1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulimwengu bila ya silaha za kinuklea

Oumilkher Hamidou5 Januari 2010

Mkutano wa kudurusu makubaliano ya kutosambaza silaha za kinuklea utaitishwa May ijayo mjini New-York

https://p.dw.com/p/LLJ1
Marais wa zamani wa Marekani na Usovieti,George Bush (kushoto) na Michail Gorbatshov wakitia saini makubaliano ya kupunguza silaha START nambari moja mnamo mwaka 1991Picha: picture-alliance/dpa

Licha ya hotuba ya rais Barack Obama ya kuwa na ulimwengu usiokua na silaha za kinyuklea,wataalam wanauangalia kwa jicho la wasi wasi mkutano wa nane wa kudurusu mkataba wa kuzuwia kutapakaa silaha za kinyuklea-na hasa kutokana na mvutano usiokwisha pamoja na Iran.

Mapema mwezi May mwaka huu,wawakilishi wa mataifa 189 yaliyotia saini mkataba wa kutosambaza silaha za kinyuklea, watakutana mjini New-York kuzungumzia umuhimu wa kuendelezwa mkataba huo. Huo utakua mkutano wa nane wa aina yake tangu mkataba wa kutosambaza silaha za kinyuklea kwa lugha ya kidiplomasia- "NPT" ulipoanza kufanya kazi mwaka 1970.

Mkutano wa mwezi May ujao una umuhimu mkubwa, anahisi Wim Bowen, ambae ni mtaalam wa masuala ya silaha-aliyewahi kuwa mwanachama wa tume ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa nchini Iraq -Professor wa fani ya usalama wa kimataifa katika chuo cha King's College mjini London:

"Huu ni wakati mgumu kupita kiasi.Miaka mitano iliyopita,watu hawakuweza kuafikiana jinsi ya kuimarisha mfumo wa kutosambaza silaha."

Mikutano minne ya kudurusu makubaliano ya kutosambaza silaha za kinyuklea iliyoitishwa tangu vita baridi vilipomalizika ilikua kila kwa mara ikigubikwa na lawama dhidi ya msimamo wa Marekani na madola mengine manne au matano yanayotambuliwa rasmi kama madola yanayomiliki silaha za kinyuklea kwa kutotekeleza ahadi za kupunguza silaha. Mkutano wa mwisho ulioitishwa mwaka 2005 ulishindwa kufikia makubaliano kutokana na mvutano huo huo. Wakishindwa tena kukubaliana mwezi Mei mwaka huu, itamaanisha mwisho wa makubaliano ya kutosambaza silaha za kinuklea.

Matumaini kwamba hali haitakua hivyo na kwamba mwaka 2010 pengine ukawa mwaka wa makubaliano ya kutosambaza silaha ameyazusha rais wa Marekani, Barack Obama, miezi minane iliyopita katika hotuba yake mjini Prague.

Obama Nobelpreisverleihung
Mshindi wa zawadi ya amani ya Nobel,rais Barack Obama wa MarekaniPicha: AP

"Kwa hivyo, hii leo nnasema wazi wazi na kwa dhati kabisa kwamba Marekani itapigania amani na usalama ulimwenguni bila ya silaha za kinyuklea."

Hiyo ilikua mara ya kwanza kwa rais wa Marekani kuzungumzia dhamiri za kuwa na ulimwengu bila ya silaha za kinyuklea.Rais Obama ameelezea pia hatua thabiti zitakazofuatwa kulifikia lengo hilo. Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kufikiwa makubaliano pamoja na Urusi kuhusu kupunguza idadi ya makombora yanayobeba vichwa vya kinyuklea- maarufu kwa jina la START pamoja na kuidhinishwa hivi karibuni na baraza la Senet la Marekani makubaliano ya kusitisha majaribio ya silaha za kinyuklea CTBT.

Mwandishi:Zumach Andreas/Hamidou Oummilkheir

Mhariri:Othman Miraji