1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya na Asia yazungumza

Maja Dreyer28 Mei 2007

Katika mkakati wao wa kuimarisha uhusiano kati ya nchi za Umoja wa Ulaya na za bara la Asia, leo kunaanza mkutano wa mawaziri wa mambo ya kigeni wa nchi za mabara haya mawili mjini Hamburg. Ikiwa ni wiki moja kabla ya mkutano wa nchi za G8 ambao pia unafanyika hapa Ujerumani, wanaharakati wanaopinga utandawazi wanayachukulia mazungumzo haya ya ASEM kama majaribio kuandamana.

https://p.dw.com/p/CHDd
Maadamano mjini Hamburg
Maadamano mjini HamburgPicha: AP

Mkutano huo wa siku mbili unapoanza mjini Hamburg, hali ni tete katika mji huo wa bandari, Kaskazini mwa Ujerumani. Mawaziri hao wa Umoja wa Ulaya na nchi 16 za Kiasia wanalindwa vikali na polisi baada ya kutokea mashambulio ya wapinzani wa utandawazi mjini humo. Maandamano ya leo ambapo walishiriki maadamanaji elfu kadhaa kutoka nchi mbali mbali za Ulaya hadi hapa yalipita salama. Lakini polisi inahofia fujo zinaweza kutokea, kama anavyosema afisa Ralf Meyer: “Lazima tuzingatie kuwa kati ya waandamanaji hao elfu tano, wengi wao wako tayari kutumia nguvu, tuseme kama elfu moja au mbili. Tutaangalia kwa karibu mambo yataendelea vipi.”

Masuala yanayozungumziwa kwenye mkutano huo ni hali katika nchi zinazokumbwa na vita za Iraq na Afghanistan, maendeleo ya mazungumzo ya kisiasa huko Korea na kudhibiti mkataba wa kutoeneza silaha za kinyuklia. Zaidi ya haya, mawaziri pia watazungumzia masuala ya hali ya hewa na nishati.

Mkutano huo wa mabara ya Asia na Ulaya ambao kwa ufupi unaitwa ASEM ulianzishwa mwaka 1996. Nchi husika zinawakilisha zaidi ya nusu ya wakaazi wote wa dunia, vile vile zaidi ya nusu ya biashara duniani. Kutokana na ukuaji mzuri wa kiuchumi wa nchi kama vile China, Japan au India, mataifa ya Asia yanazidi kupata umuhimu katika siasa za kimataifa.

Kabla ya mazungumzo ya ASEM kuanza, shirika la kimataifa linalotetea haki za binadamu, Amnesty International, lilikosoa vikali ukiukaji wa haki za binadamu katika nchi za Asia. Zikitengwa Kambodsha na Philippines, nchi zote bado zilizosalia babo adhabu ya kifo. Pia, vita dhidi ya ugaidi duniani vinatumika kuwanyamazisha wapinzani, shirika la Amnesty International limesema.

Katika taarifa yao iliyotolewa leo, tawi la Ujerumani la Amnesty International pia linadai wanaharakati wanaopanga kuandamana dhidi ya sera za kimataifa za nchi za G8 ambazo viongozi wao watakutana wiki ijayo mjini Heiligendamm, Ujerumani, wahakikishiwe haki zao za kutoa maoni yao na kuandamana kwa njia ya amani. Shirika hilo limeikumbusha polisi wa Ujerumani kuwa hatua wanazozichukua zinabidi zienda sambamba na hatari iliyopo na zisiwe kali kupita kiasi.

Kabla ya mkutano wa leo mjini Hamburg, mahakama ilipiga marufuku maandamano kufanyika karibu na uwanja wa mkutano kati kati ya mji. Mwishoni mwa wiki iliyopita polisi iliwakamata waandamanaji 11 walioanzisha fujo dhidi ya polisi. Wengi wa wanaharakati waliokuja Hamburg lakini waliandamani kwa amani, baadhi yao walijifunga midomo kwa kutumia tepu iliyoandikwa: Ukosoaji ni sawa na ugaidi. Hivi karibuni kumezuka mjadala mkali nchini humu juu ya mbinu ya polisi na idara za usalama kuzuia machafuko. Utaratibu mmoja ambao umekosolewa hasa ni kuhifadhi harufu ya watuhumiwa. Watu wengi wakiwa pia wanasiasa wa serikali ya Ujerumani walisema hiyo inakumbusha kazi za idara ya ujasusi ya Ujerumani Mashariki ya zamani.