1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yajiandaa kwa vita na waasi

Josephat Nyiro Charo6 Januari 2015

Ukraine ililihami jeshi lake jana (05.01.2015) kwa vita na waasi wanaoiunga mkono Urusi mashariki mwa nchi licha ya mazungumzo ya amani ya Berlin na mkutano kuhusu mzozo huo ukitarajiwa kufanyika wiki ijayo Kazakhstan.

https://p.dw.com/p/1EFRq
Poroschenko übergibt Kriegsgeräte
Picha: Reuters/V. Ogirenko

Shirika la habari la Ujerumani DPA limeripoti kwamba rais wa Ukraine Petro Poroshenko mwenyewe alipeleka jana ndege za kivita, mbili aina ya MIG-29, na mbili aina a Su-27, mizinga ya masafa mafupi na vifaru kwa jeshi katika eneo la Zhytomyr kaskazini mwa nchi hiyo. "Naamini mwaka wa 2015 utakuwa mwaka wa ushindi. Ili kulifikia lengo hilo tunahitaji jeshi imara lenye nguvu zaidi, na silaha za kisasa za kutosha," alisema Poroshenko. Rais huyo pia aliongeza kusema kurejea kwa amani nchini Ukraine kutategemea juhudu zao wenyewe.

"Tutakuwa na amani tutakapokuwa na mpaka uliofungwa, wakati wanajeshi wa kigeni watakapoondoka kutoka ardhi yetu na hatimaye tutakapoweza kurejesha mamlaka ya dola katika maeneo yanayokaliwa. Hili linaweza kufikiwa kwa njia ya diplomasia. Msaada wa ulimwengu unaratibiwa na juhudi zetu."

Hatua ya Poroshenko inakiuka moja kwa moja makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa mwezi Septemba mwaka uliopita katika mji mkuu wa Belarus, Minsk, ambapo pande husika katika mzozo wa Ukraine zilikubaliana kuondoa silaha nzito.

Poroschenko übergibt Kriegsgeräte
Rais Poroshenko akiwapa silaha wanajeshiPicha: Reuters/V. Ogirenko

Mkutano wa pande nne uliojadili njia za kuutekeleza mkataba wa Minsk ulifanyika jana mjini Berlin na kuhudhuriwa na wanadiplomasia wa ngazi ya juu kutoka mataifa ya Umoja wa Ulaya pamoja na Urusi na Ukraine. Maafisa walisema mkutano mpya wa kilele utakuwa na maana kama ufanisi halisi utapatikana katika kuutekeleza mkataba wa amani wa Minsk.

Wajumbe wa Ukraine na Urusi walielezea wasiwasi wao kuhusu kupatikana kwa ufanisi wowote katika mazungumzo hayo ya Berlin. Mjumbe wa Ukraine, Alexei Makeyev, alisema hafutilii mbali uwezekano wa matatizo mapya kujitokeza wakati wa mazungumzo hayo akiongeza kusema mkataba wa amani ulioafikiwa mjini Minsk ulitafsiriwa tofauti na kila upande.

Merkel anasitasita

Ujerumani na Ufaransa zimetilia shaka mazungumzo ya amani yaliyopangwa kufanyika mjini Astana nchini Kazakhstan Alhamisi wiki ijayo. Poroshenko ameelezea nia yake ya kuhudhuria mkutano wa mjini Astana pamoja na rais wa Urusi Vladimir Putin. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na rais wa Ufaransa Francoise Hollande pia wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo, ingawa serikali zote mbili zimesema zitashiriki kwa masharti kwamba makubaliano ya mjini Minsk yatiliwe maanani zaidi.

"Siwezi kusema kama mkutano kama huo utafanyika. Mkutano kama huo utakuwa na maana ikiwa tunaweza kupiga hatua na kufanikiwa," amesema msemaji wa Merkel, Steffen Seibert, siku tatu kabla ya ziara ya waziri mkuu wa Ukraine Arseniy Yatsenyuk mjini Berlin. Merkel atakutana na Yatsenyuk Alhamisi wiki hii.

Angela Merkel und Wladimir Putin Kombobild
Kansela Merkel (kushoto) na rais PutinPicha: picture-alliance/dpa/Gambarini/Druzhinin

"Tuna wazo lililo wazi kuhusu ufanisi halisi. Kwanza kabisa ni kuutekeleza kikamilifu mkataba wa amani wa Minsk na usitishwaji halisi wa mapigano na wa muda mrefu, mpaka kati ya maeneo yanayodhibitiwa na Ukraine na waasi na kuondolewa kwa silaha nzito. Mambo kama haya lazima yaandaliwe mapema," akaongeza kusema Seibert.

Rais Poroshenko pia alionya kwa uangalifu mkubwa jana akisema mazungumzo yanaweza kufanyika tu kama watafaulu kuandaa rasimu ya makubaliano kabla Januari 15.

Ufaransa yalegeza msimamo kuhusu Urusi

Rais wa Ufaransa Francoise Hollande pia alizungumzia kuhusu mzozo wa Ukraine na mkutano wa Kazakhstan wakati wa mahojiano yake ya muda wa masaa mawili na redio ya Ufaransa. Kama Merkel, Hollande atakwenda Astana kama kutapatikana ufanisi mpya vinginevyo hakuna haja kuhudhuria mkutano huo.

"Nitakwenda Astana Januari 15 kwa sharti moja kwamba ufanisi upatikane. Kama ni kukutana tu na kuzungumza bila ufanisi wowote, basi hakuna haja. Lazima tuzungumze na Putin. Lazima tumwambie tunachokitaka na tusichokitaka. Na yeye anatakiwa ajue vipi atakavyoacha."

Kiongozi huyo wa Ufaransa alikuwa na msimamo wa wastani kidogo kuhusu Urusi na rais Putin kuliko viongozi wengine wa mataifa ya magharibi, akisema vikwazo dhidi ya Urusi vinapaswa kuondolewa kama hatua zitapigwa katika kuutanzua mzozo wa Ukraine.

Hollande alijibu maswali kuhusu mazungumzo yake ya ana kwa ana na rais Putin akisema kiongozi huyo wa Urusi hataki kulitwaa eneo la mashariki mwa Ukraine. "Anachokitaka ni kubakia kuwa na ushawishi. Tunachotaka ni kwamba aheshimu mipaka ya Ukraine." Alisema rais Hollande.

Mwandishi: Josephat Charo/AFPE/DPA/REUTERS

Mhariri: Daniel Gakuba