1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya yazidisha uchunguzi kwa wasafiri

7 Aprili 2017

Raia wa Ulaya watakuwa wanachunguzwa katika maeneo ya mpakani ya nchi zilizo katika eneo la Schenghen kuanzia leo Ijumaa chini ya sheria inayonuia kupambana na wapiganaji kutoka mataifa ya kigeni wanaotoka Syria na Iraq.

https://p.dw.com/p/2arRK
Flagge der EU
Bendera ya Umoja wa UlayaPicha: imago/JuNiArt

Sheria hii inalenga kuwazuia magaidi kutoka nchi hizo mbili kuingia katika mataifa hayo ya Ulaya. Sheria hii mpya iliyoanzishwa na tume ya Ulaya, itahitaji nchi zote kuwasajili raia wote wanaoingia na kutoka eneo hilo na wasafiri wameonywa watarajie kucheleweshwa kwa safari zao barabarani na hata katika viwanja vya ndege.

Kulingana na msemaji mmoja wa Tume hiyo ya Ulaya, hatua hii ni ya kuhakikisha watu wanaovuka mipaka yao sio kitisho kwa usalama wa raia na usalama wa ndani wa eneo hilo la Schenghen, ambamo watu wana uhuru wa kusafiri bila kukaguliwa mipakani. Umoja wa Ulaya umesema umechukua hatua hii kutokana na yale mashambulizi ya Paris, mwezi Novemba mwaka 2015 na kitisho kinachoongezeka kutoka kwa magaidi.

Mataifa yote ya EU yaikumbatia sheria hiyo

Hii inamaanisha kwamba taarifa za kibinafsi na taarifa zilizo kwenye stakabadhi za usafiri za wanaosafiri nje na ndani ya eneo la Schenghen, zitachukuliwa na kuhifadhiwa katika sajili. Sheria za awali zilikuwa zinahitaji kuchukuliwa taarifa tu za wale ambao sio raia wa Umoja wa Ulaya, wanaoingia katika hilo eneo la Schenghen, ila sasa sheria hii mpya itawasajili hata raia wa Umoja huo pamoja na yeyote anaesafiri nje.

Mataifa yote 28 ambayo ni wanachama wa EU pamoja na yale mataifa mengine manne ambayo hayako katika Umoja wa Ulaya ila yako katika eneo la Schengen, yaliikumbatia sheria hiyo mpya mwezi uliopita. Mataifa hayo manne ni Uswizi, Norway, Iceland na Lichtenstein.

Gilles de Kerchove
Mshirikishi wa EU katika masuala ya ugaidi Gilles de KerchovePicha: picture-alliance/dpa

Kulingana na ripoti iliyotolewa Disemba na mshirikishi mkuu wa Umoja wa Ulaya katika masuala ya ugaidi, Gilles De Kerchove, raia 5,000 wa Umoja wa Ulaya wamesafiri kuelekea mashariki ya Kati kushiriki mapigano katika kundi linalojiita Dola la Kiislamu, tangu kundi hilo la kigaidi liwe mojawapo ya makundi yenye nguvu zaidi katika kanda hiyo kutokea mwaka 2014.

Raia wa Ukraine kusafiri bila visa nchi za EU

Kulingana na De Kerchove, takribani thuluthi moja ya hao waliosafiri wamerejea Ulaya, huku asilimia 15 hadi 20 wakikisiwa kufariki dunia na karibu nusu yao hivi wanasemekana kwamba bado wanaendelea na mapigano huko Mashariki ya Kati.

Huku hayo yakiarifiwa Bunge la Ulaya limeidhinisha raia wa Ukraine kusafiri bila visa katika nchi za Umoja wa Ulaya, na huenda suala hili likaanza mwezi Juni kama ishara ya kuiunga mkono nchi hiyo katika mapambano yake na Urusi.

Rais wa Ukraine Petro Poroshenko ameifurahia hatua hiyo.

Münchner Sicherheitskonferenz
Rais wa Ukraine Petro PoroshenkoPicha: Reuters/M. Dalder

"Hii ni kura ya kihistoria, sio tu kwa Ukraine, nina uhakika kabisa hii ni kura ya kihistoria kwa Ulaya iliyoungana. Ulaya ambayo mustakabali wa Ukraine upo," alisema Poroshenko, "hii ni zawadi nzuri kabisa kwa raia wa Ukraine kwa imani yao ya Umoja wa Ulaya, ulioanzisha na kuchochea mabadiliko ya kimaadili," aliongeza rais huyo wa Ukraine.

Hatua hiyo itawakubalia Waukraine kusafiri bila visa katika nchi za Umoja wa Ulaya kwa kipindi cha siku 90 kwa utalii ama kutembelea familia ila sio kufanya kazi.

Mwandishi: Jacob Safari/DW/AFPE

Mhariri: Gakuba, Daniel