1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya, Ujerumani zamuaga rasmi Helmut Kohl

Iddi Ssessanga
1 Julai 2017

Viongozi wa sasa na wa zamani wa dunia wamemuaga rasmi hayati Helmut Kohl, wakimkumbuka kansela huyo wa zamani wa Ujerumani kwa kuinganisha Ulaya na kuleta maridhiano kati ya maadui wa zamani barani humo.

https://p.dw.com/p/2flcd
Trauerfeierlichkeiten für Altkanzler Kohl
Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Kohl, aliefariki Juni 16 akiwa na umri wa miaka 87, alikuwa mtu mwa kwanza kupewa heshima na kumbumbuku rasmi na Umoja wa Ulaya katika mji wa Ufaransa wa Strasbourg.

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker amesema sherehe hiyo iliyofanyika katika makao makuu ya Bunge la Ulaya, karibu na mpaka na Ujerumani, ilikuwa chaguo la Kohl mwenyewe, akimuelezea kama mzalendo wa Ujerumani, na wakati huo mzalendo wa Ulaya.

Wakati wa uongozi wake wa miaka 16 kama kansela wa Ujerumani, Kohl aliongoza harakati za kuinganisha tena Ujerumani na kuundwa kwa sarafu ya pamoja na Euro.

Clinton: Kohl alitupa fursa kushiriki mambo makubwa

"Nilikuwa nazungusha macho leo, na sote tulioalikwa hapa tuliwahi kuwa madarakani, kwa nini? Kwa sababu Helmut Kohl alitupa fursa ya kushiriki katika jambo kubwa kuliko sisi wenyewe, kubwa kuliko ofisi zetu, kubwa kuliko kazi zetu," alisema rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton.

Trauerfeierlichkeiten für Altkanzler Kohl
Jeneza la Kohl likiwa kwenye boti ya MV Mainz kuelekea mji wa Speyer anakozikwaPicha: picture-alliance/AP Photo/A. Arnold

Kwa sababu sisi wote karibuni au baadae tutakuwa katika jeneza kama hilo, na zawadi pekee tunayoweza kuacha nyuma ni mustakabali bora kwa ajili ya watoto wetu na uhuru wa kufanya maamuzi yao yakiwemo makosa yao."

Kohl anakumbukwa na wengi kwa ustadi wake mkubwa alioutumia kushinda hofu za majirani wa Ujerumani wakati, mwisho wa mgawiko wa miongo kadhaa wa upande wa kikomunisti wa mashariki, na magharibi iliofuata demokrasia, ulipogeuka jambo la uhalisia mwishoni mwa miaka ya 1990.

Mrithi wake, kansela wa sasa wa Ujerumani Angela Merkel, amesema maono ya Kohl na kutoyumba kwake anapochukua msimamo vilitoa faida ya kihistoria. "Mambo mengi tunayoyachukuliwa kawaida hii leo yaliletwa naye," alisema Merkel.

"Kwamba Ujerumani Mashariki na Magharibi ziko pamoja sasa hivi, kwamba tuna soko la pamoja, kwamba hakuna ukaguzi wa mipakani kati ya mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya, ukweli kwamba mengi ya mataifa hayo yanatumia sarafu moja, kwamba Umoja wa Ulaya katika muundo wake wa sasa unaendelea kuwepo, yote hayo yanahusishwa na jina la Helmut Kohl. Ameshawishi na kutengeneza kizazi kizima."

Mwanaulaya halisi

Spika wa bunge la Ulaya Antonio Tajani alisema Kohl alistahili nafasi ya heshima katika Umoja wa Ulaya kwa kutoa mkono wa urafiki bila kusita kwa mataifa ya Ulaya Mshariki baada ya kuanguka kwa kile kinachojulikana kama pazia la chuma.

Trauerfeierlichkeiten für Altkanzler Kohl
Kansela Angela Merkel akizungumza awali katika bunge la Ulaya huku jeneza la Kohl likiwa katikati mwa ukumbi wa bunge.Picha: Reuters/A. Wiegmann

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alibainisha kuwa alikuwa mtangulizi wake, Rais wa zamani wa Ufaransa Francois Mitterand na Kohl, ni watu wawili walioshuhudia mateso ya vita kwa pande mbili hasimu, walioweza kushinda kumbukumbu mbaya za kizazi chao.

Wazungumzaji kadhaa walikumbuka ishara ya uchungu ya maridhiano mwaka 1984, wakati Mitterand na Kohl waliposhikana mikono kwenye tukio lililofanyika katika makaburi ya wahanga wa vita kuu vya pili vya dunia mjini Verdun, Ufaransa.

Baada ya tukio la mjini Strasbourg lililohudhuriwa na wageni zaidi ya 800, jeneza la Kohl lililofunikwa na bendera ya Umoja wa Ulaya lilisafirishwa kwa helikopta hadi mji wa Ludwigshafen, ambako lilibadilishiwa bendera na kufunikwa na ya Ujerumani kabla ya kuwekwa kwenye boti  ya MS Mainz kupitia Mto Rhein kuelekea mji wa Speyer kwa ajili ya ibada ya misa na hatimaye kuzikwa.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape,dpae,ebu,aptn

Mhariri: Daniel Gakuba