1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulinzi waimarishwa Misri

Kabogo Grace Patricia13 Septemba 2010

Ulinzi huo umeimarishwa kutokana mazungumzo ya ana kwa ana kuhusu amani ya Mashariki ya Kati hapo kesho.

https://p.dw.com/p/PB4n
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, Hillary Clinton, akiwa na Mjumbe Maalum wa Marekani katika Mashariki ya Kati, George Mitchell.Picha: AP

Wakati duru ya pili ya mazungumzo ya amani ya ana kwa ana ya Mashariki ya Kati yakitarajiwa kufanyika hapo kesho, Misri imeimarisha ulinzi mkali katika Rasi ya Sinai kabla ya mazungumzo hayo yaliyopangwa kufanyika katika mji wa kitalii wa Sharm el-Sheikh. Ulinzi huo umeimarishwa lengo likiwa kuhakikisha usalama wakati wa mazungumzo hayo.

Gavana wa Sinai Kusini, Mohamed Abdelfadil Shousha ameliambia shirika la habari la Ujerumani-DPA, kuwa vikosi vya usalama vimeongezwa katika vituo vya ukaguzi kwenye barabara kuu, ili kuimarisha usalama katika vizuizi barabarani. Ulinzi huo umeimarishwa kutokana na miaka ya nyuma magaidi kuzilenga hoteli ya kitalii katika Rasi ya Sinai likiwemo lile shambulio kubwa la mwaka 2006.

Huku Misri ikiimarisha ulinzi, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani Hillary Clinton, baadaye hii leo anatarajiwa kuwasili Mashariki ya Kati kwa ajili ya kushiriki katika mazungumzo hayo ya amani ya ana kwa ana kati ya Israeli na Wapalestina. Bibi Clinton aliyeambatana na Mjumbe Maalumu wa Marekani katika Mashariki ya Kati, George Mitchel, ataongoza mazungumzo hayo kati ya Waziri Mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu na Rais wa Mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas.

Aidha, baada ya mazungumzo hayo ya kesho, ujumbe huo wa Marekani utaelekea Jerusalem siku ya Jumatano kuendelea na mazungumzo mengine. Siku ya Ijumaa Rais Barack Obama wa Marekani aliitolea wito Israeli kurefusha muda wa kusitishwa kwa ujenzi wa makaazi ya Walowezi wa Kiyahudi katika Ukingo ya Magharibi unaomalizika muda wake tarehe 26 ya mwezi huu wa Septemba. Rais Obama pia aliahidi kuwa utawala wake utabakia na kuendelea kujihusisha na mazungumzo haya mapya ya amani ya ana kwa ana na kwamba hata kama yatavunjika, Marekani itaendelea kujitahidi kuyafanikisha.

Hata hivyo, licha ya Rais Obama kutoa wito huo, shirika la wanaharakati wa masuala ya amani, limesema kiasi nyumba 2,066 ziko tayari kujengwa katika eneo la Ukingo wa Magharibi, wakati ambapo muda huo uliowekwa na Bwana Netanyahu ukiwa unakaribia kumalizika. Shirika hilo la Israeli linalofuatilia ujenzi huo limesema leo kuwa ujenzi wa msingi wa nyumba hizo tayari umeanza. Aidha, shirika hilo limedai kuwa nyumba 11,000 ambazo bado msingi wake haujajengwa, pia zimeidhinishwa kujengwa.

Hatua hiyo inamaanisha kuwa hata kama serikali ya Netanyahu itaamua kuhusu hali iliyopo sasa ya kuendelea kusitisha ujenzi wa makaazi hayo, Walowezi bado wanaweza kujenga nyumba 13,000, ambapo 5,000 kati ya hizo zikiwa katika eneo la makaazi lililojitenga na ambalo lina utata katika kizuizi cha Ukingo wa Magharibi.

Mazungumzo hayo ya amani yanafanyika huku kukiwa na taarifa zilizotolewa na madaktari wa Palestina za kuuawa watu watatu na wengine wawili kujeruhiwa katika shambulio lililofanywa na kiafaru cha Israeli hapo jana katika Ukanda wa Gaza. Jeshi la Israeli lilithibitisha taarifa hizo likisema kuwa shambulio lilikuwa na lengo la kuzuia mashambulio ya maroketi yaliyokuwa yakiwalenga wanajeshi wa Israeli. Mazungumzo ya ana kwa ana kuhusu amani ya Mashariki ya Kati yalizinduliwa rasmi mjini Washington mapema mwezi huu wa Septemba baada ya kukwama kwa takribani miezi 20.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (DPA/AFPE)

Mhariri:Abdul-Rahman