1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya yapata muafaka kuhusu uokozi wa wahamiaji

21 Aprili 2015

Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu wakimbizi limesema waliozama katika ajali ya boti katika Bahari ya Mediterania ni watu 800, na mawaziri wa Umoja wa Ulaya wamekubaliana juu ya mpango wa kupunguza vifo vya wahamiaji.

https://p.dw.com/p/1FBWK
Mawaziri wa Umoja wa Ulaya katika mkutano kuhusu uokozi wa wakimbizi
Mawaziri wa Umoja wa Ulaya katika mkutano kuhusu uokozi wa wakimbiziPicha: picture-alliance/dpa/J. Warnand

UNHCR imesema kuwa imeipata idadi hiyo baada ya kuzungumza na watu walionusuruka ajali ya boti hiyo iliyozama katika Bahari ya Mediterania mwishoni mwa juma lililopita. Msemaji wa shirika hilo nchini Italia Carlotta Sami amesema manusura hao wamewaambia kwamba boti waliyokuwa wakisafiria yenye urefu wa mita 20 ilipinduka kutokana na mkanyagano wa watu, uliotokea pale boti hiyo iliposogelewa na meli ya biashara ya kireno.

Watu hao wamewaambia maafisa wa UNHCR na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, kwamba boti hiyo ilikuwa na wasafiri zaidi ya 800 wakiwemo watoto wenye umri wa miaka kati ya 10 na 12. Msemaji wa UNHCR amesema watu hao walikuwa raia wa Syria, Eritra na Somalia na kwingineko.

Wakimbizi sio mzigo wa nchi moja

Taarifa hiyo ya UNHCR imekuja wakati mawaziri wa mambo ya nje na wa mambo ya ndani wa nchi za Umoja wa Ulaya wakiwa wamekubaliana juu ya mpango wenye vipengele 10, wenye lengo la kupunguza vifo vya wahamiaji wanaotoka Afrika Kaskazini kuelekea barani Ulaya kupitia Bahari ya Mediterania. Makubaliano hayo yamefikiwa katika mkutano uliofanyika jana mjini Luxembourg.

Umoja wa Ulaya utaongeza bajeti operesheni ya kuwaokoa wakimbizi baharini
Umoja wa Ulaya utaongeza bajeti operesheni ya kuwaokoa wakimbizi bahariniPicha: MOAS/Darrin Zammit Lupi

Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini amesema katika mkutano huo, walielewana kwamba nchi zote wanachama zitashirikiana kukabiliana na mgogoro wa wakimbizi.

''Leo tumepiga hatua mpya ya kuelewana kwamba hili ni tatizo la Ulaya, na sio la nchi moja mwanachama, na kwamba inatubidi kuchukua hatua za pamoja na za haraka. Huu sio wito kutoka baadhi ya nchi, ni jibu la nchi zote''. Amesema.

Juhudi zaidi kwa ajili ya wahamiaji

Vipengele muhimu vya makubaliano yaliyofikiwa na mawaziri wa Umoja wa Ulaya ni pamoja na kuiongezea bajeti operesheni ya umoja huo kuhusu ulinzi wa mipaka na uokozi wa baharini ijulikanayo kama Triton, ili iweze kupanua eneo lake la ulinzi.

Maelfu ya wahamiaji huyaweka maisha yao hatarini kwa kusafiri kutumia mitumbwi isiyofaa kwa Safari za baharini
Maelfu ya wahamiaji huyaweka maisha yao hatarini kwa kusafiri kutumia mitumbwi isiyofaa kwa Safari za bahariniPicha: Italienische Marine/dpa

Umoja wa Ulaya pia utajaribu kukamata na kuharibu boti zinazotumiwa kuwasafirisha watu kinyume cha sheria, na kuanzisha mradi wa kujitolea kuhusu kuwapa makaazi wahamiaji utakaojenga vituo mbali mbali vya kuwahifadhi watu wanaotaka kinga.

Alipokuwa akiutangaza mpango huo wa Ulaya kuhusu uokozi wa wahamiaji, Mogherini amesema Umoja wa Ulaya unalazimika kutekeleza kwa vitendo imani yake ya kiutu, na utayarifu wake kuwasaidia wahamiaji. ''Kuwarudisha walikotoka ni njia nyingine ya kuwauwa'', amesema bi Federica Mogherini.

Wakati huo huo, polisi nchini Italia imesema imewakama watu wawili miongoni mwa 27 walionusurika ajali ya boti hiyo, ambao wanashukiwa kuwa washirika wa genge la wasafirishaji haramu wa binadamu lililopanga safari hiyo iliyoishia katika maafa. Wote wawili, mmoja raia wa Syria, mwingine raia wa Tunisia, wanakabiliwa na mashitaka ya kusafirisha watu kimagendo.

Na rais wa Umoja wa Ulaya Donald Tusk amesema ameitisha mkutano wa viongozi wa Umoja wa Ulaya Alhamis wiki hii, kuujadili zaidi mpango huo kwa ajili ya wakimbizi.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/rtre

Mhariri:Hamidou Oummilkheir