1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya yakutana Cyprus kujadili maafa ya Syria

7 Septemba 2012

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Ulaya wanakutana nchini Cyprus kujadili namna ya kuepusha maafa ya mzozo wa Syria kuingia Ulaya huku Urusi ikizitaka nchi za Magharibi kufikiria upya sera zake kuelekea Syria.

https://p.dw.com/p/164sn
Rais Dimitris Christofias wa Cyprus.
Rais Dimitris Christofias wa Cyprus.Picha: AP

Mkutano huo unafanyika katika nchi ya umoja huo ambayo iko karibu zaidi na Syria, umbali wa kilometa 100. Viongozi wa umoja wa Ulaya wanahofia huenda athari za machafuko hayo zikaingia kwenye mipaka ya nchi zake kuanzia Cyprus.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton, ameufanya mzozo wa Syria kuwa ajenda kuu ya mkutano huo wa siku mbili ambao ni wa kwanza kufanyika tangu kuanza kwa mapumziko ya msimu wa joto barani Ulaya.

Mazungumzo hayo, ambayo pia yatahusisha suala la mpango wa nyuklia wa Iran, yanafanyika wakati huu ambapo kuna wasiwasi mkubwa kuhusu kuongezeka kwa mzozo baina ya Rais Bashar al-Assad na wapinzani nchini Syria, na kuzidisha watu kukimbia makaazi yao. Mwezi uliopita pekee kiasi ya watu 100,000 wamevuka mipaka ya nchi hiyo na kukimbilia nchi jirani.

Ushawishi wa Ufaransa

Ufaransa inatazamiwa kuwashawishi washirika wenzake kwenye mkutano wa leo kutafuta njia za kupeleka misaada ya madawa, fedha na huduma nyingine muhimu kwa maelfu ya watu waliokwama kwenye machafuko ndani ya Syria katika maeneo yanayoshikiliwa na waasi.

Rais Francois Hollande wa Ufaransa (kushoto).
Rais Francois Hollande wa Ufaransa (kushoto).Picha: Reuters

Ufaransa na Uingereza zimekubaliana kuhusu haja ya kuengeza kasi ya kuunda serikali ya mpito nchini humo. Rais Francois Hollande wa Ufaransa amemuambia waziri mkuu wa Uingereza, David Cameron, na hapa ninamnukuu, "ni lazima tufanye haraka mabadiliko ya kisiasa na tuwasaidie wapinzani kuunda serikali" mwisho wa kumnukuu.

Ulaya bado imeendelea kuwa katika mgawanyiko kuhusu namna gani bora ya kuusaidia upinzani nchini Syria ambao nao umegawanyika. Marekani imeonya kuwa kabla ya kuunda serikali yoyote, upinzani ni lazima uungane kwanza. Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani, Victoria Nuland, amesema kuwa hicho ni kipengele cha kwanza cha lazima ili wakubaliane ni namna gani serikali itakayoundwa itakuwa.

Urusi yaonya

Uturuki, ambayo pamoja na Iraq, Jordan na Lebanon zinawahifadhi maelfu ya wakimbizi wa Syria, imetoa pendekezo la kuanzishwa maeneo ya salama nchini humo ili kupunguza wimbi la wakimbizi.

Rais Vladimir Putin wa Urusi.
Rais Vladimir Putin wa Urusi.Picha: picture-alliance/dpa

Hata hivyo, wazo hilo limweshindwa kukubaliwa katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa wiki iliyopita kutokana na wasiwasi uliopo baina ya mataifa ya magharibi kuhusu ugumu wa operesheni za kijeshi za aina hiyo.

Hapo jana, Rais Vladimir Putin wa Urusi alitoa wito kwa nchi za magharibi na zile za kiarabu kupitia upya sera zao juu ya Syria, akisema kuwa lengo kuu linapasa kuwa kukomesha mauwaji.

Wakti hayo yakijiri, wanaharakati wanaripoti kuwa kumezuka mapigano makali baina ya waasi na vikosi vya serikali katika eneo la kusini la mji mkuu wa Damascus. Jana pekee kiasi ya watu zaidi ya 90 waliuawa kutokana na mapigano yanayoendelea nchini humo.

Mwandishi: Stumai George/AFP/DPA
Mhariri: Miraji Othman