1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulimwengu waukaribisha mwaka mpya 2011

1 Januari 2011

Kansela wa Ujerumani ataka kuimarisha sarafu ya euro huku mashambulio ya mabomu yakiwaua watu kadhaa katika mji wa Alexandria nchini Misri na katika mji mkuu wa Nigeria, Abuja mkesha wa mwaka mpya

https://p.dw.com/p/zsMs
Kansela wa Ujerumani, Angela MerkelPicha: AP

Sherehe za kuukaribisha mwaka mpya zimeendelea kote ulimwenguni hii leo. Mjini Berlin watu takriban milioni moja walikusanyika katika lango la Brandeburg usiku wa kumkia leo kuukaribisha mwaka mpya.

Katika hotuba yake ya mwaka mpya hapo jana, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amewaonya Wajerumani juu ya haja ya kuiimarisha sarafu ya euro, akisisitiza kwamba ni msingi imara wa ustawi wa taifa. Kansela Merkel pia aliwapongeza Wajerumani kwa jukumu lao katika kuikwamua nchi kutokana na mgogoro wa kiuchumi wa hivi karibuni, unaoelezwa kuwa mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha zaidi ya miaka 60.

Huku Ujerumani ikiwa inashikilia nafasi ya tatu kwa kuwa na idadi kubwa ya wanajeshi katika kikosi cha kulinda amani kinachoongozwa na jumuiya ya kujihami ya NATO nchini Afghansitan, Bi Merkel alisema hatowasahau wanajeshi tisa wa Ujeruamani waliouwawa nchini humo mwaka jana 2010. Alisema anapania kutengeneza nafasi zaidi mpya za ajira na kuendelea kupunguza nakisi ya bajeti ya Ujerumani mwaka huu mpya wa 2011.

Shambulio la bomu Alexandria

Rais wa Misri Hosni Mubarak, amewahimiza Wakristo na Waislamu kuwa watulivu baada ya watu takriban 21 kuuwawa mkesha wa mwaka mpya kwenye mlipuko wa bomu lililokuwa limetegwa ndani ya gari moja nje ya kanisa katika mji wa Alexandria.

Bombenanschlag auf Kopten in Alexandria / Ägypten
Waumini wakipiga kelele kando ya motokaa iliyoripuka nje ya kanisa la Coptic mjini AlexandriaPicha: AP

Shirika la habari la serikali MENA limeripoti kwamba Rais Mubarak amewataka Wamisri wote kukabiliana na ugaidi na wale wote wanaotaka kuvuruga usalama na uthabiti wa nchi hiyo. Mlipuko huo, ambao ulisababisha watu zaidi ya 40 kujeruhiwa, umetokea wakati waumini walipokuwa wakitoka kanisani muda mfupi baada ya saa sita usiku wa kuamkia sikukuu ya mwaka mpya.

Hakuna kundi lolote lililodai mara moja kuhusika na shambulio hilo, lakini kundi linalojulikana kama Islamic State of Iraq, lenye mafungamano na kundi la kigaidi la al Qaeda, hivi karibuni lilitoa vitisho dhidi ya Wakristo katika eneo la Mashariki ya Kati.

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, baba mtakatifu Benedikt XVI amewatolea mwito viongozi wa dunia kuwalinda Wakristo dhidi ya mateso na kutovumiliwa. Baba Mtakatifu ameutoa mwito huo kufuatia shambulio la bomu dhidi ya kanisa moja la madhehebu ya Coptic mjini Alexandria Misri, usiku wa kumkia leo. Shambulio hilo ni hujuma ya hivi karibuni kufanywa dhidi ya Wakristo katika eneo la Mashariki ya Kati na barani Afrika. Katika siku ambapo kanisa Katoliki linaadhimisha siku ya kimataifa ya amani, papa Benedict XVI amezingatia zaidi uhuru wa kuabudu na kuvumiliana katika hotuba yake.

Wakati huo huo, jumuiya ya nchi za Kiislamu, imelilaani shambulio la mjini Alexandria likilieleza kuwa kitendo cha kihalifu na kigaidi kilichowalenga raia waliokuwa wakiabudu. Syria imesema shambulio hilo linalenga umoja na uhuru wa kuabudu nchini Misri na mataifa mengine ya Kiarabu. Ufaransa imeyaongoza mataifa ya Ulaya kulilaani vikali shambulio hilo la Alexandria.

Shambulio la bomu Nigeria

Kwa upande mwingine watu wasiopungua 30 wamewawa nchini Nigeria kwenye mlipuko uliotokea mkesha wa sikukuu ya mwaka mpya katika mji mkuu wa nchi hiyo, Abuja. Rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan amelilaumu kundi moja lenye msimamo mkali wa dini ya Kiislamu ambalo limedai kufanya mashambulio ya mabomu nchini humo hivi karibuni,ambapo watu wasiopungua 80 waliuwawa. Mlipuko wa hivi karibuni umetokea mahala penye shughuli nyingi mjini Abuja, karibu na kambi moja ya jeshi.