1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umhimu wa kujadili mzozo wa chakula katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Mohamed Dahman7 Mei 2008

Hoja zachemka kutaka suala la mzozo wa chakula duniani lijadiliwe na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

https://p.dw.com/p/Dw3D
Nchi nyingi zinahitaji msaada wa chakula kutokana na dunia kukabiliwa na mzozo wa chakula.Picha: AP

Suala la mzozo wa chakula ambalo limechochea maandamano ya mitaani na ghasia takriban katika nchi 30 ikiwa ni pamoja na Haiti,Indonesia,Ivory Coast, Mauritania, Msumbiji na Senegal na hivi karibuni kabisa nchini Somalia limeendelea kukwepwa kujadiliwa na chombo chenye nguvu kubwa kabisa cha Umoja wa Mataifa nalo ni Baraza la Usalama la umoja huo.

Baraza la Usalama litakuwa na mapungufu katika kutekeleza majukumu yake ya kudumisha amani na usalama iwapo litashindwa kuchukuwa hatua zinazohitajika mno za kinga kuzuwiya kuendelea kuwa mbaya kwa hali za usalama unaotokana na mzozo wa chakula duniani.

Anwarul Karim Chowdhry balozi wa zamani wa Bangladesh na ambaye wakati fulani aliwahi kuwa mwenyekiti wa mikutano ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa ameyaeleza hayo shirika la habari la IPS.

Chowdhry ambaye pia ni mwakilishi Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Nchi Zenye Maendeleo Duni amesema Baraza la Usalama huko nyuma liliwahi kujadili Virusi vya HIV na UKIMWI na mabadiliko ya hali ya hewa kwa kuzingatia uwezekano wa taathira zake kwa amani na usalama juu ya kwamba kulikuwa na vyombo vyengine katika mfumo wa Umoja wa Mataifa kushughulikia masuala hayo.

Baraza la Uchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa ECOSOC linapanga kuwa na mkutano juu ya mzozo wa chakula mjini New York baade mwezi huu wakati Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa FAO linaandaa mkutano wa viongozi kuanzia Juni 3 hadi 5 kujadili suala hilo mjini Rome.

Alipouulizwa iwapo mzozo huo wa chakula wa hivi sasa unapaswa kujadiliwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Balozi John Sawers wa Uingereza ambaye ni mwenyekiti wa mikutano ya baraza hilo kwa mwezi wa Mei amewaambia waandishi wa habari kuwa juu ya kwamba kuna masuala ya usalama kwa hilo la mzozo wa chakula suala hilo kwa jumla linapaswa kujadiliwa na vikao vyengine hususan cha ECOSOC.

Wakati Uingereza ilipoongoza hatua ya mwaka jana ya kuwa na mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa juu ya mabadiliko ya hali ya hewa kwa hoja kwamba kuongezeka kw aujoto duniani ni tishio la amani ya kimataifa na usalama nchi wanachama 130 wa kundi la nchi 77 zinazoendelea walipinga na kutaka suala hilo lijadiliwe na vyombo vya Umoja wa Mataifa vinavyohusika na maendeleo endelevu.

Lakini Balozi wa Uingereza wakati huo kwa Umoja wa Mataifa Emyr John Parry alikataa hoja yao hiyo na kuendelea na mkutano wa baraza la usalama chini ya uenyekiti wa Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Margaret Beckkett hapo mwezi wa April mwaka jana.

Wiki iliopita hoja hiyo hiyo ya nchi za kundi la 77 iliotupiliwa bali imetumiwa na balozi wa Uingereza John Sawers safari hii kuhalalisha mkutano wa ECOSOC juu ya mzozo wa chakula wakati akielezea mashaka ya pendekezo la mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Mwanadiplomasia mmoja wa nchi zinazoendelea akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina lake amesema huo ni mfano bora kabisa wa unafiki wa kisiasa.

Katika kipindi cha miezi michache iliopita tu watu wengine milioni 100 duniani kote wametumbukizwa kwenye utapia mlo na njaa.

Hatua ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuendelea na shughuli zake kama kawaida kwamba tatizo hilo litaondoka wenyewe inawashangaza wengi.