1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yajiandaa kwa vita

2 Machi 2014

Ukraine inajiandaa kwa vita baada ya Rais Vladimir Putin wa Urusi kutangaza kwamba ana haki ya kuivamia nchi hiyo na kusababisha malumbano makubwa kuwahi kushuhudiwa tokea kumalizika kwa Vita Baridi.

https://p.dw.com/p/1BIKB
Wanajeshi wa Ukraine wakiwa katika mji wa Feodosiya katika jimbo la Crimea(02.03.2014).
Wanajeshi wa Ukraine wakiwa katika mji wa Feodosiya katika jimbo la Crimea(02.03.2014).Picha: Reuters

Waziri Mkuu wa Ukraine Arseny Yatseniuk ambaye ameshika madaraka akiwa kama kiongozi wa serikali inayounga mkono mataifa ya magharibi baada ya Rais Viktor Yanukovich mshirika wa Urusi kuikimbia nchi hiyo wiki iliopita amekaririwa akisema leo hii " Hili sio tishio bali kwa kweli ni tangazo la vita dhidi ya nchi yangu."

Yaseniuk ametowa kauli hiyo iliyoonyeshwa na televisheni na kuongeza kusema kwamba iwapo Rais Putin anataka kuwa raia aliyeanzisha vita kati ya nchi mbili jirani na marafiki yaani Ukraine na Urusi "amefikia lengo hilo kwa inchi chache na kwamba wako kwenye ukingo wa vita."

Putin alipata kibali cha bunge hapo jana kutumia nguvu za kijeshi kuwalinda raia wa Urusi walioko kwenye jimbo la Crimea nchini Ukraine na kuyafanya mataifa ya magharibi yakimbilie kumsihi asichukuwe hatua hiyo.

Vikosi vya Urusi viko Crimea

Vikosi vya Urusi tayari vimeichukuwa Crimea bila ya kumwaga damu ambayo ni rasi ilioko katika Bahari Nyeusi ambapo Urusi ina kambi yake ya wanamaji.Leo hii vikosi hivyo vilizingira vituo kadhaa vidogo vya kijeshi vya Ukraine vilioko Crimea na kuwataka wanajeshi wake wajisalimishe. Baadhi yao walikataa na hakuna risasi yoyote ile iliyofyatuliwa.

Waziri Mkuu wa Ukraine Arseniy Yatsenyuk akizungumza na waandishi wa habari Kiev(02.03.2014)
Waziri Mkuu wa Ukraine Arseniy Yatsenyuk akizungumza na waandishi wa habari Kiev(02.03.2014)Picha: picture-alliance/AP Photo

Baraza la usalama la Ukraine limetaka vikosi vyote vya ulinzi viwekwe katika hali ya tahadhari ya hali ya juu.Wizara ya Ulinzi imetakiwa kuwaita kazini wanajeshi wa akiba ambapo kinadharia inamaanisha wanaume wote wenye umri wa miaka 40 waliojiandikisha jeshini kwa hiari juu ya kwamba itawawia vigumu kuwapatia watu hao silaha na sare.Jeshi dogo la Ukraine haliwezi kushindana na jeshi la taifa jirani lenye nguvu kubwa duniani la Urusi.

Katika uwanja wa uhuru mjini Kiev ambapo waandamanaji dhidi ya Yanukovich walikuwa wamepiga kambi kwa miezi kadhaa,maelfu ya watu wameandamana dhidi ya hatua hiyo ya kijeshi ya Urusi na kumtaka Putin aiache Ukraine.

Wasi wasi mkubwa zaidi kuliko hata ule wa Urusi kuitwaa Crimea ni ule wa majimbo makubwa ya mashariki mwa nchi hiyo ambapo Waukraine wengi wanazungumza Kirusi kama lugha ya asili.

Ukraine yataka msaada wa NATO

Maeneo hayo hapo jana yalishuhudia wanaandamanaji wanaoiunga mkono Urusi wakipandisha bendera za Urusi kwenye majengo ya serikali na kutowa wito kwa Urusi kuwahami.Serikali ya Ukraine imesema maadamano hayo yalikuwa ni jungu lililopikwa na Urusi kwa kutuma mamia ya raia wake kuvuka mpaka na kufanya maandamano hayo.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Anders Fogh Rasmussen katika makao makuu ya NATO Brussels. (02.03.2014)
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Anders Fogh Rasmussen katika makao makuu ya NATO Brussels. (02.03.2014)Picha: Reuters

Ukraine imetowa wito wa msaada kwa Jumuiya ya Kujihami ya NATO na moja kwa moja kwa Uingereza na Marekani ambazo kwa pamoja na Urusi zimesaini makubaliano ya mwaka 1994 yenye kudhamini usalama wa Ukraine baada ya kusambaratika kwa Ukraine.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier mwenye miwani.
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier mwenye miwani.Picha: picture-alliance/dpa

Katibu Mkuu wa NATO Anders Fogh Rasmussen ameishutumu Urusi kwa kutishia amani na usalama barani Ulaya. Rasmussen amesema kile inachofanya Urusi hivi sasa nchini Ukraine kinakiuka misingi ya katiba ya Umoja wa Mataifa na kuitaka ikomeshe harakati zake za kijeshi na vitisho.

Pia ametowa wito kwa Ukraine kuendelea kudumisha haki za demokrasia kwa watu wote na kuhakikisha haki za watu wachache zinalindwa.

Mabalozi wa NATO wamekutana mjini Brussels leo hii kujadili hatua za kuchukuwa.

Harakati za kidiplomasia

Onyo tafauti limetolewa na Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier ambaye ametowa taarifa leo hii akisema hali iliopo sasa ni njia ya hatari kabisa ya kuzidisha mvutano.

Hata hivyo amesema bado kuna wakati wa kutuliza vichwa na kuacha busara itumike na kwamba mgawanyiko mpya wa Ulaya bado unaweza kuepukwa.

Kama vile Rasmussen, waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani pia ameutaka uongozi mpya wa Ukraine kuhakikisha haki za Waukraine zinaheshimiwa zikiwemo zile za watu wachache zenye kujumuisha matumizi ya lugha yao.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry ametowa onyo la wazi wazi kwa Urusi leo hii kwamba inahatarisha kupoteza nafasi yake miongoni mwa nchi za Kundi la Mataifa Manane tajiri yenye maendeleo makubwa ya viwanda duniani G8 kutokana na hatua yake hiyo ya kutuma vikosi vyake huko Crimea.

Kerry amemuonya Rais Putin hatoweza kuwa na Mkutano wa Kilele wa G8 uliopangwa kufanyika Sochi nchini mwake na pengine asiweze hata kubakia katika kundi hilo la G8 iwapo hali hiyo itaendelea.Ameongeza kusema yumkini akajikuta anakabiliwa na kuzuiliwa kwa mali za makampuni ya Urusi na kampuni za Marekani zikajitowa nchini humo.

Juhudi hizo za kidiplomasia zimekuja siku moja baada ya Rais Barack Obama kutumia mazungumzo yake ya simu na Rais Vladimir Putin kujaribu kumshawishi kubadili mkondo huo.

Mwandishi: Mohamed Dahman /Reuters/AP

Mhariri.Caro Robi