1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yatafuta msaada wa kimataifa

10 Machi 2014

Ukraine inatafuta msaada wa haraka kutoka kwenye mataifa ya Magharibi, baada ya Rais wa Urusi, Vladmir Putin kusisitiza kuwa Crimea ina haki ya kujiunga na Urusi, hata kama imeonyesha utayari wake kwa mazugumzo.

https://p.dw.com/p/1BMhr
Arseniy Yatsenyuk
Arseniy YatsenyukPicha: Reuters

Timu ya Ukraine inayoungwa mkono na Umoja wa Ulaya, ambayo iliongoza maandamano ya miezi mitatu yaliyosababisha mauaji na kufanikiwa kiondoa madarakani serikali ya Viktor Yanukovych iliyokuwa inaungwa mkono na Urusi, inatafuta msaada huo kwa lengo la kulinda heshima ya taifa hilo lenye watu milioni 46, ambalo kwa sasa limegawanyika.

Uongozi wa mkoa wa Crimea, umeandaa kura ya maoni kuhusu kujiunga na Urusi, itakayofanyika tarehe 16 ya mwezi huu wa Machi. Hatua hiyo imekosolewa vikali na mataifa ya Magharibi, ambayo pia yamekasirishwa na hatua ya Urusi kulidhibiti eneo la Crimea katika operesheni ambayo haijasababisha umwagikaji wa damu, iliyoanza siku chache baada ya kuanguka kwa serikali ya Ukraine Februari 22 na kusababisha Rais Yanukovych kukimbilia Urusi.

Rais Vladmir Putin
Rais Vladmir PutinPicha: picture-alliance/dpa

Merkel aionya Urusi

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, ambaye ametoa tahadhari kuhusu hatua ya kuiwekea Urusi vikwazo, amemwambia Rais Putin kwamba kura ya maoni kwa Crimea kujiunga na Urusi siyo halali.

Mzozo wa Urusi na mataifa ya Magharibi ulishika kasi baada ya Rais Putin kuwaeleza Kansela Merkel na Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron kuwa anazitambua hatua zinazochukuliwa na viongozi wa Crimea, tangu kuanguka kwa serikali ya Yanukovych.

Hata hivyo, ofisi ya Merkel imesema kuwa Rais Putin ameahidi kufanya mazungumzo hii leo (10.03.2014) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov kuhusu kuundwa kwa ''Kundi la mawasiliano la kimataifa'' kuhusu Ukraine, hatua ambayo hapo awali aliipinga. Hatua hiyo itasaidia kuwepo mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Ukraine na serikali ya Uingereza.

Yatsenyuk kwenda Marekani

Juhudi hizo za kimataifa zinafanyika wakati ambapo Waziri Mkuu wa Ukraine, Arseniy Yatsenyuk, anajiandaa kuelekea mjini Washington kwa mazungumzo na Rais Barack Obama wa Marekani, yenye lengo la kushinikiza mpango wa amani, ikiwemo kuunga mkono uchaguzi wa urais wa Ukraine uliopangwa kufanyika Mei 25.

Rais Barack Obama
Rais Barack ObamaPicha: picture-alliance/dpa

Mkutano kati ya Rais Obama na Yatsenyuk utakaofanyika keshokutwa Jumatano (12.03.2014), utaongeza uaminifu wa serikali ya Yatsenyuk, ambayo haitambuliwi na Urusi na pia utaipatia Ukraine nafasi ya kutoa maelezo kuhusu umuhimu wa kupatiwa misaada ya kiuchumi.

Ukraine imesema inahitaji Euro bilioni 25 kwa ajili ya kuiendesha nchi hiyo katika miaka miwili ijayo, baada ya Urusi kuzuia kiasi cha Euro bilioni 15 ilichoahidi kutoa kwa Yanukovych kama malipo ya kukataa kusaini mkataba wa kihistoria na Umoja wa Ulaya, mwezi Novemba mwaka uliopita.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,DPAE
Mhariri:Mohammed Abdul-rahman