1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaNiger

Umoja wa Afrika wasimamisha shughuli zote za Niger

Sylvia Mwehozi
22 Agosti 2023

Umoja wa Afrika umeisimamisha Niger katika shughuli zake zote kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya Julai 26 na kurejelea wito wake kwa viongozi wa kijeshi kumwachia rais aliyepinduliwa Mohamed Bazoum.

https://p.dw.com/p/4VS7P
Addis Ababa
Umoja wa Afrika mjini Addis AbabaPicha: Eduardo Soteras/Getty Images/AFP

Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika, limesema katika taarifa yake kwamba limefahamu maamuzi ya Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS ya kupeleka kikosi cha dharura nchini Niger, lakini limeitaka tume ya Umoja wa Afrika kutathmini athari za kiuchumi, kijamii na kiusalama za uingiliaji kati kijeshi. Maazimio hayo yaliyosomwa katika tamko la Jumanne yalipitishwa na baraza lililoketi Agosti 14. Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS, tayari ilishaanzisha vikwazo dhidi ya Niger, vilivyoidhinishwa na Umoja wa Afrika.

Aidha, Umoja wa Afrika umerejelea wito wake kwa viongozi wa kijeshi kumwachia mara moja rais aliyepinduliwa Mohamed Bazoum ambaye anazuiliwa tangu mapinduzi na kuwataka wanajeshi hao kurejea kwenye makambi yao. Hata hivyo viongozi wa kijeshi wamekataa shinikizo la kuachia madaraka na kupendekeza kipindi cha mpito cha miaka mitatu ili kuandaa uchaguzi, mpango uliokataliwa na ECOWAS.

Berlin-Annalena Baerbock -Aissata Tall Sall
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock (kulia) na waziri wa mambo ya nje wa Senegal Aissata Tall Sall,Picha: Bernd Elmenthaler/IMAGO

ECOWAS ilisema kuwa iko tayari kuwatuma wanajeshi nchini Niger, endapo juhudi za kidiplomasia zitashindikana. Umoja wa Afrika umetoa wito kwa wanachama wake wote na jumuiya ya kimataifa kujizuia na hatua yoyote inayoweza kuhalalisha utawala wa kijeshi wa Niger. Na wakati huohuo umekataa vikali uingiliaji wowote wa nje katika mzozo huo unaofanywa na mtu au nchi yoyote nje ya Afrika, ikiwa ni pamoja na ushirikiano na makampuni ya kijeshi ya kibinafsi, wito unaoonekana kulilenga kundi la mamluki la Urusi Wagner, ambalo linafanya kazi katika nchi jirani ya Mali.

Katika hatua nyingine waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock ameunga mkono uamuzi wa ECOWAS wa kuiwekea vikwazo Niger. "Tunalaani, nalaani vikali mapinduzi ya kijeshi na tunakaribisha hatua madhubuti za ECOWAS kuhusu mgogoro wa Niger. Ujerumani na Umoja wa Ulaya zinasimama nyuma ya uamuzi wa ECOWAS wa diplomasia na kutumia shinikizo. Ili kutilia mkazo juhudi za ECOWAS, Ujerumani imesitisha malipo yote kwa Niger na sasa tunataka kushinikiza vikwazo vya mtu binafsi miongoni mwa mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya dhidi ya waliopanga mapinduzi," alisema Baerbock.

Soma pia uamuzi wa EU: Umoja wa Ulaya kuichukulia hatua kali Niger

Hayo yakijiri, Ufaransa imekanusha hii leo kwamba iliiomba Algeria kurusha ndege katika anga lake kwa ajili ya operesheni za kijeshi nchini Niger. Siku ya Jumatatu, redio ya taifa ya Algeria ilitangaza kwamba imekataa ombi la Ufaransa na kwamba inapinga hatua za kijeshi za nchi za kigeni katika kurejesha utulivu nchini Niger, ikiegemea diplomasia zaidi.