiwa kwa wawakilishi wa Ukraine walikuwa katika hali nzuri," taarifa hiyo imesema.

Marekani yaonya

Wakati huo huo Marekani imeonya jana Jumamosi(21.02.2015)kwamba "inaweza kuweka vikwazo vikali zaidi" dhidi ya Urusi katika muda wa siku chache kuhusiana na ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano, ambayo yamo katika hali mbaya licha ya waasi wanaounga mkono Urusi na majeshi ya serikali kubadilishana wafungwa.

US-Außenminister Kerry mit britischem Amtskollegen Hammond in London
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry(kulia) akiwa na mwenzake wa Uingereza Phillip Hammond(shoto)Picha: Reuters/N. Hall

Mashambulizi dhidi ya mji wa Debaltseve na zaidi ya ukiukaji mara 250 wa makubaliano ya kusitisha mapigano ambayo yanaelezwa kuwa yamefanywa na waasi wanaounga mkono Urusi yamesababisha kuikasirisha Marekani , ambayo inawalaumu Urusi kwa mzozo huu wa miezi kumi sasa.

"Iwapo hali hii itaendelea, bila shaka , kutakuwa na hatua zaidi zitakachochukuliwa ambazo zitaongeza mbinyo kwa uchumi wa Urusi ambao tayari imeelemewa," waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry amesema kwa hasira katika mkutano na waandishi habari mjini London.

Anaamini kwamba rais Barack Obama , "katika siku chache zijazo " ataamua kuhusu "hatua za ziada" ambazo zitachukuliwa kujibu hali ya ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano." Ametabiri kwamba "kutakuwa na vikwazo vikali zaidi" vitakavyowekwa.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / ape

Mhariri: Amina Abubakar