1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulinzi dhidi ya makombora wazusha wasiwasi wa kisiasa barani Ulaya

21 Machi 2007

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ameonya dhidi ya mgawanyiko baina ya nchi za ulaya kutokana na mpango wa Marekani wa ulinzi dhidi ya makombora katika maeneo ya Ulaya ya kati.

https://p.dw.com/p/CHHq
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani

Bibi Merkel amesisitiza kuwa bara la Ulaya litadhoofika zaidi iwapo litatoa nafasi ya migawanyiko miongoni mwa nchi zake.

Ujerumani imesisitiza kila mara juu ya msimamo wake wa kufanyika majadiliano kuhusu swala la kuwekwa vifaa vya ulinzi dhidi ya makombora katika nchi za Poland na Jamuhuri ya Czech.

Ujerumani inataka mpango huo ujadiliwe ndani ya nchi wanachama wa NATO pamoja na Urusi.

Wanasiasa wa Ujerumani vilevile wameeleza wasiwasi wao pamoja na kuonya dhidi ya kurejea enzi za vita baridi.

Mpango huo wa ulinzi dhidi ya makombora hata bado haujaanza kujengwa na pengine huenda ujenzi huo usifanyike kamwe lakini umeitumbukiza ulaya katika mzozo wa kisiasa.

Mjadala mkali umezuka juu ya mpango huo wa Marekani, Urusi inahisi kutishiwa na mpango huo na vilevile inahisi kuwa haikushirikishwa.

Mpango huo wa Marekani unatishia kuzigawa nchi za umoja wa Ulaya.

Lakini Marekani inasisitiza kuwa mpango huo unalenga tu kupambana dhidi ya vitisho vya baadaye kutoka nchi kama vile Iran wazo ambalo linapingwa vikali na Urusi ambayo inaonya kuwa hatua hiyo ni sawa na kuanzisha mashindano mapya ya silaha.

Marekani imekiri kwamba hadi sasa hakuna ushahidi kuwa Iran ina uwezo wa kuunda makombora ya masafa marefu yanayoweza kuwa tayari kufanya mashambulio, lakini hakun a anaejua nini kinaweza kutokea katika siku za usoni inadai Marekani.

Akifafanua sababu za kuweka ulinzi huo dhidi ya makombora waziri wa mambo ya nje wa Marekani bibi Condoleeza Rice amesema.

Tunaishi katika dunia ambapo Urusi na Marekani zinashirikiana vizuri sana….tunaishi katika dunia ambapo ni vigumu hata kudhania kwamba panaweza kutokea vita vya nyuklia kati ya Urusi na Marekani. Katika msingi gani ama patakuwa na sababu gani za kisiasa.

Juu ya wasiwasi wa Urusi mkuu wa mkakati huo wa ulinzi wa Marekani ameeleza kuwa Urusi na nchi za NATO zimepewa taarifa juu mpango huo wakati wote.