1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umma waongezeka katika miji mikubwa

P.Martin28 Juni 2007

Kwa mara ya kwanza katika historia ya binadamu,katika mwaka 2008 zaidi ya nusu ya umma duniani,itakuwa ikiishi katika miji mikubwa.

https://p.dw.com/p/CHBy
Idadi ya wakaazi wa mashambani inazidi kupungua
Idadi ya wakaazi wa mashambani inazidi kupunguaPicha: Ferdinando Sciana/Magnum Photos

Idadi ya wakazi huongezeka kwa kasi kubwa hasa katika miji ya nchi zinazoendelea.

Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu idadi ya watu duniani-UNPF,ifikapo mwaka 2008, zaidi ya nusu ya umma wa bilioni 6.6 duniani, itaishi katika miji mikubwa.Lakini kwa hivi sasa, miji haina uwezo wa kuwa na idadi hiyo ya watu. Mkurugenzi-mtendaji wa UNFP,Bibi Thoraya Ahmed Obaid,alipozungumza na waandishi wa habari,baada ya ripoti hiyo kutolewa mjini London alisema,miji inapaswa kutimiza mahitaji ya umma unaozidi kuongezeka.Isipofanya hivyo,itakabiliwa na vitisho vya vurugu.Amesema,pasipokuwepo mipango inayofaa,basi miji kote duniani, itapambana na kitisho cha umasikini mkubwa, itikadi kali za kidini,nafasi duni kwa vijana na hata haki za wanawake zitadhurika vibaya.

Kuambatana na ripoti ya UNFP,idadi ya wakazi katika miji inatazamiwa kufikia bilioni 5 ifikapo mwaka 2030.Mjumbe wa UNFP,Bibi Bettina Maas amesema:

“Kwa hivyo haitoshi kushughulikia changamoto za hivi sasa tu.Kinachohitajika zaidi ni kwa miji kuchukua hatua za kujikinga.Huu ni wakati wa kutenda,kwani miji ni mustakabali wa ulimwengu.”

Kwa sehemu kubwa,masikini ndio wanaosababisha idadi ya watu kuongezeka katika miji.Sasa umasikini katika miji,unaongezeka kwa haraka kuliko sehemu za mashambani.Ripoti ya Umoja wa Mataifa inasema,hivi sasa theluthi moja ya wakazi katika miji ni walala hoi,hiyo ikiwa ni watu bilioni moja.Zaidi ya asilimia 90 ya walala hoi wanaishi katika nchi zinazoendelea.

Kwa sababu hiyo,mipango ya miji inapaswa kuzingatiwa vyema,ikiwa ni pamoja na kutambua haki ya masikini kuishi katika miji.Wakati huo huo,maeneo ya mashambani nayo yapatiwe umeme na maji.

Hata waziri wa misaada ya maendeleo wa Ujerumani, Bibi Heidemarie Wieczorek-Zeul alipozungumza mjini Berlin,kuhusu ripoti ya Umoja wa Mataifa, alisisitiza umuhimu wa kuwepo jitahada zaidi katika miji.Akaongezea kuwa maendeleo katika maeneo ya mashambani lakini yasisahauliwe. Akifafanua zaidi alisema:

“Sawia,ni muhimu pia kuendeleza mikakati ya maendeleo ya miji husika,wakati wa kufanya kazi na madola shirika.Kwanza kabisa,mikakti hiyo ishirikishe jamii za kiraia,makundi ya masikini na hasa izingatie wanawake.”

Wakati huo huo,wataalamu wa UNPF wanahofia pia athari za mabadiliko ya hali ya hewa duniani. Sababu ni kuwa asilimia 13 ya miji mikubwa duniani,ama ipo sehemu za pwani au karibu na mito.