1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Afrika yaiwekea vikwazo Madagascar

Kabogo Grace Patricia17 Machi 2010

Vikwazo hivyo ni pamoja na kunyimwa visa viongozi walioko madarakani na kutaifishwa kwa mali zao katika benki za kigeni.

https://p.dw.com/p/MV93
Kiongozi wa Madagascar, Andry Rajoelina.Picha: picture-alliance/ landov

Umoja wa Afrika umewawekea vikwazo viongozi wa Madagascar walioko madarakani hii leo kutokana na viongozi hao kwenda kinyume na wito uliotolewa na umoja huo wa kutekeleza mikataba ya kumaliza mgogoro wa kisiasa uliodumu kwa mwaka mmoja sasa. Tarehe 16 ya mwezi Februari mwaka huu, Umoja wa Afrika wenye nchi wanachama 53 ulitoa muda wa mwezi mmoja kwa kisiwa hicho kilichopo Bahari ya Hindi kinachoongozwa na Andry Rajoelina, kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa mwaka uliopita baada ya mfululizo wa mazungumzo baina ya kiongozi huyo na mahasimu wake wa kisiasa. Kamishna wa Amani na Usalama wa Umoja wa Afrika, Ramtane Lamamra amesema kuwa vikwazo hivyo vilivyotangazwa hii leo vimewekwa dhidi ya Rajoelina na wafuasi wake 190.

Akiulizwa jinsi wananchi wa kisiwa hicho walivyoipokea taarifa hiyo ya  vikwazo, mwanasheria na mshauri wa zamani wa Umoja wa Afrika kuhusu Madagscar Jean-Enrique Rakotoarsu aliiambia Deutsche Welle kutoka mjini Antananarivo kuwa, ''Ni vigumu kufahamu lakini kwa maoni yangu binafsi ni kwamba Madagascar inajitumbukiza katika hatua ya kujiua yenyewe kisiasa kwa sababu umma umeanza kujirudi na kuupinga utawala uliopo madarakani. Kwa sababu kwa hakika tunaishi katika hali ngumu ya kiuchumi, kuna watu kadhaa wamepoteza nafasi zao za kazi na pia tunaishi katika hali ya ukosefu wa usalama.''

Rajoelina aliyechukua madaraka huku akiungwa mkono na jeshi la Madagascar mwezi Machi mwaka uliopita wa 2009, alikataa kugawana madaraka na marais watatu wa zamani wa nchi hiyo na badala yake alitangaza kuandaa uchaguzi. Mwanzoni mwa mwezi huu, Rajoelina alikataa mualiko wa Umoja wa Afrika wa mazungumzo na mahasimu wake kwenye makao makuu ya umoja huo yaliyopo mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Balozi wa Uganda kwenye Umoja wa Afrika, Mull Sebujja Katende, alisema mwezi uliopita kuwa umoja huo utaiwekea vikwazo Madagascar, ingawa hakufafanua zaidi ni vikwazo vya aina gani ambavyo vitawekwa dhidi ya nchi hiyo. Rajoelina, mwenye umri wa miaka 35, aliongoza maandamano ya wiki kadhaa nchini humo ya kumuondoa madarakani Rais Marc Ravalomanana, lakini chama chake kimeshutumiwa na jumuiya mbalimbali za Afrika na mataifa mengine yenye nguvu duniani.

Wakati huo huo, vikosi vya jeshi la Madagascar vimetumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji wanaoupinga uongozi wa Rajoelina. Makundi madogo madogo ya waandamanaji walijaribu kuziba barabara kwa kutumia mawe na matofali katika mji mkuu wa nchi hiyo, Antananarivo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE)

Mhariri:M. Abdul-Rahman