1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya wagawika kuhusu mkuu wa kamisheni

28 Mei 2014

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamegawika juu ya anayestahiki kuiongoza Kamisheni ya Ulaya, lakini wanaunganishwa na hofu zao juu ya nguvu za vyama vya siasa kali kupitia uchaguzi wa bunge la Ulaya.

https://p.dw.com/p/1C81D
Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya anayemaliza muda wake, Jose Manuel Barroso (kulia) na Rais wa Baraza la Ulaya, Herman Van Rompuy, kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Brussels.
Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya anayemaliza muda wake, Jose Manuel Barroso (kulia) na Rais wa Baraza la Ulaya, Herman Van Rompuy, kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Brussels.Picha: picture-alliance/AP

Vyama vinavyoutilia shaka Umoja wa Ulaya nchini Ufaransa na Uingereza ndivyo vilivyoibuka na ushindi katika uchaguzi huo wa Ulaya, na sasa katika kusaka majibu ya hali hiyo, Rais Francois Hollande wa Ufaransa na Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, wamekuja na masuluhisho tafauti katika mkutano huu wa kilele.

Cameron, ambaye chama chake cha kihafidhina kimepata viti 19 kwenye bunge hilo, ilhali chama cha siasa kali za kizalendo, UKIP, kikijinyakulia viti 24, anaamini kuwa lazima Umoja wa Ulaya unapaswa sasa kujibinya na sio kujitanua.

"Tunahitaji mtazamo ambao unatambua kuwa Brussels imekuwa kubwa sana, imekuwa na mari kubwa mno, na imekuwa ikiingilia mno mambo ya mataifa wanachama. Tunahitaji kurudisha mambo mengi zaidi kwa mataifa wanachama. Iwe taifa mwanachama popote inapolazimika, na Ulaya pale tu inapolazimika." Alisema Cameron wakati akiwasili kwenye chakula cha jioni hapo jana (27.04.2014)

Hollande ataka mageuzi yasiyo ya utekezaji

Kwa Rais Hollande wa Ufaransa, hali ni mbaya zaidi. Chama cha siasa kali cha National Front kinachoongozwa na Marine Le Pen, kimepata viti 24, kikikizidi chama cha kisoshalisti cha Hollande kwa viti 11. Naye pia anataka mageuzi, ingawa ya tahadhari kwenye Umoja wa Ulaya.

Rais Francois Hollande wa Ufaransa.
Rais Francois Hollande wa Ufaransa.Picha: picture-alliance/dpa

"Kamisheni ya Ulaya haihitaji mageuzi ya kitaasisi, hilo si jukumu lake, bali kujikita kwenye vipaumbele, kuonesha ufanisi zaidi inapohitajika hivyo na sio kuongeza mambo pale yasipolazimika. Si suala la kubadili mkataba, bali ni utekelezaji wa mkataba unaopaswa kubadilika, unaotakiwa ni uwepesi tu." Amesema Hollande mbele ya waandishi wa habari siku ya Jumatano (tarehe 28.04.2014)

Merkel kama msuluhishi

Ni Kansela Angela Merkel wa Ujerumani anayeonekana kusimama kama mpatanishi kwenye mfadhaiko uliowakumba wenzake kwenye Umoja huo. Muungano wa vyama vyake vya kihafidhina ulishinda kwenye uchaguzi wa Bunge la Ulaya, ingawa nako chama cha AfD, kinachopinga madaraka makubwa ya Umoja wa Ulaya na sarafu ya euro, kinaingia kwenye Bunge la Ulaya kwa mara ya kwanza.

"Natarajia tutapiga hatua nzuri. Mkutano huu utakuwa ni juu ya kazi ya Kamisheni ya Ulaya kwa miaka mitano ijayo na kisha ndio masuala binafsi. Tunajua kuwa hakuna kundi la vyama lililo na wingi wa kutosha peke yake. Hivyo tutapaswa kupata wingi mkubwa na sasa tutaweka misingi ya kuendelea na jambo hilo."

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.Picha: Reuters

Hadi sasa, viongozi wengi wanakwepa makabliliano ya moja kwa moja juu ya ikiwa Jean-Claude Juncker, mgombea wa vyama vya mrengo wa kati kulia, au Martin Schulz wa vyama vya kisoshalisti, ateuliwe kuwa rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya, kama linavyotaka bunge hilo.

Viongozi kadhaa walisema watajikita zaidi kwenye sera kabla ya masuala hayo ya uteuzi ambayo yanagusa hisia kali za mirengo ya kisiasa, na hivyo wamempa jukumu Rais wa Baraza la Ulaya, Herman Van Rompuy, kufanya majadiliano juu ya ajenda na uongozi wa kamati tendaji ya Umoja wa Ulaya.

Kwa mujibu wa mkataba wa Umoja wa Ulaya, kamati tendaji inaweza tu kupendekeza rais wa kamisheni hiyo kwa kuzingatia matokeo ya uchaguzi wa bunge.

Mwandishi: Bernd Riegert/Mohammed Khelef
Mhariri: Iddi Ssessanga