1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Afrika wajikuta njia panda baada ya Gaddafi

25 Agosti 2011

Wakati Walibya wanafurahia kuanguka kwa mji wa Tripoli katika mikono ya waasi, Waafrika katika mataifa mengi walijizuwia na furaha hiyo.Umoja wa Afrika hata hivyo haujaweka wazi iwapo utatambua baraza la mpito.

https://p.dw.com/p/12NfA
Waasi wakishangiria katika kasri la Mouamer Gaddafi la Bab Al-AziziyaPicha: dapd

Wakati Walibya wengi wakifurahia kukamatwa kwa mji mkuu wa Libya Tripoli na waasi , Waafrika katika mataifa mengi walijizuwia na furaha hiyo. Walikuwa na uhusiano wenye hisia tofauti na Gaddafi. Kwa upande mmoja Gaddafi alikuwa ni mgeni maarufu wa kitaifa kila mara anapotembelea taifa fulani, kwa kuwa alikuwa akija na mkoba wa fedha. Alisaidia sana mapambano dhidi ya ukoloni, lakini pia aliwasaidia madikteta kwa kuwapatia silaha , na pia alimsaidia rais Zuma katika harakati zake za kuingia madarakani, licha ya kuwa hilo linapingwa. Na pia umoja wa Afrika unachukua hatua za tahadhari sana katika hatua zinazotokea kila siku nchini Libya. Leo Ijumaa umoja wa Afrika unafanya kikao maalum kwa ajili ya Libya. Lakini bado hali haijafahamika wazi , iwapo viongozi wa serikali na mataifa ya Afrika watawatambua waasi wa Libya.

Matamshi ya rais wa Ghana John Atta Mills yanaonyesha wazi mshutuko mkubwa kuhusiana na hali ya Gaddafi ambayo imeuyumbisha umoja wa Afrika.

"Tunatambua kuwa baraza la usalama na amani la umoja wa afrika litakutana , lakini Ghana inachunguza hali ilivyo, na tutachukua uamuzi sahihi, ikitiliwa maanani kile ambacho ni cha manufaa kwa taifa letu".

Kiongozi mwenzake mwenye nguvu zaidi wa Afrika kusini Jacob Zuma ameonyesha hadi sasa msimamo wa wazi wakati akieleza shutuma zake kwa mashambulizi ya NATO.

Jacob Zuma Brüssel Belgien Südafrika Gipfel
Rais Jacob Zuma, wa Afrika kusini , amekuwa akiishutumu jumuiya ya NATO kwa kuishambulia LibyaPicha: picture-alliance/dpa

"Tumejikuta katika hali, ambapo mataifa yaliyoendelea yameamua kuingilia kati katika bara la Afrika, katika utaratibu ambao haujakubalika. Tumeona kuwa maazimio haya yanaendewa kinyume katika hali ambayo haikubaliki kabisa".

Zuma anaitupia lawama jumuiya ya NATO, kwa kuendesha sera za mabadiliko ya utawala na kulikandamiza jukumu la Afrika katika utatuzi wa mzozo huo. Kuhusu juhudi zake mara mbili zilizoshindwa za upatanishi mjini Tripoli hapendi sana kuzizungumzia. Gaddafi alimkaribisha Zuma katika hema alimokuwa akiishi. Ni hivi karibuni tu waziri wa mambo ya kigeni wa nigeria Ashiru alitamka wazi kuwa serikali nyingi katika mataifa ya Afrika zilikuwa zikikubaliana na Gaddafi. Miongoni mwa nchi hizo ni Zimbabwe, kuna mahoteli kadha nchini Kenya na Afrika kusini na mara nyingi chama tawala cha ANC kilipata fedha nyingi kutoka kwa Gaddafi katika mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi. kwa hiyo si jambo la kushangaza , kwamba hadi sasa mataifa hayo hayakuwaunga mkono waasi. Anakiri hivyo waziri wa mambo ya kigeni wa Afrika kusini Nkoana- Mashabane kuwa haikuwa rahisi kulikubali baraza hilo la mpito. Anatoa wito lakini.

"Tungependa kutoa wito kwa mamlaka ya mpito kuanzisha haraka mjadala wa walibya wote, wenye nia ya kuunda uwakilishi halisi wa serikali ulio katika misingi wa watu wa Libya".

Afrika kusini inasisitiza kuhusu kile kinachojulikana kama utaratibu maalum, "Roadmap", ya umoja wa Afrika, ambayo inazungumzia kuhusu mjadala wa aina hiyo, kura ya maoni kuhusu katiba na hatimaye ufanyike uchaguzi. Inawezekana kwa vyovyote vile kuwa mtazamo huu wa umoja wa Afrika ukatekelezwa. Lakini ni pale tu baraza la taifa la mpito la Libya litakapopendelea kufuata. Huenda pia Libya isiwe na haja na umoja wa Afrika.

Mwandishi : Stäcker , Claus / ZR / Sekione Kitojo

Mhariri : Yusuf Saumu