1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umaarufu wa rais Bush wapungua

Josephat Charo3 Julai 2007

Inawezekana kulikuwa na wakati ambapo rais George W Bush wa Marekani alimuonea wivu mwenzake wa Urusi Vladamir Putin wakati wa mazungumzo yao katika shamba la familia yake huko Kennebunkport, Maine nchini Marekani. Umaarufu wa rais Putin nchini Urusi unampa ushawishi mkubwa lakini umaarufu wa rais Bush unaendelea kupungua huku akijianda kuacha madaraka miezi tisa ijayo.

https://p.dw.com/p/CHBk
Rais Putin (kushoto) na rais Bush katika shamba la Kennebunkport, Maine
Rais Putin (kushoto) na rais Bush katika shamba la Kennebunkport, MainePicha: AP

Huku rais Vladamir Putin wa Urusi akiendelea kujipatia sifa nchini mwake, mambo ni tofauti kwa rais George W Bush wa Marekani. Kwa mujibu wa matokeo ya kura ya maoni yaliyotolewa wiki iliyopita, umaarufu wa rais Bush umeshuka na kufikia kiwango cha chini kabisa na ushawishi ndani ya chama chake unaonekana ukipungua kwa kasi kubwa.

Kupungua kwa ushawishi wa rais Bush katika chama chake cha Republican kulidhihirika wiki iliyopita wakati wabunge 37 kati ya wabunge 49 wa chama hicho walipompinga kwenye kura iliyoyakwamisha matumaini yake ya kutaka kuzibalisha sheria za uhamiaji katika kipindi cha miezi 18 iliyosalia kabla kumaliza awamu yake.

Matokeo ya kura hiyo yaliashiria kushindwa kwa swala muhimu na pengine rahisi miongoni mwa maswala manne muhimu ya ndani yaliyojumulisha pia kubadili mfumo wa usalama wa kijamii, kupunguza kodi, na sheria zinazolenga kupunguza visa vya watu kukimbilia mahakamani kufungua kesi za madai ya mateso. Lakini kushindwa kwa mswada wa sheria kuhusu uhamiaji ni pigo kubwa lililoonekena kudhoofisha nguvu ya kisiasa aliyokuwa nayo rais Bush.

Kura ya maoni iliyofanywa na shirika la habari la CBS nchini Marekani imedhihirisha kuwa umaarufu wa rais Bush umeshuka kufikia asilimia 27, ikiwa ni asilimia moja tu zaidi ya kiwango kilichotolewa na jarida la Newsweek majuma mawili yaliyopita. Shirika la Fox News ambalo mara kwa mara limekuwa likitoa viwango vya juu ya uungwaji mkono wa rais Bush pia liliripoti kiwango cha chini kabisa cha asilimia 31wiki iliyopita.

Uungwaji mkono wa rais Bush na Wamarekani ulishuka chini ya asilimia 50 kati ya wakati alipochaguliwa tena kuwa rais wa Marekani mnamo mwezi Novemba mwaka wa 2004 na wakati wa kuapishwa kwake miezi miwili baadaye. Gazeti la Washington Post limesema Bush hajafaulu kujiongezea umaarufu tangu wakati huo na limemueleza kuwa kiongozi aliyeendelea kukataliwa na umma wa Marekani kwa kipindi kirefu katika historia ya leo ya Marekani.

Huku upinzani wa wabunge wa mrengo wa kulia wa chama cha Republican dhidi ya mswada wa uhamiaji ukisadia kufafanua kuanguka kwa rais Bush katika kura za maoni za hivi karibuni, Irak bado inabakia kuwa swala pekee muhimu linalomuharibia sifa rais Bush. Katika uchunguzi uliofanywa na shirika la CBS la Marekani wiki iliyopita, asilimia 23 ya Wamrekani walioulizwa walisema wanakubaliana na jinsi rais Bush anavyovishughulikia vita vya Irak, huku asilimia 70, wakiwemo wanachama wa chama cha Republican, wakisema wanapinga.

Asilimia 40 ya Wamarekani walisema wanataka wanajeshi wote wa Marekani waamriwe kuondoka Irak na warejee nyumbani, huku asilimia 26 wakitaka idadi ya wanajeshi ipunguzwe. Uchunguzi uliofanywa na shrika la habari la CNN hivi majuzi ulidhihirisha matokeo kama hayo.

Huku uchaguzi ukitarajiwa kufanyika miezi 16 ijayo nchini Marekani, wabunge wa chama cha Republican wanaendelea kufahamu kwamba rais Bush na makamu wake Dick Cheney, ambaye pia naye anapingwa na asilimia 28 ya Wamarekani, ni kikwazo katika kuzifikia ndoto zao za kisiasa. Na huku uchaguzi ukikaribia shinikizo la kuipinga ikulu ya white house utaendelea kama ilivyotokea wakati wa kuupigia kura mswada wa sheria za uhamiaji.